MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 1 BAADA YA UTATU TAREHE 14/06/2020

MADA: MUNGU AU ULIMWENGU

MASOMO:
ZABURI 78: 17 – 22
YOHANA 7:40 – 52,
MATENDO YA MITUME 5: 34 – 42

SHABAHA: Wasilkilizaji waweze kutambua kuwa uchaguzi sahihi nu ule wa kuchagua Mungu kwa sababu wakati wote yupo sahihi.

UTANGULIZI
Biblia inatufundisha kuwa Mungu sio nguvu Fulani tu inayomuwezesha mwanadamu kufanya jambo Fulani bali ni nafsi hai na hili huonekana wazi mtu unapokubali kumjia yeye na kupata mahusiano na ushirika nae (Yn 17:3)

Mungu ni nafsi hai iliyojidhihirisha kwenye nafsi tatu ili kumsaidia mwanadamu asibaki tu na ujuzi mdogo au hisia tu.(Yer 1:1 – 3, 2Pet 1:21)

Mungu ni wa milele asiyetawaliwa. Hawezi kupimwa kwa kipimo cha wakati, kwa sababu yeye hana mwanzo wala mwisho (Zab 90:2, Isa 48:12, Yn 5:26) Hana haja ya kutoa hesabu mahali popote wala kwa kiumbe chochote na hana haja ya kutoa sababu kwa uamuzi wake wala kuelezea matendo yake (Zab 115:3, Mdo 4:48) ingawa katika neema yake mara nyingine anafanya hivyo (Mwa 18:17 – 19, Efe 1:9) Hekima yake haina kikomo na hivyo iko nje ya uwezo wa mwanadamu ( Zab 50: 10 – 13, Mdo 17:24 – 25) Jambo lolote analolitenda analitenda kwa sababu ameamua hivyo, wala si kwa sababu alilazimika kufanya hivyo (Efe 1:11)
Mungu ni mwenye enzi na mamlaka yote. Hakuna kikomo kuhusu kuwepo kwa Mungu au ujuzi wake. Jambo hili ni kweli kwa furaha na hofu. Kwa furaha sababu hakuna mtu amtegemeaye ataweza kutengwa naye; na kwa hufu kwa sababu hakuna dhambi inayoweza kufichwa mbele zake ( Zab 139: 1 – 12, Ebr 4:13).

Mungu habadiliki lakini anajibu na kuitikia, Mungu asiyebadilika maana yake hana kikomo wala mwanzo wala mwisho hivyo hana namna ya kuongeza au kupunguza hali na sifa zake. (Kut 34:6 – 7) kutokubadilika kwa Mungu kuna maana kuwa yeye ni thabiti katika matendo yake yote(Ebr 6:17 – 18, Yak 1:17)

Biblia inaeleza ulimwengu ni vitu vilivyoumbwa na Mungu au watu wanaoishi katika ulimwengu (Zab 90:2, 98:7,9) kwa sababu ya dhambi ulimwengu ulikuwa sehemu ambamo shetani anatawala katika maisha ya watu (Yn 12:31, Rum 5:12 1Yoh 5:19) mara nyingi biblia inasema juu ya ulimwengu kuwa ni jambo lililo ovu au kinyume cha Mungu (Yn 7:7, Yak 4:4). Ulimwengu katika maana hii ni jambo la wanadamu wenye dhambi pamoja na tabia mbaya zilizo alama za wanadamu wenye dhambi.

Mkristo hawezi kushinda majaribu ya ulimwengu kwa kutumia mbinu za ulimwengu. Njia moja tu ya kushida ulimwengu ni kutegemea nguvu ya Kristo, aliyemshinda shetani aliye mkuu wa ulimwengu huu (Yn 12:31, 1Yoh 5: 4 – 5)
Kwa kuzitegemea nguvu za Mungu wanadamu wanao uwezo wa kuushida ulimwengu na kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Wote tunaalikwa kati ya Ulimwengu na Mungu basi tuchague Mungu Huku tukifahamu haya ambayo neno la Mungu linatufunza katika somo nililolisoma kuwa:-

1. KAZI YA MUNGU HAIHITAJI KUJIHURUMIA KULIKO KUMTEGEMEA YEYE
 Wanafunzi wakiwa na ujasiri wa hali ya juu pamoja na kutambua wivu uliotawala kwa ajili ya mafanikio yao, huku wakiwa wamepigwa marufuku kali kufundisha kwa kutumia jina la Yesu na ufufuo wake na wakitambua mamlaka ya baraza lile na uwezo wa wanachoweza kuwafanyia hata kuwaua ila waliendelea kuwaeleza wazi kuwa wao ndio waliomuuua Yesu pasipo kujali nini kitawapata kutokana na ukweli huo.

 Hii ndio kazi ya wakristo wote kutokufungia macho uonevu unaojitokeza na kueleza ukweli wote kwa yeyote pasipo kujali chochote ambacho kinataka kukuondoa kwenye imani ya kumtegemea Mungu

2. UKIWA NA UHAKIKA NA NGUVU ZA MUNGU MAMBO YA DUNIA HAYAWEZI KUYUMBISHA IMANI YAKO
 Jumapili iliyopita tulijifunza juu ya Farisayo aitwae Nikodemu ambaye alikuwa mwanafunzi wa siri wa Yesu Kristo ambaye alikuwa mwalimu wa torati, tajiri na aliyeheshimika na sasa wanafunzi wake wanapoanza huduma tunakutana na Mfarisayo mwingine ambaye ni mwalimu wa torati, tajiri na aliyeheshimika sana ambaye anaonyesha anakuballiana na mafundisho ya Yesu na anatoa maamuzi ya hekima kuwa mambo amabyo yameanza ambayo asili yake sio Yesu Kristo basi hufa ila kama yameanzishwa na msingi wa Yesu Kristo kamwe hayawezi kuvunjika na ni hatari kupambana nayo. Na Ushauri huu unapokelewa.

 Yanaweza kutokea mambo ambayo huyaelewi ila kwa vile una uhakika na nguvu za Mungu basi mwachie Mungu mwenyewe ni hakimu mwenye haki.

3. HATUHITAJI KUWAOMBEA MABAYA ADUI ZETU
 Wanafunzi wanachapwa viboko na wanapoachiwa wanaondoka kwa furaha kuwa wamehesabiwa mateso kwa ajili ya Yesu na wanadumu wakiomba na kufundhisha juu ya uweza na Mungu huku wakitambua kuwa ulimwengu hauwezi kuwafanya chochote.

 Adui zetu wakikaza kutuudhi nasi tuzidi kuongeza kiasi cha furaha yetu tukitambua kuwa nguvu za Mungu zitatupatia haki yetu.

HITIMISHO
Mungu atuwezeshe tuweze kumtumikia kwa uaminifu na ujasiri pasipo kuogopeshwa na vitisho vya wote wanaoukataa ukweli pasipo kujihurumia sababu Mungu mwenyewe asiyetawaliwa wala kubadilika atatulinda daima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *