MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 21/06/2020

siku ya 2 baada ya utatu

SOMO: TUKAE PAMOJA KWA UMOJA
MASOMO Yohana17:20-21
?Efeso 5:8-14
? Zaburi 133

UTANGULIZI
• Jumapili ya Leo ni sikukuu kubwa ya KKKT, tuanze mafundisho yetu ya leo kwa kumtakia ndugu yako heri ya siku kuu.
• Leo ni jumapili ambayo tunaazimisha kuunganika kwa makanisa saba ya Kilutheri Tanganyika ambayo ni:-
a) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Iraqw
b) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la kaskazini mwa Tanganyika
c) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kaskazini Magharibi mwa Tanganyika
d) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kati mwa Tanganyika
e) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Kusini mwa Tanganyika
f) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara Digo
g) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Uzaramoni – Uluguru

• Makanisa haya saba yalipoungana yalikwa na washarika laki tatu (300,000) tarehe 19/06/1963 hadi kufikia leo hii kanisa moja la Kilutheri lina zaidi ya dayosisi 25 na waumini zaidi ya milioni sita. (6,000,000)
• Siku ya leo tunaadhimisha miaka mia moja na thelathini (133) ya ulutheri Tanzania.
• Mwaka huu neno linalosindikiza sikukuu hii ni kutoka YOHANA 17;20-21 ambalo linaendelea kukaza juu ya umoja katika kanisa.
• Mlango huu wa 17 ni mlango wenye sala ya Yesu, kwanza anaanza kwa kujiombea yeye mwenyewe, kisha anawaombewa wanafunzi wake na anahitimisha kwa kuwaombea waumini wote wawe na umoja.
• Kipengele tulichosoma kinatufundisha mambo kadhaa

1. YESU NDIE MWANZILISHI WA KANISA
• Aliwaita wanafunzi na kuwaandaa kwa kazi maalumu ya kulihubiri neno lake ( Marko 3:14)
• Aliwaandaa kuifanya kazi aliyokuwa anaifanya yeye mwenyewe
• Aliwataka wawe na umoja ili waweze kuwa na lengo moja
• Maswali ya kujiuliza sisi wenyewe
a) Wewe umeandaa watu wa kufanya kazi ambayo unaifanya?
b) Je, wewe katika kazi/ huduma unayoifanya unazingatia umoja? Au unatengeneza makundi?

2. LENGO LA YESU NI KUONA KANISA MOJA
• Mungu anawataka waumini wote wawe na umoja na kuweka tofauti zao pembeni(Yesu anajua kuwa tunazo tofauti ila tukubali kuziweka pembeni na kuwa na umoja katika lengo moja)
• Umoja huu anataka ufanane na umoja wa Mungu na Yesu yaani umoja usio wa Kinafiki, umoja ambao hauwezi kutenganishwa. ( Umoja wetu katika utofauti wetu ufanye hata watu kushangaa tumeweza vipi kuwa wamoja)
• Umoja huu uwe ni umoja uliofungwa katika upendo wa kweli ( Yohana 13:34 – 35)
• Swali la kujiuliza waumini wale wanaojitenga na ibada kama vile kutokuwa kundini na kuanzisha madhehebu mengine bado Yesu anawahesabu kama wanafunzi wake? Wengine hata kukwepa majukumu ya kazi za umoja kama vile sadaka za umoja nk ni wafuasi wa Yesu Kweli?

3. UMOJA WA KIKRISTO UWE UMOJA WENYE MALENGO
• Umoja huu unapaswa uwe umoja unaoendelea kukua kama tulivyoona historia ya kanisa letu.
• Umoja huu uwe ni umoja wenye imani moja
• Umoja huu uwe ni umoja unaoendeleza utukufu wa Mungu ulimwenguni kote.
• Umoja unaosogeza waumini wote kuwa familia moja, kijiji kimoja. Tukitambua kuwa Yesu ndie mwanzilishi wa utandawazi ( Matayo 28:19 – 20, Mdo 1:8)
• Kanisa la Kiinjili la Kilutheri kwa kutambua kwamba misioni ya Bwana Yesu inaendelea kukua na kupanuka imeendelea kujitahidi kuleta umoja kwa kuweka uwiano wa sadaka za umoja ili kukidhi hitaji hili ambazo zinafanya kazi ya:-
a) Kutuma wachungaji maeneo ya misioni ya ndani na nje ya nchi
b) Kuhisani masomo ya wanafunzi wanaotoka maeneo ya misioni
c) Kuendesha vituo vya kazi za umoja kama vile Ofisi kuu ya kanisa, Shule ya viziwi mwanga na Njombe, Radio sauti ya injili, Seminari ndogo ya Morogoro nk.
Mimi na wewe tumeshiriki vipi katika misioni hii ya Yesu?

HITIMISHO
• Roho mtakatifu atusaidie kutambua kusudi la Yesu kwa kanisa lake nasi kama wafuasi wa kweli tuungane kwa upendo kuliendeleaza kanisa la Mungu.
• Umoja ni silaha kubwa sana katika huduma yetu ya uinjilisti. Ubora wa ushirikiano wetu unawavuta watu wengi kwa Mungu na udhaifu wa umoja wetu unalitawanya kundi la Mungu na kulipoteza huku ushuhuda wetu ukiendelea kuwa dhaifu
• Tuwavute watu kwa Mungu kwa kudumisha umoja miongoni mwetu.
AMEN.