MAHUBIRI YA JUMAPILI TAREHE 28/06/2020

Somo:NEEMA YA MUNGU ITUOKOAYO
Masomo:
Zaburi 59:1-9
Matendo 11:1-15
*Luka 8:26-39

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa ili kupata ahadi za Mungu tunapaswa kumtegemea Mungu.

“Kwa kuwa mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea” (Lk 19:10)

UTANGULIZI: Leo ikiwa ni siku ya tatu baada ya utatu tunaangalia mada izungumzayo juu ya Neema ya Mungu ambayo inatuwezesha sisi kuupata wokovu.

> Neema maana yake ni mafanikio aliyonayo mtu kutokana na majaaliwa ya mwenyezi Mungu au kwa juhudi zake mwenyewe.

> Hivyo:- tunaweza kusema kuwa leo tunazungumzia juu ya mafanikio aliyonayo mtu kutoka kwa mwenyezi Mungu ambayo yanaleta wokovu katika maisha ya mtu.

> Katika kutafakari Neema hii ya Mungu iletayo wokovu tumepewa kisa kutoka katika biblia Luka 8:26 – 39. Kisa hiki ambacho kimeelezwa hapa pia kimeelezwa katika kitabu cha mathayo 8:28-34 na kitabu cha Marko 5:1-20 ikizungumza habari ya mtu aliyepagawa na pepo wachafu ambao wamejitambulisha kwa jina la Legion maana yake ni jeshi kubwa la warumi lenye nguvu lililokwa na idadi ya wanajeshi 6000.

Katika kisa hiki unajifunza mambo yafuatayo:-

SHETANI NI MHARIBIFU

Mtu huyu ambaye amepagawa nna pepo tunaambiwa kuwa alikuwa Uchi, aliishi makaburini, na alikuwa akijikatakata na mawe (Marko 5:3) Shetani anapoingia kwetu hahurumii hata miilil yetu atatutaabisha na kuwa wahitaji wakati wote.

ULINZI WA KIBINADAMU HAUJITOSHELEZI

Mtu huyu alifungwa kwa pingu na hata kwa minyororo ila aliikata yote na wanadamu wakakata tama nay eye na kumuacha alivyo. Unaweza kutegemea wanadamu wanaweza kukusaidia ila ni kwa kitambo kidogo na utabaki katika shida yako.

BINADAMU WENGI WANAANGALIA KITU KULIKO UTU

Tunaelezwa kuwa baada ya mtu huyu kuponywa watu wa mji ule walimfukuza Yesu kwa sababu walipiga hesabu ya hasara ya nguruwe 2000 waliofia majini waliona mwenzao amepata hasara kubwa sasa hawakujua nani angefuata wakaogopasana wakaamua kumwambia aondoke kwao.

MUNGU ANAJISHUGHULISHA NA MAHITAJI YETU

Yesu alivyoona kuwa mtu huyu yupo uchi, anaishi makaburini mbali na watu na alikuwa akijikata mwili kwa mawe alijua kuwa anahitaji msaada hivyo aliona nguruwe hawana umuhimu kama mtu wake akayaelekeza mapepo kwa nguruwe na kumponya yule kijana. Mapepo yalikwepa kwenda kuzimu yakidani kuwa yakiingia kwa nguruwe yatakuwa salama ila baada ya kuingia nguruwe walikufa wote na mapepo bado yakaenda kuzimu.

UKIMKUBALI MUNGU UTAKUWA SALAMA

Baada ya mtu huyu kuponywa alitulia chini ya miguu ya Mungu akiwa amevaa nguo na akiwa na akili yake timamu. Amani ya kweli inapatikana kwa kumkubali Yesu

MEMA ANAYOKUTENDEA MUNGU ANATAKA UMTUMIKIE

Mtu aliyeponywa alitaka kandamana na Yesu ila yesu alimwambia aende kuelezea habari njema za Yesu kwa watu wa nyumbani kwake kwa kuwa eneo lile liikuwa ni eneoo la wapagani nao waone wema wake. Baraka tunazopata tunatumwa tukahubiri.

HITIMISHO

Bora kuwa mlinzi wa getini kwa Mungu kuliko kuwa mfalme au malkia nje ya Mungu sababu huko hakuna mafanikio ya kweli, mafanikio ya kweli yaletayo wokovu yanapatikana kwa Mungu tu.

MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 21/06/2020

siku ya 2 baada ya utatu

SOMO: TUKAE PAMOJA KWA UMOJA
MASOMO Yohana17:20-21
?Efeso 5:8-14
? Zaburi 133

UTANGULIZI
• Jumapili ya Leo ni sikukuu kubwa ya KKKT, tuanze mafundisho yetu ya leo kwa kumtakia ndugu yako heri ya siku kuu.
• Leo ni jumapili ambayo tunaazimisha kuunganika kwa makanisa saba ya Kilutheri Tanganyika ambayo ni:-
a) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Iraqw
b) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la kaskazini mwa Tanganyika
c) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kaskazini Magharibi mwa Tanganyika
d) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kati mwa Tanganyika
e) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Kusini mwa Tanganyika
f) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara Digo
g) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Uzaramoni – Uluguru

• Makanisa haya saba yalipoungana yalikwa na washarika laki tatu (300,000) tarehe 19/06/1963 hadi kufikia leo hii kanisa moja la Kilutheri lina zaidi ya dayosisi 25 na waumini zaidi ya milioni sita. (6,000,000)
• Siku ya leo tunaadhimisha miaka mia moja na thelathini (133) ya ulutheri Tanzania.
• Mwaka huu neno linalosindikiza sikukuu hii ni kutoka YOHANA 17;20-21 ambalo linaendelea kukaza juu ya umoja katika kanisa.
• Mlango huu wa 17 ni mlango wenye sala ya Yesu, kwanza anaanza kwa kujiombea yeye mwenyewe, kisha anawaombewa wanafunzi wake na anahitimisha kwa kuwaombea waumini wote wawe na umoja.
• Kipengele tulichosoma kinatufundisha mambo kadhaa

1. YESU NDIE MWANZILISHI WA KANISA
• Aliwaita wanafunzi na kuwaandaa kwa kazi maalumu ya kulihubiri neno lake ( Marko 3:14)
• Aliwaandaa kuifanya kazi aliyokuwa anaifanya yeye mwenyewe
• Aliwataka wawe na umoja ili waweze kuwa na lengo moja
• Maswali ya kujiuliza sisi wenyewe
a) Wewe umeandaa watu wa kufanya kazi ambayo unaifanya?
b) Je, wewe katika kazi/ huduma unayoifanya unazingatia umoja? Au unatengeneza makundi?

2. LENGO LA YESU NI KUONA KANISA MOJA
• Mungu anawataka waumini wote wawe na umoja na kuweka tofauti zao pembeni(Yesu anajua kuwa tunazo tofauti ila tukubali kuziweka pembeni na kuwa na umoja katika lengo moja)
• Umoja huu anataka ufanane na umoja wa Mungu na Yesu yaani umoja usio wa Kinafiki, umoja ambao hauwezi kutenganishwa. ( Umoja wetu katika utofauti wetu ufanye hata watu kushangaa tumeweza vipi kuwa wamoja)
• Umoja huu uwe ni umoja uliofungwa katika upendo wa kweli ( Yohana 13:34 – 35)
• Swali la kujiuliza waumini wale wanaojitenga na ibada kama vile kutokuwa kundini na kuanzisha madhehebu mengine bado Yesu anawahesabu kama wanafunzi wake? Wengine hata kukwepa majukumu ya kazi za umoja kama vile sadaka za umoja nk ni wafuasi wa Yesu Kweli?

3. UMOJA WA KIKRISTO UWE UMOJA WENYE MALENGO
• Umoja huu unapaswa uwe umoja unaoendelea kukua kama tulivyoona historia ya kanisa letu.
• Umoja huu uwe ni umoja wenye imani moja
• Umoja huu uwe ni umoja unaoendeleza utukufu wa Mungu ulimwenguni kote.
• Umoja unaosogeza waumini wote kuwa familia moja, kijiji kimoja. Tukitambua kuwa Yesu ndie mwanzilishi wa utandawazi ( Matayo 28:19 – 20, Mdo 1:8)
• Kanisa la Kiinjili la Kilutheri kwa kutambua kwamba misioni ya Bwana Yesu inaendelea kukua na kupanuka imeendelea kujitahidi kuleta umoja kwa kuweka uwiano wa sadaka za umoja ili kukidhi hitaji hili ambazo zinafanya kazi ya:-
a) Kutuma wachungaji maeneo ya misioni ya ndani na nje ya nchi
b) Kuhisani masomo ya wanafunzi wanaotoka maeneo ya misioni
c) Kuendesha vituo vya kazi za umoja kama vile Ofisi kuu ya kanisa, Shule ya viziwi mwanga na Njombe, Radio sauti ya injili, Seminari ndogo ya Morogoro nk.
Mimi na wewe tumeshiriki vipi katika misioni hii ya Yesu?

HITIMISHO
• Roho mtakatifu atusaidie kutambua kusudi la Yesu kwa kanisa lake nasi kama wafuasi wa kweli tuungane kwa upendo kuliendeleaza kanisa la Mungu.
• Umoja ni silaha kubwa sana katika huduma yetu ya uinjilisti. Ubora wa ushirikiano wetu unawavuta watu wengi kwa Mungu na udhaifu wa umoja wetu unalitawanya kundi la Mungu na kulipoteza huku ushuhuda wetu ukiendelea kuwa dhaifu
• Tuwavute watu kwa Mungu kwa kudumisha umoja miongoni mwetu.
AMEN.

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 1 BAADA YA UTATU TAREHE 14/06/2020

MADA: MUNGU AU ULIMWENGU

MASOMO:
ZABURI 78: 17 – 22
YOHANA 7:40 – 52,
MATENDO YA MITUME 5: 34 – 42

SHABAHA: Wasilkilizaji waweze kutambua kuwa uchaguzi sahihi nu ule wa kuchagua Mungu kwa sababu wakati wote yupo sahihi.

UTANGULIZI
Biblia inatufundisha kuwa Mungu sio nguvu Fulani tu inayomuwezesha mwanadamu kufanya jambo Fulani bali ni nafsi hai na hili huonekana wazi mtu unapokubali kumjia yeye na kupata mahusiano na ushirika nae (Yn 17:3)

Mungu ni nafsi hai iliyojidhihirisha kwenye nafsi tatu ili kumsaidia mwanadamu asibaki tu na ujuzi mdogo au hisia tu.(Yer 1:1 – 3, 2Pet 1:21)

Mungu ni wa milele asiyetawaliwa. Hawezi kupimwa kwa kipimo cha wakati, kwa sababu yeye hana mwanzo wala mwisho (Zab 90:2, Isa 48:12, Yn 5:26) Hana haja ya kutoa hesabu mahali popote wala kwa kiumbe chochote na hana haja ya kutoa sababu kwa uamuzi wake wala kuelezea matendo yake (Zab 115:3, Mdo 4:48) ingawa katika neema yake mara nyingine anafanya hivyo (Mwa 18:17 – 19, Efe 1:9) Hekima yake haina kikomo na hivyo iko nje ya uwezo wa mwanadamu ( Zab 50: 10 – 13, Mdo 17:24 – 25) Jambo lolote analolitenda analitenda kwa sababu ameamua hivyo, wala si kwa sababu alilazimika kufanya hivyo (Efe 1:11)
Mungu ni mwenye enzi na mamlaka yote. Hakuna kikomo kuhusu kuwepo kwa Mungu au ujuzi wake. Jambo hili ni kweli kwa furaha na hofu. Kwa furaha sababu hakuna mtu amtegemeaye ataweza kutengwa naye; na kwa hufu kwa sababu hakuna dhambi inayoweza kufichwa mbele zake ( Zab 139: 1 – 12, Ebr 4:13).

Mungu habadiliki lakini anajibu na kuitikia, Mungu asiyebadilika maana yake hana kikomo wala mwanzo wala mwisho hivyo hana namna ya kuongeza au kupunguza hali na sifa zake. (Kut 34:6 – 7) kutokubadilika kwa Mungu kuna maana kuwa yeye ni thabiti katika matendo yake yote(Ebr 6:17 – 18, Yak 1:17)

Biblia inaeleza ulimwengu ni vitu vilivyoumbwa na Mungu au watu wanaoishi katika ulimwengu (Zab 90:2, 98:7,9) kwa sababu ya dhambi ulimwengu ulikuwa sehemu ambamo shetani anatawala katika maisha ya watu (Yn 12:31, Rum 5:12 1Yoh 5:19) mara nyingi biblia inasema juu ya ulimwengu kuwa ni jambo lililo ovu au kinyume cha Mungu (Yn 7:7, Yak 4:4). Ulimwengu katika maana hii ni jambo la wanadamu wenye dhambi pamoja na tabia mbaya zilizo alama za wanadamu wenye dhambi.

Mkristo hawezi kushinda majaribu ya ulimwengu kwa kutumia mbinu za ulimwengu. Njia moja tu ya kushida ulimwengu ni kutegemea nguvu ya Kristo, aliyemshinda shetani aliye mkuu wa ulimwengu huu (Yn 12:31, 1Yoh 5: 4 – 5)
Kwa kuzitegemea nguvu za Mungu wanadamu wanao uwezo wa kuushida ulimwengu na kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Wote tunaalikwa kati ya Ulimwengu na Mungu basi tuchague Mungu Huku tukifahamu haya ambayo neno la Mungu linatufunza katika somo nililolisoma kuwa:-

1. KAZI YA MUNGU HAIHITAJI KUJIHURUMIA KULIKO KUMTEGEMEA YEYE
 Wanafunzi wakiwa na ujasiri wa hali ya juu pamoja na kutambua wivu uliotawala kwa ajili ya mafanikio yao, huku wakiwa wamepigwa marufuku kali kufundisha kwa kutumia jina la Yesu na ufufuo wake na wakitambua mamlaka ya baraza lile na uwezo wa wanachoweza kuwafanyia hata kuwaua ila waliendelea kuwaeleza wazi kuwa wao ndio waliomuuua Yesu pasipo kujali nini kitawapata kutokana na ukweli huo.

 Hii ndio kazi ya wakristo wote kutokufungia macho uonevu unaojitokeza na kueleza ukweli wote kwa yeyote pasipo kujali chochote ambacho kinataka kukuondoa kwenye imani ya kumtegemea Mungu

2. UKIWA NA UHAKIKA NA NGUVU ZA MUNGU MAMBO YA DUNIA HAYAWEZI KUYUMBISHA IMANI YAKO
 Jumapili iliyopita tulijifunza juu ya Farisayo aitwae Nikodemu ambaye alikuwa mwanafunzi wa siri wa Yesu Kristo ambaye alikuwa mwalimu wa torati, tajiri na aliyeheshimika na sasa wanafunzi wake wanapoanza huduma tunakutana na Mfarisayo mwingine ambaye ni mwalimu wa torati, tajiri na aliyeheshimika sana ambaye anaonyesha anakuballiana na mafundisho ya Yesu na anatoa maamuzi ya hekima kuwa mambo amabyo yameanza ambayo asili yake sio Yesu Kristo basi hufa ila kama yameanzishwa na msingi wa Yesu Kristo kamwe hayawezi kuvunjika na ni hatari kupambana nayo. Na Ushauri huu unapokelewa.

 Yanaweza kutokea mambo ambayo huyaelewi ila kwa vile una uhakika na nguvu za Mungu basi mwachie Mungu mwenyewe ni hakimu mwenye haki.

3. HATUHITAJI KUWAOMBEA MABAYA ADUI ZETU
 Wanafunzi wanachapwa viboko na wanapoachiwa wanaondoka kwa furaha kuwa wamehesabiwa mateso kwa ajili ya Yesu na wanadumu wakiomba na kufundhisha juu ya uweza na Mungu huku wakitambua kuwa ulimwengu hauwezi kuwafanya chochote.

 Adui zetu wakikaza kutuudhi nasi tuzidi kuongeza kiasi cha furaha yetu tukitambua kuwa nguvu za Mungu zitatupatia haki yetu.

HITIMISHO
Mungu atuwezeshe tuweze kumtumikia kwa uaminifu na ujasiri pasipo kuogopeshwa na vitisho vya wote wanaoukataa ukweli pasipo kujihurumia sababu Mungu mwenyewe asiyetawaliwa wala kubadilika atatulinda daima.

MUHUTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 07/06/2020

MUHUTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 07/06/2020

SIKU YA UTATU MTAKATIFU: BABA, MWANA NA ROHO MTAKATIFU

ZABURI 118:24-29
1wakoritho3:10- 12,
YOHANA 3:1-15

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kutambua kuwa Mungu anapenda wote wawe na umoja kama yeye alivyo mmoja katika nafsi tatu.

1. UTANGULIZI
• Nitaanza somo letu leo kwa kueleza kwa Ufupi utatu ni nini.

2. UTATU NI NINI?
• Utatu mtakatifu ni hali ya kuwa Watatu katika umoja kamili. Jina hilo linatumika hasa kufafanulia imani ya Wakristo wengi kwamba Mungu pekee, ni nafsi tatu zisizotenganika kamwe Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

• Katika Biblia, Kwa agizo la Yesu watakaomuamini wanatakiwa kubatizwa kwa jina la hao watatu (Injili ya Mathayo28:19). Agizo hilo la mwisho lilifuata na kujumlisha mafundisho yake mbalimbali kuhusu Baba, kuhusu yeye mwenyewe kama Mwana na kuhusu Roho Mtakatifu.

• Ufafanuzi wa kitheolojia, Umoja wa Nafsi hizo unatokana na asili yake pekee, yaani Baba ambaye ndani mwake anamzaa Mwana kama mwanga toka kwa mwanga, kama Neno au Wazo lake (Hekima), tena anamvuvia Roho Mtakatifu kama Upendo ambao unamuunganisha na Mwana na kukamilisha umoja wao.

• Katika matamko rasmi ya Kanisa, Imani hiyo ilizidi kufafanuliwa hasa katika karne IV, mitaguso mikuu ya kwanza ilipochukua msimamo dhidi ya wazushi waliokanusha uungu wa Yesu na wa Roho Mtakatifu. Ilipata muundo wa kudumu katika Kanuni ya Imani ya Nikea-Konstantinopol iinayotumika hadi leo katika madhehebu mengi ya Ukristo.

• Kwa imani hiyo tunapaswa kusadiki hasa Utatu wa Mungu pekee, kwamba ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Milele yote Baba kwa jinsi alivyo ndani mwake anamzaa Mwana na kumvuvia Roho Mtakatifu, kama vile jua linavyotoa mwanga na joto lisitenganike navyo. Mwana, ambaye “ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake” (Eb 1:3), alisema: “Nimekuja kutupa moto duniani” (Lk 12:49). Naye Roho aliwashukia wafuasi wake “kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu” (Mdo 2:3-4).

• Mungu hagawanyiki hata kidogo, bali daima ni Umojakamili. “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” (Mk12:29). Tumuabudu yeye peke yake katika nafsi tatu, na Utatu wa nafsi katika Umoja wa hali yake, tusichanganye nafsi wala kugawa Umungu. Baba si Mwana wala Roho Mtakatifu. Mwana si Baba wala Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu si Baba wala Mwana. Lakini milele yote nafsi hizo tatu ni Mungu yuleyule pasipo tofauti ya kuzitenganisha: kila moja imo ndani ya nyingine. “Mimi na Baba tu umoja” (Yoh10:30).

• Tumejua kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu kwa sababu Baba aliwatuma kwetu Mwanae na Roho Mtakatifu. “Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, ‘Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye’” (Math 3:16-17). Naye akaagiza, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu” (Math 28:19). Ni nafsi tatu zenye jina moja, yaani Umungu mmoja tu.

• Umoja wa Mungu unategemea hasa kwamba Mwana na Roho Mtakatifu wanachanga Umungu wa Baba, ambaye wanatokana naye pasipo utengano wowote. Baba anajifahamu na kujipenda: wazo analojifahamu ndiye Mwana, upendo anaojipenda katika wazo hilo ndiye Roho Mtakatifu. “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yoh 17:24).

• Nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji, kila nafsi akiuchangia kulingana na sifa yake maalumu ndani ya Utatu. Baba Mwenyezi sifa yake ni Uwezo. Mwana kama Neno la Baba sifa yake ni Hekima. Roho kama Pumzi ya uhai ya Baba sifa yake ni Upendo. Katika Uwezo wake Baba anafanya yote kwa Hekima na Upendo, hasa katika utume wa Mwana aliyefanyika mtu na katika utume wa Roho kama paji. “Amin, amin, nawaambia: Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile” (Yoh 5:19).

4. MUNGU ANATAKA UMOJA WA KANISA UIGE MFANO WA NAFSI TATU ZA MUNGU
• Ule utukufu ambao Yesu alikuwa nao kabla hajaja duniani wa kumuona baba na Roho mtakatifu ambao anamuomba Baba amrudishie atakapo kuwa mbinguni ndio anaouomba utukufu huo ulikalie kanisa lake, wote wawe na Umoja na tabia zote za Ki- Mungu, tabia zilizo njema ambazo ni Upendo, Utakatifu, haki, rehema nk.

• Umoja wa nafsi za Mungu kama nilivyoeleza ni umoja ambao hautenganishwi kamwe hivyo ndivyo ambavyo Mungu anataka kuona kanisa lake linakuwa na umoja.
5. UMOJA TULIONAO MUNGU ANATAKA TUUIMARISHE ZAIDI
• Yesu anaomba umoja wetu upate kukamiika ili wanafunzi wajue kuwa Mungu anawapenda sana kama jinsi anavyompenda Yesu na wanapaswa kushikwa na upendo ule ule ambao Baba na Mwana wanao ili utukufu wake uzidi kudhihirika na ulimwengu ujue nguvu zake.

• Umoja ulionao na mwenzako kama mmoja wa kiungo cha kanisa la Mungu umetawaliwa na Upendo wa kweli? Mungu anatutaka pamoja na umoja pia tuwe na upendo wa Kweli miongoni mwetu.

6. UMOJA NA UPENDO WETU UTUWEZESHE KUITIMIZA KAZI YA MUNGU
• Yesu Kristo anawataka wanafunzi wake kuifanya kazi yake ambayo anaianzisha pale msalabani ya kumkomboa mwanadamu wawe wainjilisti wazuri katika kuifanya kazi ya Mungu na kulinda Umoja wa kanisa wakati wote wa huduma yao.

• Mungu anakutaka na wewe kuendelea kazi hii njema ya kuhakikisha kanisa linaongezeka kukua huku likidumisha umoja na Upendo.

7. HITIMISHO
• Mungu mmoja mwenye nafsi tatu atuwezeshe tuweze kuwa na umoja wa kweli ulio tawaliwa na Upendo Miongoni mwetu.

AMEN.