KKKT DAYOSISI YA KUSINI ,JIMBO LA NJOMBE, USHARIKA WA UWEMBA,MTAA WA MJIMWEMA
MADA: KUNGOJEA AHADI YA BABA
MASOMO:
ZABURI 42:8 – 11,
YAKOBO 5:13 – 15
*YOHANA 16: 1 – 13
SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya Utakaso wetu kutuwezesha kufika mbinguni hivyo wasikilize maongozi yake.
UTANGULIZI
Leo tunajifunza juu ya kungojea ahadi za Mungu ambazo ametuahidi kwa ajili ya upendo wake kwetu na pia kwa ajili ya maombi ambayo tumepeleka kwake ambayo tunauhakika kuwa ameyasikia na yupo tayari kutujibu kwa wakati ambao ni sahihi kwake.
Katika somo hili la injili ya Yohana hapa Yesu anazungumza na wanafunzi wake akiwa na furaha kuwa anarudi kwa baba yake na huku wanafunzi wakiwa na huzuni kwa kuachwa na Yesu ila anaahidi kuwa atatupatia msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu.
Katika mistari hii yote tuliyosoma tunaweza kuona mambo mengi amabyo yanaleta elimu kubwa sana kwetu ila nataka tuyaangalie haya machache kwa siku ya leo.
1. YESU KRISTO NI NGAO YETU MAISHANI
Yesu akiwa anataka kuwapa habari wanafunzi wake kuwa atawaacha ila atawapa msaidizi anataka wanafunzi wake waelewe kuwa wakati akiwa nao chuki zote na adha zilielekezwa kwake kama kiongozi wao ila sasa anapoondoka watambue kuwa wao watabaki kama kiongozi hivyo chuki na adha zitaelekezwa kwao.
Habari hii inawahuzunisha wanafunzi ila Yesu anataka kuwaandaa wajue kuwa watapitia hayo ila wakiwa nae kwa njia ya Roho Mtakatifu atakayewalea baadae basi wataweza kuvumilia.
Maisha ya mtu aliye ndani ya Yesu Kristo yanaweza kupita katika chuki, dhiki na mateso ila ukiwa na Yesu atakuwezesha kuyastahimili yote na kuvuka salama.
Maisha nje ya Yesu ni maisha yaliyo rahisi kushambuliwa na kuumizwa na hata kufa hivyo tusiondoke kwenye mikono salama ya Yesu Kristo.
2. ROHO MTAKATIFU NI MSAIDIZI AMBAYE KILA MTU ANAPASWA KUWA NAE.
Yesu anaahidi kuwa wanafunzi wake wasihuzunike sana sababu atawapa msaidizi ambaye atafanya mambo kadhaa katika maisha yao
a. Atawatetea na kupambana na wapinzani wao
b. Kuwafundisha na kuwasaidia kuelewa mambo ya sasa na baadae
Ni kweli tunahitaji mtetezi na mfundishaji wa kweli iti tuwee kuelewa mambo yanayoendelea kwenye maisha yetu na ulimwenguni kwa ujumla.
Yapo mengi yanayotuumiza na kututesa na yapo mengi ambayo tunajitahidi kuyaelewa ila bado hatujayaelewa hivyo msaidizi huyu tuliyeahidiwa ambaye ni Roho Mtakatifu ktujitahidi aweze kuwepo katika maisha yetu wakati wote.
3. HUZUNI HUTUONDOA KWENYE MPANGO WA MUNGU
Kuhuzunika sio kubaya ila kuhuzunika kunakopelekea mtu kupoteza matumaini huko ni njia ya kutuelekeza kuondoka kwenye mpango wa Mungu.
Tunawaona wanafunzi walikuwa na huzuni hadi wakashindwa kuona furaha ya Yesu kurejea kwa baba yake na pia wakawa hawaelewi waliyokuwa wanaambiwa na Yesu hivyo Yesu akawaambia itabidi niache kuzungumza nanyi hadi Roho Mtakatifu atakapowajia awafundisha yote yanayotoka kwangu.
a. Huzuni inaweza kukufanya ukawa mbinafsi na kujipendelea pasipo kutazama wengine na Baraka wanazoweza kupata kwa maamuzi wanayofanya kama wanafunzi walivyojifikiria wao tu na kushindwa kumfikiria Yesu Kristo
b. Huzuni inapelekea kushindwa kusikiliza sauti ya Mungu na hata kusababisha Mungu acheleweshe ujumbe ambao alitaka kukupa kama Yesu alivyofanya kwa wanafunzi wake.
4. SIKU ZOTE YESU NI MSHINDI
Ulimwengu unaweza kufikiria umeshinda kwa kumtesa Yesu na wanafunzi wake lakini utalipa kwa dhambi zake wakati Mungu atakapotangaza hukumu.
Ulimwengu utahukumiwa juu ya dhambi yake ya kutokumwamini Yesu Kristo ambaye hutupatia haki ya kweli kwa njia ya kifo, kufufuka na kupaa kwake kwenda mbinguni.
Mwanzoni unaweza kufikiri umeshinda kwa kuwanyanyasa, kuwaonea na hata kuatesa watu wa Mungu lakini ukweli ni kuwa Mungu hatakubali ufanye hivyo wakati wote lazima atakufikisha kwenye hukumu hivyo tujitahidi kukaa na Yesu aliye mshindi wakati wote hata kama tunapitia magumu.
HITIMISHO
Mungu atusaidie tuendelee kudumu katika kumwamini yeye kwani yeye ndie anayeyajua maisha yetu atatulinda na kutushindia wakati wote.
AMEN
Asante mtumishi wa Mungu
Ubarikiwe mpendwa
Amina