MJUE ADUI YAKO.

Watu wengi tuna hasira, uchungu, ghadhabu, maumivu, mapambano, chuki na kisasi na mashindano mengi moyoni, tukiamini kabisa kuna watu waliotusababishia hali hiyo, watu tunawaona wabaya, maadui, tunawaita wakarofi na majina mengi tuwezavyo kuwaita. Wanaweza kuwa watu wa mbali ama wa karibu, aweza kuwa mke au mume, mchumba au rafiki, jirani, mfanyakazi mwenzako, ama yeyote yule unayehisi kakukosea.
Lakini leo nataka nikuambie adui yako mkubwa wala si huyo unayemdhani, huyo ni msaidizi tu wa adui yako, adui yako yuko ndani yako mwenyewe, anayekuumiza, anayekutukana, anayekuadhibu, anayekunyanyasa yuko ndani yako na kwa kuwa umeshindwa kummudu ndio maana hasira zako na lawama zako umezihamishia kwa msaidizi wa adui yako ambaye ndio yule unayemdhania.

Umewahi jiuliza? Kabla hujachukia ndani yako lazima kuna sauti mbili zilishindana, moja ikakuambia usichukie nyingine ikakuambia haiwezekani utaonekana mjinga, ile sauti iliyoshinda ya ubaya ndiyo adui yako mkubwa, maana kinyume cha hapo wala usingefanya maamuzi hayo. Umemuadhibu bure mtu wa mbali lakini ulipaswa kumwadibisha mtu wako wa ndani kwa wema na hapo ungeweza kujisamehe kabla hujaadhibu unayedhani kakukosea.

Adui wa ndani ni mbaya kuliko wa nje, maana kama nje kukiharibika utakimbilia ndani kupata usalama, ila ndani kukiharibika jua huna pa kukimbilia, na huyo adui akikushinda kabisa atakuua au kukusababishia madhara mengi kiakili na kiafya, NDIO MAANA USISHANGAE MTU KAJIUA AU KAJIDHURU JUA KASHINDWA VIBAYA NA ADUI YAKE WA KARIBU AMBAYE NI YEYE MWENYEWE.

Biblia haijakosea inaposea LINDA SANA MOYO WAKO, KULIKO YOTE UYALINDAYO, MAANA HUKO NDIKO ZITOKAKO CHEMICHEMI ZA UZIMA. najua mpaka sasa adui wa ndani bado anakushawishi uupuuze ujumbe huu, ni lazima umshinde kama kweli unataka amani ya ndoa yako, kazi yako, jirani yako, ndugu zako nk. Ukimshinda adui wa ndani hakuna adui nje kamwe ila ukishindwa na adui wa ndani basi kila atakayekugusa iwe bahati mbaya au makusudi basi atakuwa adui yako.

Mungu akupe kuelewa haya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *