IBADA YA TAREHE 06 AGOSTI 2023 SIKU YA BWANA YA 9 BAADA YA UTATU

Somo:TUENENDE KWA HEKIMA
ZABURI 119:161–168; MATHAYO 10:5–15, MITHALI 1:1–7*
WIMBO: TMW 294
MAFAFANUZI
1. UTANGULIZI: Mithali 1:1
Kitabu kinaitwa Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa misemo ya hekima kuhusu hali halisi ya maisha ya kila siku yenye busara na haki ikigusa mada mbali mbali. Kitabu kinatoa mafundisho yenye mafumbo ambayo yalikuwa ya kawaida katika Maisha yao ya wakati ule. Ni misemo mifupi mifupi ambayo ni rahisi hata kuikariri. Kama vile Mfalme Daudi alivyo chimbuko la Zaburi katika Israeli ndivyo Mfalme Sulemani alivyo chimbuko la hekima katika Israeli. Inatajwa kuwa Sulemani aliandika Mithali 3,000 na nyimbo 1,005 wakati wa maisha yake (1 Wafalme 4:32–34). Na wakaenda Mataifa yote kwa Sulemani ili waisikie hekima yake.

Kitabu hiki kinaitwa Mithali za Mfalme Sulemani wa Israeli, lakini ni hakika kwamba Sulemani hakuziandika zote. Nyingine zinatajwa kuwa ziliandikwa na Aguri bin Yake (Mithali 30:1–33) na Mfalme Lemueli (Mithali 31:1–9), na wengine wametajwa kuwa wenye hekima bila kutajwa majina yao (Mithali 22:17 na 24:23). Mkazo ni kufundisha hekima ya jinsi ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Sura nne za kwanza ni mkazo juu ya asili ya hekima na umuhimu wake na sura zinazofuata ni mkusanyiko wa mistari miwili miwili mifupi yenye mithali zenye nguvu zinazogusa mambo mbali mbali ya maisha kama ndoa, upendo, uvivu, bidii ya kazi, maonyo kuhusu ulevi na uasherati.

Mfalme Sulemani alifahamika kwa umaarufu na upekee wa hekima ya ajabu. Sulemani alipopewa nafasi na Mungu katika ndoto ya kuomba jambo lolote atakalo, aliomba hekima ya kuliongoza taifa la Israeli na Mungu alijibu ombi lake (1 Wafalme 3:3–13). Zipo habari katika kitabu cha Wafalme wa kwanza zinazoonyesha jinsi alivyotumia hekima aliyopewa na Mungu. Mfano maarufu ni wa kesi ya wanawake wawili makahaba ambao walimgombania mtoto aliye hai wakimkataa aliye kufa (1 Wafalme 3:16–28).

2. MITHALI 1:2-7 KUSUDI KUU LA KITABU
Mwanzoni kabisa mwa kitabu Sulemani anaelezea kusudi la kitabu cha Mithali. Ni kujenga maisha ya uadilifu yanayofaa kimwili na kiroho. Kumpatia msomaji hekima, busara na maarifa ya Kimungu. Yanatajwa makusudi makuu matatu:

(a) Ili kuwapa wajinga werevu (Mithali 1:4).
Kuwapa wajinga, au watu wa kawaida werevu au busara. Hao ni watu wasio wasomi, hawa ndio wenye kiu ya kupokea mafundisho. Kitabu hiki kinapaswa kuwafundisha hawa wasio na uzoefu ili kujua nini cha kufanya na wafanye namna gani katika maisha yao. Na kijana atapata utambuzi au ufahamu hata kwa mambo ambayo hakuyafahamu. Sifa moja wapo kubwa ya watu wa kawaida (simple people) au ambao wametajwa kuwa wajinga ni wepesi. Mithali 14:15 inasema: Mjinga huamini kila neno, bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. Huyu mtu ni mwepesi au hata inaweza kusemwa kuwa ni mjinga, anaweza kuwa na maoni lakini akakosa hoja za nguvu.

(b) Kuwapa vijana maarifa na tahadhari (Mithali 1:4)
Vijana na wale watu wepesi wapo kuelekea utu uzima au kwenye hekima. Kitakachowapa tahadhari na uchaguzi sahihi katika maisha haya ni kukubali kufundishwa hekima. Hata nyakati za sasa kuna mambo mengi yanahitaji kuchambua kwa hekima na kuishi maisha ya tahadhari. Nyenzo ya kuishi maisha ya tahadhari ni hekima.

(c) Kuwaongezea elimu wenye hekima na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia (Mithali 1:5-6) waweze kuishi maisha ya uadilifu.

Kumbe kitabu cha mithali hakipo kwa ajili ya wajinga na wale wasio na uzoefu tu bali hata kwa wale wenye hekima. Kwa kupitia mafundisho ya mithali hizi wenye hekima wataongezewa elimu zaidi na zaidi. Mwenye ufahamu atafikia mashauri yenye njia, yanayomwezesha kutatua matatizo magumu kama ilivyokuwa na mfalme Sulemani alipoletewa kesi ya wale wanawake wawili waliogombania mtoto. Kumbe hakuna mwisho katika kutafuta maarifa na hekima.
Anasema mithali zinampelekea mtu kujua hekima na adabu, kutambua maneno ya ufahamu na kufundishwa matendo ya busara katika haki na hukumu na adili. Katika kujua hekima ifahamike kwa kizazi chetu kinaitwa cha habari na upeanaji wake (information age) lakini sio wengi katika kizazi hiki wanaotafuta hekima. Kujua maneno ya ufahamu maana yake yameandikwa yanapaswa kusomwa au kuangaliwa. Mithali 3:21 anasema Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, shika hekima kamili na busara.
Kujua hekima: Kuna tofauti kati ya hekima (wisdom) na maarifa (knowledge). Mtu anaweza kuwa na maarifa au ufahamu lakini asiwe na hekima. Kwani maarifa (knowledge) ni mkusanyiko wa ukweli wa mambo (facts about things) lakini hekima (wisdom) ni matumizi sahihi ya vile ambavyo tunavifahamu katika maisha yetu. Maarifa au ufahamu (knowledge) yanaweza kutuelezea namna mfumo wa utawala wa fedha lakini hekima ndiyo itasimamia matumizi sahihi ya fedha, kwa mfano kusimamia makisio ni hekima zaidi kuliko utaalamu. Shida yetu leo watu wengi wamejikuta wanatafuta fedha na sio hekima. Wengi tunaweka nguvu katika kupata elimu na sio hekima. Swali linakuja, hekima inatafutwaje? Mithali 1:7 na Zaburi 111:10 zinaweka wazi kuwa kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima. Kumbe hekima na maarifa vyanzo vyake ni kumcha Bwana. Na ukienda kwa Ayubu 28 unaona maelezo marefu kabisa.
Kufundishwa matendo ya busara/hekima
Mithali zipo kama shule au chuo cha hekima. Lakini tuingie chuoni tukiwa na moyo pamoja na akili wazi kupokea mafunzo. Tukifanya hivi haki, hukumu na adili/usawa vitatokea katika maisha yetu.

Lakini msingi mkuu wa hekima na maarifa ni kumcha Bwana ambacho ndicho chanzo cha maarifa yote (Mithali 1:7; Zaburi 111:10). Kitabu cha mithali kimeweka mkazo wake katika mambo halisi ya maisha na sio nadharia. Lakini kinatupa ukweli kwamba msingi ni fundisho la kitheologia kuwa maarifa na hekima yanatokana na kumcha Mungu, kuwa na hofu ya Mungu. Hofu ya Mungu ni kumjua Mungu, kujitoa kwa Mungu, kujinyenyekesha kwa Mungu.

3. TUENENDE KWA HEKIMA
Wiki iliyopita tuliongozwa na kichwa kinachosema uchaguzi wa busara na leo tunazunguzia hekima. Mara nyingi tunajikuta tunatumia maneno haya mawili kwa wakati mmoja, hekima na busara. Nimeeleza kwa kirefu tofauti zake katika kitabu cha Mafafanuzi ya Mahubiri ya mwaka 2020 ukurasa wa 199 na ukurasa wa 205. Kwa haraka utaona kuwa hekima ni pana kuliko busara. Hekima inasimama kama usukani wa kuendesha busara.

Somo letu linatuhimiza kuenenda kwa hekima katika dunia ambayo imebadilika mno katika mfumo wake. Mahusiano katika ndoa yameingia changamoto kubwa mno. Migogoro katika ndoa ni mingi. Ukiangalia kwa undani utagundua kuwa kuna vitu vya msingi vinakosekana. Maarifa ya maisha ya ndoa na hekima za Kimungu zimekosekana. Na mahali fulani imeelezwa kuwa ndoa za watu walioenda shule ndio zinaongoza kuleta shida, kumbe maarifa na elimu vimeshindwa kuleta maelewano katika ndoa. Biblia imeshatuambia chanzo cha maarifa na hekima ni kumcha Bwana. Mungu asipopewa nafasi halisi katika maisha yetu hakuna usalama.

Hata wale wanaoonekana kama wacha Mungu, watu wa dini sana wamepata shida hiyo hiyo kwa sababu ya kukosekana kwa misingi ya kweli ya neno la Mungu. Akili zimeshindwa kufundishika. Neno linasema: Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama (Zaburi 32:8). Mfano wa ndoa ni mmoja tu. Zipo changamoto nyingi zaidi ya hizo ambazo zinahitaji hekima za Mungu.

Kuna hitaji hekima katika malezi ya watoto na mahusiano kati ya wazazi na watoto, katika kutunza mazingira yetu, katika kutafuta na kutumia fedha.

Mambo yote haya kwa kutumia maarifa yetu hatuwezi kuyamudu, maana adui yupo kazini wakati wote. Tunahitaji uongozi wa Mungu. Na uzuri wake ni kwamba, ndani yetu huishi Roho wa Mungu. Huyu ndiye hekima yetu na mwongozo wetu kwa kila jambo. Maana yake, ili kuenenda kwetu kuwe kwa hekima, lazima tuhakikishe tupo na yeye aliye asili ya hekima. Mungu atusaidie tumpe nafasi Roho wake maana ni katika yeye tutakuwa na hekima na hivyo tutaweza kuenenda kwa hekima. Amen.