03/05/2020 JUBILATE – MPIGIENI BWANA KELELE ZA SHANGWE MADA: MAISHA MAPYA NDANI YA KRISTO YESU

KKKT DAYOSISI YA KUSINI,JIMBO LA NJOMBE, USHARIKA WA UWEMBA,
MTAA WA MJIMWEMA

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 3 BAADA YA PASAKA TAREHE 03/05/2020

JUBILATE – MPIGIENI BWANA KELELE ZA SHANGWE

MADA: MAISHA MAPYA NDANI YA KRISTO YESU

MASOMO: ZABURI 107: 25 – 32, MATHAYO 9:14 – 17, *ISAYA 25: 1 – 8

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa Ndani ya Yesu yanapatikana maisha ya ushindi hivyo wamtegemee daima.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, Jumapili ya leo tunajifunza juu ya maisha mapya ndani ya Kristo Yesu. Kwa tafsiri yangu juu ya mada hii ni kuwa yapo Maisha ndani ya Yesu ambayo kila mmoja hapa anayo na pia kuna maisha mapya ndani ya Yesu Kristo ambayo baadhi yetu tunayo maisha hayo.

Naweza kusema Maisha ndani ya Yesu Kristo ni maisha yale ya mazoea ambayo unatambua kuwa Yesu yupo, na umesikia akitenda mambo ya ajabu lakini hilo halikuzuii wewe kutenda kwa kiburi, dharau na majivuno.

Na Maisha mapya ndani ya Yesu Kristo ni maisha yenye mabadiliko, maisha yanayomtegemea Mungu na kuziona nguvu zake zikitenda kazi. Yaani ni maisha yenye mafanikio yanayotambua kuwa Mungu ameahidi kutufundisha ili tuweze kupata faida. (Isaya 48:17)

Katika kusindikiza mada tuliyopewa leo ya Maisha Mapya ndani ya Kristo Yesu tumepewa neno la Mungu kutoka Isaya 25: 1 -8 ambapo tunajifunza mambo kadhaa ambayo ni:-

1. LENGO LA MUNGU KURUHUSU ADHABU KATIKA MAISHA YETU NI ILI TUKUMBUKE UWEPO WAKE NA KUMUABUDU.
Kama nilivyoeleza kwenye utangulizi kuwa maisha ndani ya Mungu ni maisha ya mazoea, sasa Mungu anapotaka kuondoa haya mazoea anaruhusu adhabu kidogo ili tuweze kumkumbuka na tumsifu.

Isaya hapa anazungunza katika wimbo wake wa shukrani kuwa Mungu ameviharibu vitu ambavyo wanadamu walivijenga kwa kiburi chao na uwezo wao, maisha yamekuwa ni uchungu mtupu na miji ya kifahari imekuwa magofu hakuna wakaaji kabisa na kwa hilo mataifa watishao wataogopa lakini lengo lake lipo kwenye ule mstari wa tatu ambalo ni ili watu walio hodari katika hali hii wabaki wakimtukuza Mungu.

Kipindi hiki ambacho tunapitia hatari hii ugonjwa huu wa Corona ni kipindi ambacho tunaona kweli maisha yamekuwa machungu, miji mikubwa inabaki kuwa magofu watu wake wanakufa kweli na hata kwetu na mataifa makubwa yanayotisha yannaogopa sana sitaki kusema hili ni pigo kutoka kwa Mungu ili tumrudie ila nasema kwa kupitia hili watu wengi wamemrudia Mungu na wale walio hodari hata katika shida hii hawataacha kumtukuza Mungu.

2. MAISHA MAPYA NDANI YA YESU KRISTO NI MAISHA YA MABADILIKO
Maisha mapya ndani ya Kristo Yesu ni maisha ambayo yanashuhudia mabadiliko kila siku ni maisha ambayo mtu anashuhudia nguvu za Mungu na kuzikiri kweli kweli.

Neno la Mungu katika Isaya linaonyesha wazi kuwa ni maisha ambayo yanatoa nafuu kwa wote wanaoteswa ( ni ngome kwa maskini mhitaji katika dhiki yake, mahali pa kukimbilia wakati tufani) kuwanyamazisha watesi wote wanaojishughulisha na maisha ya watu wa Mungu.(Wale wanaoshangilia kwa kututesa sababu wanaona wameshinda hakika watashushwa)

3. MABADILIKO YA KWELI YANALETA FURAHA KWA MUNGU INAYOLETA MAFANIKIO KATIKA MAISHA YETU
Kama nilivyoeleza tangu awali kuwa maisha mapya ndani ya Kristo Yesu ni maisha yanyoleta mabadiliko na mabadiliko hayo yanapokuwa ya kweli yanaleta mafanikio katika maisha yetu.

Neno la Mungu katika Isaya linaeleza wazi kuwa Mungu atafanya sherehe na wote wanaomtegemea na katika sherehe hiyo Mungu atafanya mambo kadhaa ambayo ni:-

a) Atawaharibu maadui zetu wote

b) Atafuta machozi yote

c) Ataondoa huzuni tote

d) Ataiondoa aibu yote iliyotukabili

e) Ataondoa kifo hata Milele.

Kipindi hiki tumeitwa sana katika kutubu ili Mungu atuondolee ugonjwa huu wa Covid-19 na tukihimizana kurejea kitabu cha Mambo ya Nyakati wa pili 7:14. Ukweli unabaki kuwa toba inahitaji mabadiliko ya kwelikweli ili mabadiliko hayo yaweze kutuondolea adui yetu huyu, kutufuta machozi, kutuondolea huzuni na hata aibu ambayo inaonekana kwetu kwa sababu tumeruhusu ibada kuendelea.

Mabadiliko ya kweli ya rohoni na mwilini. Mwilini tukifuata ushauri wa wataalamu kukabiliana na adui huyu mkubwa kwa sasa Covid -19 kama vile kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa, kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, kutokuwa na safari zisizokuwa na sababu ya msingi nk
Rohoni tukiendelea kumuomba Mungu kwa nguvu zetu zote na uwezo aliotujalia, tukitubu na kumkataa shetani na kazi zake zote na mambo yake yote.

HITIMISHO
Tuendelee kumtegemea Mungu na kumtumikia kwa uaminifu na hakika upya wa maisha yetu ndani ya Yesu Kristo utaonekana kwa mafanikio.
AMEN.
@Evjohn
0768386606