10/05/2020 KANTANTE DOMINION-MWIMBIENI BWANA WIMBO MPYA

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 4 BAADA YA PASAKA TAREHE 10/05/2020

MADA: MWIMBIENI BWANA WIMBO MPYA

MASOMO: ZABURI 100: 1 – 6, UFUNUO 15: 1 – 4, *ZABURI 69: 29 – 36

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa aina ya maisha wanayoishi haiondoi uwezo wa Mungu katika kuwaokoa wazidi kumtegemea.

UTANGULIZI
 Bwana Yesu asifiwe, Leo ni jumapili ambayo kila mtu awe mwenyewe, au katika familia, au katika kundi kwa pamoja tunaalikwa kumuimbia Mungu wimbo mpya.

 Upya wa wimbo sio maneno mapya yaliyotungwa katika umahiri wa kisanii bali ni moyo unaomaanisha kile unachokitamka katika hali unayopitia kwa matumaini makubwa kuwa Mungu atafanya.

 Katika kutafakari mada hii tunatafakari neno la Mungu kutoka kitabu cha Zaburi 69: 29 – 36 ambapo tunamuona muimba zaburi akitambua hali ya uhitaji na umsikini alionao ila haimzuii kuamini kuwa Mungu atamponya yeye, na wote wanaomtegemea na sio wanaomtegemea tu hata taifa lake litaokolewa hivyo ataendelea kuimba nyimbo za furaha ya matumaini na kumshukuru Mungu kwa wokovu aliompatia yeye, ndugu, jamaa na marafiki zake na hata taifa lake.

Katika kisa hiki tunajifunza mambo makuu yafuatayo:-

1. MUNGU HUBAKI KUWA MUNGU BILA KUJALI CHOCHOTE UNACHOPITIA
 Wakati mwingine katika maisha hufikiri kuwa tunapopitia katika hali zinazosababisha maumivu, wasiwasi na uhitaji labda Mungu ametuacha na hata watu wengine hujitahidi kuficha hali wanayopitia ila ukweli unabaki kuwa Mungu habadilishwi na hali unayoipitia bado anabaki kuwa Mungu.

 Mwimbaji wa Zaburi analionyesha hilo kuwa japokuwa ni maskini mhitaji mwenye wasiwasi na maumivu makali ambayo hakustahili ila hayupo tayari kutafuta msaada kwa mtu au kitu kingine chochote zaidi ya kumtafuta Mungu sababu ana uhakika kuwa kitakachomuokoa na kumuinua tena ni WOKOVU WA MUNGU PEKE YAKE

 Moyo wenye shukrani juu ya wokovu huu utajidhihirisha kwenye kumsifu Mungu (Moyo wenye shukrani wakati wote una wimbo wa kumtukuza Mungu.)

 Huduma za kiroho kama vile kumsifu Mungu(Kuimba nyimbo mbalimbali), Kumuabudu Mungu, kumuomba Mungu vina umuhimu zaidi ya sadaka.

2. MAISHA YA SIFA YANAIMARISHA IMANI ZA WAAMINIFU WANAOPITA KATIKA KIPINDI CHA MATESO
 Maisha ya kumsifu Mungu sio kwamba yanakuimarisha wewe peke yako na kukupatia wokovu bali wote amabo wanatazama jinsi Mungu anavyokuokoa nao wataimarika imani zao.

 Mungu ataweka tofauti kati ya watu wanaomtegemea na wale wasiomtegemea kwani yeye ni Mungu:-

a) Anayeleta furaha kwa wote wanaoonewa,

b) Hufufua mioyo iliyokata tamaa na matumaini,

c) Husikiliza maombi ya wahitaji wote,

d) Huwafungua wafungwa wote.

 Katika kipindi hiki tunachopitia changamoto ya ugonjwa huu wa COVID 19 na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu tubadili namna ya kukabiliana nao sio kila siku kupokea habari mbaya tu. Sasa tuelewe kwamba ugonjwa upo na unaua tena kwa haraka hivyo tuchukue tahadhari na tuendelee kumsifu Mungu. Niliona wakati Raisi wetu anaposema tuombe nchi nyingi zilimbeza sana ila sasa nimeanza kuziona nazo zinafuata utaratibu huu wa maombi.

 Maombi yameondoa hofu kwa watanzania na sasa imeanza kuambukiza na nchi nyingine kuwasaidia watu wake kuondoa wasiwasi. Sisi tuongeze bidii kumuomba Mungu na kumsifu daima.

3. MUNGU MWENYE UWEZO WA KUOKOA MTU MMOJA ANAO UWEZO WA KUOKOA TAIFA.
 Kama watu mbalimbali wanamsifu na kumuabudu Mungu na wokovu unatokea katika maisha yao, basi uwezo huo pai unaweza kutenda kazi katika taifa. Tunapoona taifa linataka kuanguka au tayari limeshaanguka tukimuita Mungu wetu kwa kweli atatusikia na kuliokoa taifa letu.

 Muimba zaburi anaeleza kuwa Mungu ataliokoa taifa la Yuda na watu watakaa na kumiliki, wale wanaomtumaini Mungu watarithi na wote wanao mtumaini hakika watakaa katika miji iliyookolewa.

 Wale kweli ambao wataelekeza tumaini lao kwa Mungu katika hali zote ni kweli nchi itaokolewa na watu watabaki hai kwa ajili ya kuishi wakimsifu Mungu.

HITIMISHO
Mungu hawezi kugeuzwa na hali yoyote ya kibinadamu bali wote wanaomtumainia hakika wataokolewa wao pamoja na familia zao na nchi yao.

AMEN.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *