SIKU YA BWANA YA 9 BAADA YA UTATU

IBADA YA TAREHE 09 AGOSTI 2020

TUENENDE KWA HEKIMA
ZABURI 119:25-32; LUKA 12:44-48

MAHUBIRI: KOLOSAI 4:2-6

1. UTANGULIZI
Katika mafafanuzi/mahubiri ya juma lililopita tuliangalia uhusiano uliopo kati ya hekima na busara. Tukawa tumesema kwamba hekima ni pana kuliko busara na ipo kama usukani wa kuiendesha busara. Busara ni namna ya kuamua jambo kwa akili kufuata mazingira. Na pia tukasema busara ni hekima inavyoonekana katika matendo. Na mkazo wetu ulikuwa katika uchaguzi wa busara. Mimi katika mahubiri nilikaza nguvu ya uchaguzi (the power of choice) na nikasema hivi tulivyo ni matokeo ya uchaguzi, nikamnukuu Dkt. John C. Maxwell aliyeandika “life is full of choices and every choice you make, makes you” (maisha yamejaa uchaguzi na kila uchaguzi unaoufanya unakutengeneza wewe). Mwisho niliorodhesha kanuni 4 za kutuongoza tunapofanya uchaguzi ili hekima ijidhihirishe katika maisha yetu.

(a) Zingatia vipaumbele na utabiri matokeo ya uchaguzi wako. Vipaumbele vinaongozwa na tunu ulizo nazo, maono na dhamira (values, vision and mission). Maana, changamoto mara nyingi sio kuchagua kati ya baya na jema bali kati ya zuri na zuri zaidi.

(b) Usikubali hisia zikuongoze. Epuka kufanya uchaguzi ukiwa na furaha sana ama huzuni/hasira
(c) Fikiria njia mbadala nyingi kabla ya kufanya uchaguzi na maamuzi.

(d) Jifunze kusikiliza dhamiri (Roho Mtakatifu). Je, unasikia amani moyoni na lile unalochagua? Amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu (Kolosai 3:15).

Leo tunaambiwa tuenende kwa hekima mbele za wasioamini. Na somo letu Kolosai 4:2-6 ligusa suala la uinjilisti tunaweza kufanya kwa njia ya wengine kwa kuwaombea (4:2-4) au tunaweza kufanya wenyewe moja kwa moja kwa kuuendea ulimwengu (4:5-6). Mungu anatutaka tuwe makini na maisha ya sala binafsi na pia namna ya kuhusiana na watu wa dunia hii, namna ya kuishi katika ulimwengu kwa hekima.

2. DUMUNI KATIKA KUOMBA
Yesu aliwahi kufundisha pia juu ya kuomba bila kukoma katika Luka 11:5-10. Mtu aliyefikiwa na rafiki usiku wa manane akiomba asaidiwe mikate kwa ajili ya mgeni, Yesu anasema ataamka kwa vile hataki kuendelea kusumbuliwa. Na pia katika Luka 18:1-8 Yesu alitoa mfano wa kadhi aliyemsaidia mwanamke mjane kwa kuona anamsumbua kila siku kuomba amsaidie.

Paulo akawahimiza Wakolosai kuendelea kuomba kwa bidii kama yeye alivyowaombea pia (Kolosai 1:3-8). Na anaposema dumuni katika kuomba tafsiri nyingine zinatupeleka kwenye maana ya kuwa uwe na nguvu (be strong). Uwe na juhudi kubwa. Huwezi kuendelea katika maombi kama huna pumzi na juhudi katika maombi. Ni kupambana, ni vita ya kuangusha ngome za Shetani.
Maombi sio tukio la mara moja katika maisha ya mkristo. Maombi ni jambo la kila siku mbele za Mungu (1 Thesalonike 5:17).

3. MKESHE KATIKA KUOMBA NA KUSHUKURU

Paulo anawahimiza Wakolosai kuwa macho, kukesha. Hii ni lugha ya kiulinzi au kiaskari. Walinzi hodari husimama usiku mzima ili kuhakikisha lindo lao lipo salama. Kwa hiyo wanapaswa kuwa macho wakati wa maombi wasilale usingizi. Mara nyingi mwana maombi anakumbana na uchovu wa mwili na hivyo kumfanya alale usingizi wakati wa kuomba.

Yesu aliwahimiza wanafunzi wake kukesha katika maombi katika matukio mawili muhimu. Pale alipokuwa nao mlimani katika tukio la kugeuka sura (Luka 9:28-33), Petro, Yakobo na Yohana walilemewa na usingizi na kushindwa kuomba. Mahali pengine ni katika Bustani ya Gethsemani (Mathayo 26:36 -46). Walilala na akawauliza, je, hamkuweza kukesha nami hata saa moja? (26:40).

Ipo vita wakati wa maombi. Unaweza kufikiri ni vita kati ya maombi na usingizi, lakini kama unaona rohoni, kuna nguvu nyuma yake. Hakuna wajibu unaweza kufanyika kwa ufanisi bila maombi. Lakini kila uombapo kuna upinzani! Pamoja na kuomba walipaswa kumshukuru Mungu.

Maombi siyo ”Mungu nipe hiki na kile na kile! Tunasogea mbele zake kwa shangwe na shukrani kwa Mungu. Katika shukrani tunamshukuru Mungu kwa namna alivyo na atendavyo. Ukuu wake, uaminifu wake, upendo wake, neema yake, hekima yake, na mengine mengi! Bila Mungu kututendea kwa namna atendavyo, hatuwezi kudumu hata siku moja.

Katika maombi, tunaomba ufalme wake uje. Ufalme wa Mungu ukija, tunapata mahitaji yetu na kwa namna Mungu aonavyo inafaa. Tunapoomba tunashukuru sio kwa sababu tumepata tayari, bali kwa sababu tunaamini kuwa tunapata, maana Mungu ni mwaminifu. Shukrani inatuhakikishia kuwa tunamwendea Mungu tunayemwamini kuwa anajibu.

4. MTUOMBEE MUNGU ATUFUNGULIE MLANGO WA NENO TUNENE SIRI YA KRISTO
Wakolosai wanahimizwa kuomba kwa ajili ya viongozi wao wa kiroho. Viongozi wa kiroho wasipopata neema au kibali machoni pa Mungu watakwamisha shughuli za kiroho. Paulo hakuwahimiza kuomba kwa ajili ya mahitaji yake binafsi bali Mungu afungue mlango kwa neno la Mungu, yaani fursa ya kuhubiri injili, tena ili anene siri ya injili impasavyo sio kama atakavyo yeye. Hapa kuna siri kubwa! Sio kila anayesimama mimbarani na kuhubiri anahubiri Neno la Mungu. Kwa hiyo Paulo anaomba Wakolosai wamwombee ili ahubiri Neno la Mungu. Paulo anasema kuwa alikuwa kifungoni kwa sababu ya uaminifu wa kuhubiri injili ya Kristo na alikuwa tayari kupokea matokeo ya uaminifu huo hata kupata vifungo zaidi. Ukihubiri Neno la Mungu katika kweli yake, wakuu wa giza kupitia watumishi wao watatikisika na kupanga njama za kukuangamiza! Ukiweza soma habari za Danieli. Au jifunze vizuri upinzani uliokuwepo katika huduma ya Bwana Yesu. Lakini wajapojipanga kwa upinzani wa aina yoyote ile, kuna nguvu ya Mungu itujiayo katika maombi! Katika maombi tunajadiliana na kusemezana na Mungu. Mungu huja kututia nguvu na kufanyika ngao yetu.

5. ENENDENI KWA HEKIMA MBELE YA WASIO AMINI/ULIMWENGU
Paulo anawakumbusha Wakosolai kuwa maisha ya kiroho sio tu kujifungia ndani kwa maombi bali wanahitaji kuishi hekima yao kwa vitendo, kuwa na busara kama tulivyojadili somo lililopita. Hii itawaongoza namna ya kuongea na kuishi. Kwa wakati ule, tayari kulikuwa na picha mbaya kuhusu ukristo. Lakini kwa njia ya hekima na mwenendo wao walitakiwa kuiondoa ile picha mbaya na kuuonesha ulimwengu uzuri ulio katika Bwana unaodhihirika katika maisha ya Wakristo. Mienendo yetu ni mahubiri yanayoishi. Tunapaswa kumdhihirisha Yesu Kristo katika maisha yetu pia, sio maneno tu!

6. MUUKOMBOE WAKATI
Neno kuukomboa wakati linabeba maana zifuatazo: kutumia wakati kwa njia nzuri kabisa (making the best use of time) kutumia kwa makini kila fursa inayojitokeza (making the most of every opportunity), au kutumia kwa ufanisi kila wakati unalionao (make effective use of our time). Mtume Paulo kwa Waefeso 5:15-20 anasema enendeni kwa hekima mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu na wasiwe wajinga. Kila nafasi katika maisha ni muhimu lazima itumike kwa ukamilifu wote na kwa manufaa. Ndio maana imesemwa kuwa wakati ni mali. Kiroho ni kama alikuwa anawaambia kuwa wakati ni mfupi tusikubali mtu afe bila kumjua Yesu. Lakini hata wakati huu wenye mabadiliko makubwa ya kiuchumi, muda ni moja kati ya rasilimali muhimu sana katika kuleta maendeleo. Wanaojua wanatumia vizuri. Kwa bahati mbaya wapo watu ambao hawajaelewa thamani ya muda hawatunzi muda mahali wanapo hitajika.

Kuna mtu alisema hivi: nilipokuwa mtoto sikuwa na cha kufanya zaidi ya kutambaa na kusubiri nisaidiwe hiki na kile, wakati huo muda ulikuwa unatambaa. Nilipokuwa kijana nilianza kuona hili na lile, nikawa ninaongea pia, lakini muda ulianza kutembea. Nilipokuwa mtu mzima tayari ninajua maana ya maisha, nilianza kushughulika na mambo muhimu, muda ulikuwa unakimbia kweli. Nimekuwa mzee, ninataka nirekebishe nilipokesea, muda umepaa! Haupo tena! Mhubiri anasema vizuri: ”Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako kabla hazijaja siku utakaposema…” (Mhubiri 12:1). Usipotumia wakati vizuri, utakuja kujuta!
Bwana Yesu alionesha kuwa wana wa ulimwengu, yaani walio wa ufalme wa giza wanajua kuutumia wakati (Luka 16:8). Lakini wana wa nuru ni wazito kweli! Kwa nini wana wa ulimwengu wanajua kuukomboa wakati? Mkuu wao anajua kuwa anao muda mfupi sana! Kwa hiyo amejipanga vya kutosha na watumishi wake wanamtii! Watu wa Mungu, tusipoukomboa wakati, tutapoteza dira. Mambo mengi yataharibika na hivyo tutamletea hasara Bwana wetu pasipo sababu! Lazima tuenende kwa hekima na kuuomboa wakati!

7. MANENO YENU YAJAE NEEMA NA MUNYU NA MPATE KUJUA JINSI YA KUJIBU
Njia nyingine ya kumtangaza Kristo ilikuwa ni kwa njia ya usemi wao. Anasema maneno yao yawe na neema na munyu. Yawe na chumvi ambayo kazi yake ni kutunza kitu kisiharibike na kutia ladha nzuri. Na busara (hekima iliyo katika matendo) ingewawezesha hata kujua jinsi ya kumjibu kila mtu. Walipaswa kujibu kufuata mafundisho ya biblia sio kwa jinsi wanavyojifahamu. Na kwa vile walidhaniwa kuwa wajinga wasio na akili, basi kwa njia ya usemi wao wangedhihirisha kuwa sio watu wa kawaida. Walitakiwa kutafuta neema ya kuwa wazungumzaji wazuri.

8. JUMLISHO
Kuenenda kwa hekima katika ulimwengu ulioanguka sio rahisi. Yesu alipokuwa anawatuma wanafunzi kwenda kuhubiri aliwaambia, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kuweni na hekima kama nyoka lakini wanyenyekevu kama njiwa. Kondoo wakati wote yupo na mchungaji wake. Bwana Yesu anatutaka tujue kuwa peke yetu hatuwezi. Ndio maana hapa Paulo anakaza kuomba na kuombeana. Mbwa mwitu wapo kila mahali, tena hata mahali tunapodhani tupo salama. Bila Mungu kutufumbua macho, hatutastahimili. Tunamhitaji Bwana wakati wote. Ndio maana tunaambiwa tuenende kwa hekima. Hekima ya kweli hutoka kwa Bwana. Tukiwa na Bwana, tunahakikishwa hekima. Atatuwezesha kunena na kutenda kama itupasavyo. Lililo kuu katika kuenenda kwetu, tuukoboe wakati. Maana tupo kwa kitambo. Muda hautusubiri. Basi Mungu aliyetuita atuwezeshe kuenenda kwa hekima nyakati zote. Amen

Na mchg. Dkt. George Mark Fihavango
Askofu
From Mwinjilist Joseph Mshana