Category Archives: Uncategorized

IBADA YA TAREHE 06 AGOSTI 2023 SIKU YA BWANA YA 9 BAADA YA UTATU

Somo:TUENENDE KWA HEKIMA
ZABURI 119:161–168; MATHAYO 10:5–15, MITHALI 1:1–7*
WIMBO: TMW 294
MAFAFANUZI
1. UTANGULIZI: Mithali 1:1
Kitabu kinaitwa Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa misemo ya hekima kuhusu hali halisi ya maisha ya kila siku yenye busara na haki ikigusa mada mbali mbali. Kitabu kinatoa mafundisho yenye mafumbo ambayo yalikuwa ya kawaida katika Maisha yao ya wakati ule. Ni misemo mifupi mifupi ambayo ni rahisi hata kuikariri. Kama vile Mfalme Daudi alivyo chimbuko la Zaburi katika Israeli ndivyo Mfalme Sulemani alivyo chimbuko la hekima katika Israeli. Inatajwa kuwa Sulemani aliandika Mithali 3,000 na nyimbo 1,005 wakati wa maisha yake (1 Wafalme 4:32–34). Na wakaenda Mataifa yote kwa Sulemani ili waisikie hekima yake.

Kitabu hiki kinaitwa Mithali za Mfalme Sulemani wa Israeli, lakini ni hakika kwamba Sulemani hakuziandika zote. Nyingine zinatajwa kuwa ziliandikwa na Aguri bin Yake (Mithali 30:1–33) na Mfalme Lemueli (Mithali 31:1–9), na wengine wametajwa kuwa wenye hekima bila kutajwa majina yao (Mithali 22:17 na 24:23). Mkazo ni kufundisha hekima ya jinsi ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Sura nne za kwanza ni mkazo juu ya asili ya hekima na umuhimu wake na sura zinazofuata ni mkusanyiko wa mistari miwili miwili mifupi yenye mithali zenye nguvu zinazogusa mambo mbali mbali ya maisha kama ndoa, upendo, uvivu, bidii ya kazi, maonyo kuhusu ulevi na uasherati.

Mfalme Sulemani alifahamika kwa umaarufu na upekee wa hekima ya ajabu. Sulemani alipopewa nafasi na Mungu katika ndoto ya kuomba jambo lolote atakalo, aliomba hekima ya kuliongoza taifa la Israeli na Mungu alijibu ombi lake (1 Wafalme 3:3–13). Zipo habari katika kitabu cha Wafalme wa kwanza zinazoonyesha jinsi alivyotumia hekima aliyopewa na Mungu. Mfano maarufu ni wa kesi ya wanawake wawili makahaba ambao walimgombania mtoto aliye hai wakimkataa aliye kufa (1 Wafalme 3:16–28).

2. MITHALI 1:2-7 KUSUDI KUU LA KITABU
Mwanzoni kabisa mwa kitabu Sulemani anaelezea kusudi la kitabu cha Mithali. Ni kujenga maisha ya uadilifu yanayofaa kimwili na kiroho. Kumpatia msomaji hekima, busara na maarifa ya Kimungu. Yanatajwa makusudi makuu matatu:

(a) Ili kuwapa wajinga werevu (Mithali 1:4).
Kuwapa wajinga, au watu wa kawaida werevu au busara. Hao ni watu wasio wasomi, hawa ndio wenye kiu ya kupokea mafundisho. Kitabu hiki kinapaswa kuwafundisha hawa wasio na uzoefu ili kujua nini cha kufanya na wafanye namna gani katika maisha yao. Na kijana atapata utambuzi au ufahamu hata kwa mambo ambayo hakuyafahamu. Sifa moja wapo kubwa ya watu wa kawaida (simple people) au ambao wametajwa kuwa wajinga ni wepesi. Mithali 14:15 inasema: Mjinga huamini kila neno, bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. Huyu mtu ni mwepesi au hata inaweza kusemwa kuwa ni mjinga, anaweza kuwa na maoni lakini akakosa hoja za nguvu.

(b) Kuwapa vijana maarifa na tahadhari (Mithali 1:4)
Vijana na wale watu wepesi wapo kuelekea utu uzima au kwenye hekima. Kitakachowapa tahadhari na uchaguzi sahihi katika maisha haya ni kukubali kufundishwa hekima. Hata nyakati za sasa kuna mambo mengi yanahitaji kuchambua kwa hekima na kuishi maisha ya tahadhari. Nyenzo ya kuishi maisha ya tahadhari ni hekima.

(c) Kuwaongezea elimu wenye hekima na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia (Mithali 1:5-6) waweze kuishi maisha ya uadilifu.

Kumbe kitabu cha mithali hakipo kwa ajili ya wajinga na wale wasio na uzoefu tu bali hata kwa wale wenye hekima. Kwa kupitia mafundisho ya mithali hizi wenye hekima wataongezewa elimu zaidi na zaidi. Mwenye ufahamu atafikia mashauri yenye njia, yanayomwezesha kutatua matatizo magumu kama ilivyokuwa na mfalme Sulemani alipoletewa kesi ya wale wanawake wawili waliogombania mtoto. Kumbe hakuna mwisho katika kutafuta maarifa na hekima.
Anasema mithali zinampelekea mtu kujua hekima na adabu, kutambua maneno ya ufahamu na kufundishwa matendo ya busara katika haki na hukumu na adili. Katika kujua hekima ifahamike kwa kizazi chetu kinaitwa cha habari na upeanaji wake (information age) lakini sio wengi katika kizazi hiki wanaotafuta hekima. Kujua maneno ya ufahamu maana yake yameandikwa yanapaswa kusomwa au kuangaliwa. Mithali 3:21 anasema Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, shika hekima kamili na busara.
Kujua hekima: Kuna tofauti kati ya hekima (wisdom) na maarifa (knowledge). Mtu anaweza kuwa na maarifa au ufahamu lakini asiwe na hekima. Kwani maarifa (knowledge) ni mkusanyiko wa ukweli wa mambo (facts about things) lakini hekima (wisdom) ni matumizi sahihi ya vile ambavyo tunavifahamu katika maisha yetu. Maarifa au ufahamu (knowledge) yanaweza kutuelezea namna mfumo wa utawala wa fedha lakini hekima ndiyo itasimamia matumizi sahihi ya fedha, kwa mfano kusimamia makisio ni hekima zaidi kuliko utaalamu. Shida yetu leo watu wengi wamejikuta wanatafuta fedha na sio hekima. Wengi tunaweka nguvu katika kupata elimu na sio hekima. Swali linakuja, hekima inatafutwaje? Mithali 1:7 na Zaburi 111:10 zinaweka wazi kuwa kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima. Kumbe hekima na maarifa vyanzo vyake ni kumcha Bwana. Na ukienda kwa Ayubu 28 unaona maelezo marefu kabisa.
Kufundishwa matendo ya busara/hekima
Mithali zipo kama shule au chuo cha hekima. Lakini tuingie chuoni tukiwa na moyo pamoja na akili wazi kupokea mafunzo. Tukifanya hivi haki, hukumu na adili/usawa vitatokea katika maisha yetu.

Lakini msingi mkuu wa hekima na maarifa ni kumcha Bwana ambacho ndicho chanzo cha maarifa yote (Mithali 1:7; Zaburi 111:10). Kitabu cha mithali kimeweka mkazo wake katika mambo halisi ya maisha na sio nadharia. Lakini kinatupa ukweli kwamba msingi ni fundisho la kitheologia kuwa maarifa na hekima yanatokana na kumcha Mungu, kuwa na hofu ya Mungu. Hofu ya Mungu ni kumjua Mungu, kujitoa kwa Mungu, kujinyenyekesha kwa Mungu.

3. TUENENDE KWA HEKIMA
Wiki iliyopita tuliongozwa na kichwa kinachosema uchaguzi wa busara na leo tunazunguzia hekima. Mara nyingi tunajikuta tunatumia maneno haya mawili kwa wakati mmoja, hekima na busara. Nimeeleza kwa kirefu tofauti zake katika kitabu cha Mafafanuzi ya Mahubiri ya mwaka 2020 ukurasa wa 199 na ukurasa wa 205. Kwa haraka utaona kuwa hekima ni pana kuliko busara. Hekima inasimama kama usukani wa kuendesha busara.

Somo letu linatuhimiza kuenenda kwa hekima katika dunia ambayo imebadilika mno katika mfumo wake. Mahusiano katika ndoa yameingia changamoto kubwa mno. Migogoro katika ndoa ni mingi. Ukiangalia kwa undani utagundua kuwa kuna vitu vya msingi vinakosekana. Maarifa ya maisha ya ndoa na hekima za Kimungu zimekosekana. Na mahali fulani imeelezwa kuwa ndoa za watu walioenda shule ndio zinaongoza kuleta shida, kumbe maarifa na elimu vimeshindwa kuleta maelewano katika ndoa. Biblia imeshatuambia chanzo cha maarifa na hekima ni kumcha Bwana. Mungu asipopewa nafasi halisi katika maisha yetu hakuna usalama.

Hata wale wanaoonekana kama wacha Mungu, watu wa dini sana wamepata shida hiyo hiyo kwa sababu ya kukosekana kwa misingi ya kweli ya neno la Mungu. Akili zimeshindwa kufundishika. Neno linasema: Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama (Zaburi 32:8). Mfano wa ndoa ni mmoja tu. Zipo changamoto nyingi zaidi ya hizo ambazo zinahitaji hekima za Mungu.

Kuna hitaji hekima katika malezi ya watoto na mahusiano kati ya wazazi na watoto, katika kutunza mazingira yetu, katika kutafuta na kutumia fedha.

Mambo yote haya kwa kutumia maarifa yetu hatuwezi kuyamudu, maana adui yupo kazini wakati wote. Tunahitaji uongozi wa Mungu. Na uzuri wake ni kwamba, ndani yetu huishi Roho wa Mungu. Huyu ndiye hekima yetu na mwongozo wetu kwa kila jambo. Maana yake, ili kuenenda kwetu kuwe kwa hekima, lazima tuhakikishe tupo na yeye aliye asili ya hekima. Mungu atusaidie tumpe nafasi Roho wake maana ni katika yeye tutakuwa na hekima na hivyo tutaweza kuenenda kwa hekima. Amen.

IBADA YA TAREHE 30 JULAI 2023 SIKU YA BWANA YA 8 BAADA YA UTATU

Somo:WEMA WA MUNGU WATUVUTA TUPATE KUTUBU
ZABURI 27:5-10; 2 KOR. 7:7-12;HOSEA 14:1-3*
WIMBO: TMW 149
MAFAFANUZI

1. UTANGULIZI

Ujumbe wa kitabu cha Nabii Hosea uliwasilishwa kwa njia ya kuigizwa katika Maisha ya nabii mwenyewe. Kwa mtazamo wa utumishi na ufuasi haikuwa njia rahisi ya kuwasilisha ujumbe. Nabii Hosea aliagizwa na Mungu kuoa mwanamke kahaba na kuzaa naye watoto. Mungu alisema anafanya hivyo kwa sababu nchi imefanya uzinzi mwingi. Mwanamke aliyemwoa aliitwa Gomeri (Hosea 1:2-3). Hata baada ya kuolewa na Nabii Hosea, Gomeri aliendelea kwenda kufanya uzinzi na wanaume wengine na Hosea aliendelea kumrudisha na hata kumnunua kwa fedha ( Hosea 3:2).

Katika mlango wa tatu nabii anafafanua alichoagizwa na Mungu kufanya na sababu za kufanya hivyo. Aliagizwa ampende mwanamke apendwaye na Rafiki yake naye ni mzinzi, kama vile Mungu awapendavyo wana wa Israel ingawa wamegeukia miungu mingine (Hosea 3:1).

Ndani ya ujumbe wa Hosea kuna onyo kwamba kama Israeli hataacha uzinzi (kuabudu miungu mingine) ataadhibiwa vikali. Lakini kumbuka, adhabu huwa na lengo la kumrekebisha mkosaji. Hukumu ndio shida. Labda mhukumu awe na huruma. Sura zinazofuata Hosea 4-13 zinahusu Mungu na Israeli asiye mwaminifu. Ndani yake sura za 4 na 5 zinazungumzia uzinzi ambao Israeli anaufanya kwa kuabudu miungu mingine. Sura ya 6 Efraimu alirudi kuadhibiwa. Njooni tumrudie Mungu maana yeye amerarua na yeye atatuponya (Hosea 6:1); Sura za 7-12 Israeli (Efraimu) atapona hukumu kama atamrudia Mungu anayempenda. Efraim ni kabila ambako wafalme wengi walitoka. Sura ya 13 Israeli atahukumiwa sasa na sura ya 14 inaonyesha kuwa Israeli ataokolewa baadaye.

Ukijumlisha ujumbe wa Hosea unakuwa tabia yao ya kutokuwa waaminifu ndio sababu ya hukumu itakayokuja. Hii sura ya mwisho ni ya matumaini kwa taifa lililotubu. Hosea aliitwa kuhudumu katika taifa lililochanganyikiwa na limepoteza maadili na uchaji. Alipewa wajibu mkubwa mno wa kuoa kahaba na yeye kubaki mwaminifu katika ndoa yake kama Mungu alivyo hata kama mke wake alikwenda kwa wanaume wengine.

Fikiria tu njia hii ya kuwasilisha uasi ambao umefanywa na wana wa Israeli angepewa mchungaji mmojawapo leo. Kwanza, yeye mwenyewe angesema hiyo sio sauti ya Mungu na wale wanaoogonzwa naye wengi wangetia mashaka kama kweli ni Mungu ameruhusu hilo.

2. HOSEA 14:1-3

Sura hii ya mwisho ya kitabu cha Hosea inakuja na kitu cha pekee baada ya kutupitisha kwenye ujumbe wa hukumu. Anakuja na ujumbe wa rehema. Rehema ni msaada unaoambatana na huruma. Mungu mwenyewe anatoa maelekezo namna ya kufanya toba ili kumrudia Mungu. Anaelekeza ili kufikia toba nini cha kusema na nini cha kufanya. Ujasiri wa kutubu unajengwa na utayari wa Mungu kuwapokea wenye dhambi wanaporudi. Mungu anasema nitawaponya kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo kwa maana hasira yangu imemwacha (Hosea 14:4,8). Pia zipo faraja kubwa ambazo ameziandaa kwa ajili ya Israeli anayetubu (Hosea 14:5,7). Ujumbe unahitimishwa kwa swali kwamba ni nani aliye na hekima na atayafahamu mambo haya? Na nani mwenye busara atakaye yajua? Ni maswali yanayotuhusu sisi sote katika ukweli wa kuyapokea haya (Hosea 14:9).

Hosea 14:1 Israeli mwenye dhambi anaitwa kurudi (kutubu).

Kumbe kila mtu anahitaji ujumbe wa toba hata walio ndani ya agano kama Israeli. Kwa hiyo hata Wakristo ndani ya kanisa wanahitaji ujumbe wa toba kila siku. Israeli mrudie Mungu wako kwa maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako. Na kurudi ni kurejesha uhusiano (fellowship) uliopotea au uliovunjika. Ulipotea au kuvunjika namna gani? Ni pale walipoanguka au kujikwaa kwa sababu ya kuabudu miungu mingine na kumwacha Mungu aliye hai ambaye anawapenda. Ndio picha ya ndoa ya Hosea na Gomeri. Wanarudi kwa njia gani? Ni kwa kutubu na kutengeneza.

Hosea 14:2 Chukueni maneno pamoja nanyi

Wanaporudi wameelekezwa maneno ya kwenda nayo ambayo ni kumwambia Bwana: Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema. Na hivyo ndivyo mtakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe.
Wanapomrudia Bwana hawaendi kimya kimya na lazima waende kama Bwana anavyotaka na anavyoelekeza. Hataki wafikiri tu mioyoni na kujisikia hatia ya dhambi bali wakiri maneno hayo kwa midomo yao. Wamwambie Mungu kwamba tunakupenda na kwamba tumekukosea. Hata katika mahusiano yetu mfano ya mume na mke huwa ina nguvu kumwambia mwenzi kwamba unampenda, hata kwenye viapo vya ndoa wenzi huwa wanakiri kwa midomo yao kueleza upendo wao na kujitoa kwao katika ndoa. Katika viapo hivyo tunabeba maneno pamoja nasi. Mtume Paulo katika Warumi 10:8-10 anasema mtu kwa moyo huamini hata kupata haki na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

Je, tunachukua maneno gani pamoja nasi?

Hayo maneno sahihi ya kwenda nayo tunayapata kutoka kwa Mungu mwenyewe katika neno lake. Mfano Mdo 3:19 tunaambiwa tubuni basi mrejee, ili dhambi zenu zifutwe. Na Mathayo 3:2 Yohana alihubiri tubuni mwache dhambi zenu. Na Yesu alianza huduma yake kwa kuagiza toba, Mathayo 4:17 tubuni.. Upo umuhimu wa kukiri maasi yetu kwa midomo yetu. Zaburi 32:5 c; Nalisema nitayakiri maasi yangu kwa Bwana. Katika toba kuna umuhimu mkubwa wa mtu kukiri kosa alilofanya. Katika mifumo mingi ya kanisa wapo watu waliopewa wajibu wa kuwasikiliza wengine wanapotengeneza mambo yao na Mungu. Kuna wachungaji waliokula kiapo cha kufanya hivyo. Kuna watu wanafundisha kuwa inatosha kumwambia Mungu makosa yako, sawa lakini kuna mahali hali na hatia ya dhambi haiishi hadi mtu amekiri kwa midomo yake. Shida ni pale ambapo huduma imeingiliwa na watu ambao hawana dhamana ya kufanya hilo na kusimama kama mawakili wa siri za Mungu au wale wenye dhamana wanapokengeuka na kuharibu huduma. Lakini ukweli utabaki kuwa katika toba upo umuhimu wa kukiri kwa midomo yetu.

Tunamwambia nini Mungu katika toba yetu?

Ondoa maovu yote na utupokee kwa rehema zako. Hata katika sala ya Bwana Yesu alitufundisha kukiri makossa yetu mbele za Mungu ili atusamehe. Tunaporudi kwa Mungu lazima tunyenyekee mbele zake na kukubali kwamba tumekosa, tumefanya dhambi na tunahitaji msaada wake. Tunamhitaji yeye tu hatuna lolote la kufanya Zaidi ya kujiachia mikononi mwake.

Na ndivyo tutatoa sadaka ya midomo yetu kama sadaka ya ng’ombe. Maana yake maneno yetu ya toba na sifa mbele za Mungu ni sadaka ya kuteketezwa mbele za Mungu. Katika toba hiyo tutakiri wazi na kutengeneza mambo matatu:
(a) Kukataa kutegemea mataifa ya kigeni (Ashuru). Mungu pekee yake ndiye mwokozi wetu.
(b) Tutaacha kutegemea uwezo wa kivita kama kutegemea farasi (Zaburi 20:7).
(c) Tutakataa kutegemea sanamu, kazi za mikono yetu bali tutamtegemea Mungu pekee yake.
Wito wa nabii Hosea katika kifungu hiki (Hosea 14:1-3) ni kuwaita Israeli kurudi kwa Mungu kwa moyo wa dhati. Amewapa maneno ya kuomba wanaporejesha uhusiano wao na Mungu. Mwana mpotevu katika Luka 15:11-32 yeye alipanga maneno ya kusema anaporudi nyumbani kwa baba.
Kitabu cha Hosea kinahusu mambo ya dhambi na hukumu lakini pia upendo na huruma za Bwana kwa watu wasiostahili kama ambavyo Gomeri hakustahili kuwa mke wa nabii. Na Upendo huo wa Mungu umeonyeshwa kwa njia ya ndoa hiyo ya nabii Hosea na mwanamke Gomeri. Ni picha inayoumiza moyo kwa mtazamo wa kibinadamu, je, kwa Mungu mtakatifu sio zaidi?

3.WEMA WA MUNGU WATUVUTA TUPATE KUTUBU

Kutokana na mafunzo ya kitabu hiki utagundua kuwa kumbe Mungu anapomtendea mema huyu mwanadamu aliye mwovu sio kwamba anataka aendelee kutenda uovu bali anataka avutwe na upendo wa Mungu na hivyo aweze kugeuka na kujinyenyekesha kwa toba.
Mungu atujalie tutambue hilo na kutumia neema hiyo ya nguvu ya toba.
Amen.

KIPIMO CHA IMANI

Tangu nimeokoka nimebahatika kusikia mafundisho mengi sana mazuri kuhusu imani, wakati mwingine nilijifunza kuwa huhitaji imani kubwa kung’oa mlima, na nilipoijaribu imani ndogo kung’oa mlima, mlima uliishinda imani yangu ndogo. Je! Wapi hasa nilikosea mpaka kushindwa kuung’oa mlima mkubwa kwa imani ndogo? ( nadhani nilihitaji imani inayokua kama mbegu ya haladali, mpaka kuzidi ukubwa wa mlima ndipo niung’oe)

Leo ninataka kukueleza kipimo cha imani yako kwa maelezo haya.

Kama imani yako ya kufa ni kubwa kuliko ya kuishi basi jua huna imani au imani yako ni haba, hivyo kikubwa lazima kishinde kidogo.

Kama imani yako ya kutokupona ina nguvu kuliko kupona basi huna imani, au imani yako haba na chenye nguvu kitashinda.

Kama imani yako ya kukosa ni hakika kuliko ya kupata basi imani yako ni ndogo hivyo kukosa kutashinda, na kama imani yako ya laana ni zaidi ya baraka nakuhakikishia kila utakapoongea, utakachowaza, utakachoota, utakacokiona na kukikiri kitakuwa ni laana, balaa, mikosi na chenye nguvu kwenye akili yako, moyo wako na kinywa chako ndicho kitakachoshinda na kutokea kwenye maisha yako.

Nadhani umeshajipima kwenye eneo lako, sasa ni kazi yako kuhakikisha unaifanya imani yako iwe kubwa kuliko, mlima, magonjwa, madeni, na mahusiano ndipo utakapoweza kubadilisha mwonekano wa kinachokutisha kwa imani. KUMBUKA CHENYE NGUVU, UZITO, NA UHAKIKA NDICHO HUSHINDA.
Wakati wewe unaona haiwezekani kuna watu imewezekana, tofauti yako na yao ni kile unachokiona kigumu wao walikiona chepesi. Iga mwenendo wao utafanikiwa
Bwana akibariki sana.
#victoriousyear2020
contact 0768386606

SIKU YA BWANA YA 13 BAADA YA UTATU

wazo la wiki: JIRANI YANGU

Masomo:
Zaburi 28:1-4
Mathayo 12:46-50
Matendo 28:7-10*
Rangi: KiJANI
Wimbo:TMW 410
UTANGULIZI
Leo tunatafakari juu ya mada ya Jirani zetu tukilitazama neno la Mungu kutoka
Matendo 28:7-10
> Jirani kulingana na tafsiri ya Kiswahili ni mtu yeyote aliye karibu na mahali
unapoishi.
> Jirani mi mtu muhimu sana katika maisha ya kila mtu, yawezekana anaweza kuwa
rafiki yako au adui zako.(Hekima inahitajika kuishi nae)
> Biblia tangu Agano la kale inaelekeza kuwa kila mtu anapaswa kumpenda jirani
yake kama nafsi yake( Law 19:17 – 18)
> Upendo wa namna hii haukuwa rahisi hivyo watu wengi walijitahidi kukwepa
wajibu huo na mara nyingi walihoji ni watu gani wanapaswa kuwa majirani.
Hata kipindi cha Yesu watu walijitahidi kumuuliza swali hili, na Yesu aliweka wazi
kuwa jirani ni :-
a. Mtu yeyote aliye na dhiki ni jirani yetu ( Lk 10: 29 – 37)
b. Jirani ni watu wote hata kama ni adui yetu ( Mt 5: 43 – 47)
Wajibu mkubwa aliopewa mwanadamu ni kumpenda Mungu na Jirani ( Mt 22:36-40,
Rum 13:8-10,Gal5:14,Yak2:8, 1 Yoh 4:20, Mt 3:28, 14:21)
Somo ambalo tumepewa kujifunza juu ya jirani kwa mwaka huu tunajifunza juu ya
jinsi ya kumtendea jirani hasa wale ambao tunafikiria hawawezi kuwa majirani.
1. AMRI IPO TUNAPOSHINDWA KUJITAWALA JUU YA JIRANI ZETU
> Mtu akifanyiwa ovu hupenda kulipa ovu kubwa zaidi na kuanzisha mashindano
baina ya watu waliogombana au kufanyiana maovu.
> Kutokana na kushindwa huku kujitawala hisia zao, kulisababisha haki kukosekana
katikati ya watu.(Law 24: 19 -20)
> Watu walipewa sheria ili iweze kusaidia ili adhabu iweze kulingana na Kosa.
2. WANA WA MUNGU WANAWAZA MEMA JUU YA JIRANI ZAO
> Kama nilivyoeleza kuwa jirani ni mtu yeyote mwenye dhiki hata kama akiwa adui
yako na unapaswa kumpenda kama nafsi yako
> Wajibu huu mzito wa kumpenda jirani kama nafsi yako uliendelea kuwatesa watu
wengi hadi kipindi cha Yesu.
> Kazi kubwa ya kukamilisha torati aliyoifanya Yesu katika mahubiri ya mlimani pia
aligusia suala la jinsi ya kukaa na watu kwa mtazamo mpya wa wana wa Mungu.
 Anawataka watu wa Mungu wasiwe na Mashindano juu ya uovu. Ukishindana
na uovu utajikuta inakuondolea uthamani wa kuwa mwana wa Mungu.
 Mtu akikufanyia jambo la kukuonea wewe usinung’unike fanya kwa upendo
utakaomshangaza mtesi wako; Jitahidi kuwa mkarimu kwake (Rum 12:20)
 Tusing’ang’ane kukariri neno la Mungu pasipo upendo wa kweli ndani yetu
kwa Mungu na jirani zetu
 Kuweka haja za wenzetu mbele kuliko matakwa yetu
 Tuwe na mizigo juu ya wengine (Mith 3:29)
3. MATENDO MEMA KWA JIRANI YANA MALIPO YAKE.
Jirani mtendee mema hata kama unaona hastahili, sababu unavyofanya hivyo sio
kwake tu bali unajitengenezea malipo yako Mbinguni na kujipa kibali cha kuwa
mwana wa Mungu ( Lk 6:35)
HITIMISHO
Mungu atuwezeshe tuweze kutambua thamani ya watu wengine zaidi kuliko makosa
wanayotutendea ili tuweze kuwatendea mema hata pale wanapotuudhi.
AMEN.
imeandaliwa na
Ev.John

MAHUBIRi Ya SIKU YA BWANA YA 12 BAADA YA UTATU

SOMO: TUTUMIE VYEMA NDIMI ZETU

masomo:
Zaburi 134
Mithali 10:11-13
Mathayo 8:1-4*

SHABAHA: WASIKILIZAJI WAELEWE YA KWAMBA KILA NENO LA ULIMI LAZIMA LITATOLEA HESABU KAMA JEMA AU BAYA SIKU YA HUKUMU

UTANGULIZI
Usemi ni uwezo mmojawapo wa mwanadamu wenye nguvu zaidi, kwa sababu kwa maneno yake anaweza kuleta manufaa makubwa, lakini pia anaweza kuleta hasara kubwa ( Mit 12:18,25; Yak 3:5,9)
Mtu awezaye kutawala ulimi wake anaweza kutawala nafsi yake yote ( Yak 3:1-4,7)
Uovu wa mtu huonekana kwa ulimi ambao haujatawaliwa ( Mk 7:21 – 23; Yak 3:6)
Maneno mengi ya mtu huonyesha upumbavu wake hivyo kila mmoja anapaswa kuutawala ulimi wake, utawala huo lazima uwe wa kweli isiwe ni kutumia maneno matamu tu ili afiche mawazo yake, yeye ni mnafiki na unafiki sio mzuri ( Zab 41: 5-6, Mit 10:18, Mt 22:15 – 18)
Ugeuzi wa maneno kwa ujanja au hila ni aina ya uongo ( Mit 12:19, 2Kor 4:2, Efe 4:25) Iwapo mtu anataka aseme ukweli kila wakati pia anatakiwa afanye hivyo kwa roho ya Upendo na maneno yake yaonyeshe tabia yake ( Mit 10:11, 20 – 21; 16:23; Efe 4:15, Yak 1:19)
Usemi wako unaonyesha hali yako ya kiroho na usemi huo utatumiwa siku ya hukumu kama ushahidi wako ( Mt 12: 36 – 37)
Hakuna neno ambalo Mungu halijui katika yale yote unayonena (Zab 139:4)

• Katika mistari hii miwili kutoka katika kitabu cha mithali inatufundisha mambo muhimu yafuatayo kuhusu matumizi ya Ulimi.

1. USEMI WA MWENYE HAKI UNA HEKIMA NA WEMA
Mtu aliye na hekima wakati wote anajua kuutunza ulimi wake, maneno yake wakati wote ni maneno yaliyokolea busara.
Maneno ya mtu wa haki yanatamani kuona mema kwa wengine na yamejaa hekima(Mith 10:20 – 21)
Mtu mwenye hekima si mwepesi wa kusema na akisema maneno yake yamejaa baraka na mema.

2. USEMI WA MTU MWOVU WAKATI WOTE UNADANGANYA NA KUUMIZA(Zab 10:7)
Mtu mwovu wakati wote huwaza mabaya kwa wengine na hupenda kutamka laana kwa watu wengine(Zab 52: 2 – 4)
Maneno yake yamejaa uongo na kujipendekeza( baadhi ya vitu asivyopenda Mungu Mith 6:17)
Mtu mwovu huwa mnafiki na kutaka kujionyesha kuwa ni mwema mbele za watu tu.

3. ULIMI MWOVU UTAADHIBIWA
Mungu atamharibu na kumuondolea mbali mwenye maneno mbaya ( Mith 10:31)
Atakuondoa katika nyumba yako( Zab 52:5)
Kifo kitampata mwenye ulimi wenye hila (Mith 17:20)

HITIMISHO
Mungu atusaidie tuweze kutumia ulimi wetu vizuri tukijua kuwa maneno yetu ipo siku tutayatolea hesabu.
AMEN.
imeandaliwa na mwinjilist John
KKKT -SD Njombe

#0768386606