Category Archives: Korona update

ASKOFU SHOO,MUNGA NA MALASUSA WATOA NENO JUU YA COVID19

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo pamoja na Maaskofu Dk. Alex Malasusa na Stephen Munga
wametoa maagizo kwa washarika katika kuukabili ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Dayosisi wanazoziongoza Maaskofu hao pia wameagiza Wakristo kuoba kwa bidii juu ya ugonjwa huo.

Mkuu wa Kanisa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, aliesme kuwa pamoja na yote yanayoendela kamwe Kanisa hilo halitaacha kumuabudu Mungu.

“Naomba ifahamike kuwa, pamoja na yote endapo ugonjwa huu utaendelea japo siyo ombi letu, tupo tayari kufanya mabadiliko ya taratibu zetu za Ibada lakini hatutuacha kumwabudu Mungu,” alisema Askofu Dk. Shoo.

Akihubiri kwenye Ibada ya kumuingiza kazini Mkuu mpya wa jimbo la Hai, Mch. Biniel Mallyo Askofu Dk. Shoo alisema kuwa huu ni wakati wa kumkaribia Mungu, kwa kuwa inaonekana kwa nguvu na akili za kibinadamu, hatuwezi zaidi ya kimkimbilia yeye.

“Niwasihi kila mmoja wetu kuacha hofu na tung’ang’ane kwa kufanya maombi ya toba kwa Mungu wetu,” alisema Askofu Dk. Shoo.

Mkuu huyo wa Kanisa aliwapa matumaini Watanzania, akieleza kuwa ugonjwa huo utapita maana Mungu amesema atatulinda dhidi ya mauti na magonjwa.

Aliwasihi Wakristo kuwaombea watumishi wa sekta ya afya ili wasiathirike pindi wanapotoa huduma kwa wale waliothibitika kuugua ugonjwa huo.

Aidha Askofu Shoo alisema Kanisa hilo litafanya maombi maalum yanayofanana ili kumsihi Mungu aliepushe Taifa na ongezeko la virusi vya corona na katika Ibada hiyo makundi mbalimbali yalifanya maombi maalumu ya kuomba toba kwa Mungu.

MUNGA ATAKA MAOMBI YA KUFUNGA

Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (DKMs), Dk. Stephen Munga ameandika waraka maalumu ambao umesambazwa kwenye Sharika zote za Dayosisi hiyo, juu ya hatua za kuchukua kuhusiana na ugonjwa huo unaotajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa ni janga la dunia.

“Ninaandika waka huu kwenu nikijua kwamba ulimwengu kwa ujumla na Taifa letu linapita katika kipindi kigumu cha mapambano dhidi ya gonjwa la COVID 19,” alisema Askofu Dk. Munga kupitia waraka huo.

Kupitia waraka huo, Askofu Dk. Munga alinukuu maneno ya Mungu kutoka kitabu cha Yeremia 17: 14 unaosema; “Uniponye ee Bwana nami nitaponyeka, uniokoe nami nitaokoka kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.”

Aidha Mkuu huyo wa DKMs alionya juu ya watu wanaopuuza ugonjwa huo na kuwatahadharisha kuwa makini na manabii wa uongo wanaotaka waone kuwa ugonjwa huo siyo kitu. “Ieleweke kwamba tunashughulika na janga.”

Alitoa wito wa maombi kwa wanakanisa na kutubu katika kipindi hichi cha kwaresma.

“Nawaalika wana DKMs kuungana na watakatifu wengine hapa Tanzania na duniani katika kuomba na kufunga,” ulisema waraka wa Askofu na kuongeza;

“ Tena kwa sababu tumo katika kipindi cha Kwaresima hembu tukumbushwe kuingia ndani zaidi katika roho ya toba.

Tumuombe Mungu msamaha wa dhambi zetu, msamaha wa dhambi za Taifa letu na dhambi ya ukengeufu wa ulimwengu wa kumuacha Mungu na kujivunia maarifa na nguvu za wanadamu,” iliongeza sehemu ya waraka huo wa Askofu Dk. Munga.

Askofu Munga alisema kuwa maombi hayo yafanyike katika siku zote zilizobaki za majira ya Kwaresma ba kuhitimishwa katika siku ya pili ya Pasaka.

MALAUSA: TOMBE KWA ROHO, TUOMBE KWA AKILI

Naye Askofu Dk. Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliwaambia washarika wa Dayosisi hiyo kuwa ni lazima wajitunze kwa kuzingatia wataalamu wa afya wanavyosema.

“Tusisubiri viongozi wa serikali ndiyo watuambie namna ya kutunza hekalu la Bwana, sisi ni lazima tutunze usafi wetu, kwa hiyo tunapoambiwa kunawa, tusisalimiane hayo ni mambo ambayo sisi tunatakiwa tuwe mstari wa mbele na kuwa mabalozi wa kuyafanya hayo.

“Tunaposema kuwa tunapunguza makusanyiko ya katikati ya wiki siyo kwamba hatutaki Ibada, lakini kwa sababu ya hali halisi ilivyo imebidi tusimame kidogo si kwamba hatuzipendi na si kwamba hatutaki kumuabudu Mungu lakini tuombe kwa roho na tuombe kwa akili,” alisema Askofu Dk. Malasusa.

Mkuu wa DMP alisema ni wakati wa kuomba kwa roho na akili na pale hali itakapokuwa njema watu wataendelea kukutana.

RAIS WA WALUTHERI ATOA NENO

Corona ambayo imetikisa dunia pia imefanya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (FMKD-LWF) nalo kuandika barua maalumu kwa makanisa yake wanachama duniani kote kusisitiza jambo hilo la maombi.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Rais wa Fungamano hilo Askofu Mkuu Dk. Filibus Musa na Katibu Mkuu Dk. Martin Junge FMKD imewataka wanachama wake kusimamia mstari wa kitabu cha 2Tim 1:2 unaosema Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na moyo wa kiasi.

“Huu ni wakati wa kuendelea kuamini uwepo wa huruma za Mungu katika maisha ya mwanadamu. Tunao ujasiri tukijua kuwa Mungu hatuachi kamwe, hata kama itamaanisha kupitia mateso ya msalaba.

“Tunauona msalaba wa Yesu Kristo kama alama ya nguvu na tumaini letu. Tunaalika makanisa wanachama kuombeana hasa kwa nchi na makanisa ambayo yako katika kiini cha mlipuko wa virusi hivyo,” ilisema barua hiyo.

FMKD imeorodhesha maombi 12 ambayo wanachama wake watayaomba juu ya ugonjwa huo.

Mojawapo ya maombi hayo yalisema; “Uwe msaada wetu hasa wakati huu ambapo virusi vya corona vinazidi kusambaa ulimwenguni, uponye wagonjwa, uzisaidie na kuzilinda familia zao na marafiki ili wasiathirike. Ee Mungu, sikia kilio chetu.”

Makanisa na watumishi mbalimbali wa Mungu wanaendela kutoa wito wa kuomba juu ya ugonjwa huo ambao kwa hapa nchini tayari umesababisha kifo cha mtu mmoja huku wagonjwa wakiwa 20 ambao 17 kati yao, kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wanaendele vizuri wawili wakiwa wamepona.

COVID-19 ilianzia nchini China Desemaba mwaka jana na hadi sasa imeenea dunia nzima.