MAHUBIRI YA SIKU YA 5 BAADA YA PASAKA TAREHE 17/05/2020 IITWAYO ROGATE MAANA YAKE OMBENI.

KKKT DAYOSISI YA KUSINI, JIMBO LA NJOMBE MJINI, USHARIKA WA UWEMBA, MTAA WA LUSITU.

MAHUBIRI YA SIKU YA 5 BAADA YA PASAKA TAREHE 17/05/2020 IITWAYO ROGATE MAANA YAKE OMBENI.

MASOMO: ZABURI 107:1 – 8, MARKO 10:46 – 52, *MATENDO YA MITUME 12:5 – 17

MADA: OMBENI KATIKA JINA LA YESU KRISTO

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kutambua kuwa wakiomba kwa Jina la Yesu Hakika watapokea majibu yao hivyo waelekeze maombi yao kwake.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, Jumapili ya leo tunajifunza juu ya kuomba kwa kutumia Jina la Yesu Kristo ambalo ndio msaada wetu wakati wote( Wafilipi 2: 9 – 11)

Kwa kuutazama ukweli huu tumepewa kujifunza kutoka kitabu cha maendo ya Mitume 12: 5 – 17 ambapo tunapata habari za Petro kufungwa gerezani na Kanisa linakutana vikundi vikundi na kumuomba Mungu anayeleta msaada wa kweli kwa kanisa na kwa Petro mwenyewe.

Katika habari hii tunaweza kujifunza haya yafuatayo:-

1. KATIKATI YA NDORUBA UKIWA MIKONONI MWA MUNGU ANAKUPA AMANI
 Hapa tunaona jinsi ambavyo Petro akiwa amefungwa gerezani katikati ya ulinzi Mkubwa, amefungwa minyororo kwenye miguu na kikono tena kwenye chumba cha ndani na siku chache zilizopita rafiki yake na mtumishi mwenzake Yakobo ndugu yake Yohana aliuwawa lakini yeye anapata Usingizi tena tunaambiwa alilala fofofo.

Usingizi una mafundisho mengi na siku ya leo tujifunze moja juu ya Usingizi

 Wakati wa matatizo, shida na dhiki ni vigumu sana kupata Usingizi ( Esta 6:1,Ayu 3:13)

 Mungu anaporuhusu Usingizi kwa mtu wake anataka kuleta mwanzo mpya (Mwa 2:21, 28:16,)

 Katikati ya dhoruba Mungu humpa rafiki yake Usingizi akitaka atulie na kuwa na amani tayari kupokea Baraka. (Zab 3:5,127:2)

 Kwa maelezo hayo unaona jinsi ilivyokuwa vigumu Petro kupata Usingizi ila kwa ajili Petro alijua kuwa maono yay eye kulijenga kanisa hayajakamilika na aliahidiwa na Mungu kuwa atalala akiwa mzee.

 Maisha yetu yamejaa dhoruba nyingi, mateso mengi na mahangaiko ila bado Mungu anabaki kuwa Mungu kwetu, ukiangalia hasa katika kipindi hiki cha Ugonjwa huu waCOVID – 19 mahangaiko ni mengi kila mahali ila tusiache kuelekeza imani yetu kwa Mungu yeye atatupa amani na matulizo ya kweli a Ushindi wa kutosha

2. MUNGU ANAPOANZA KUTENDA HUTENDA ZAIDI YA ULIYOTAZAMIA NA KUKUACHA KWENYE MSHANGAO
 Mungu anapofanya ukombozi katika maisha yetu sio kwamba anatushangaza sisi wenyewe bali hata wale waliotuzunguka wanabaki kushangaa.

 Wakati Petro amelala Mungu ameruhusu kanisa kuomba kwa ajili ya Petro na Petro anapookolewa anashangaa na kanisa lililokuwa linamuombea nalo linashangaa wote Petro na Kanisa wanapoona ukuu wa Mungu wanafikiria ni ndoto kumbe ni Mungu yupo kazini.

 Yapo mambo ambayo tunaona kuwa hayawezekani kabisa ila tukiingia kwenye maombi yanawezekana kwa kiwango ambacho hata sisi wenyewe hatuwezi kuamini ila ukweli unabaki kuwa Mungu ni mwaminifu kwetu na hataacha kututendea mazuri wakati wote tunapoelekeza tumaini letu kwake.

*3. MAOMBI HUFANYA YOTE YAWEZEKANE*
 Shetani anapokupata anahakikisha kuwa anafunga kila njia ambayo anaona inaweza kukusaidia kunusurika katika mikono yake. Tunaona Jinsi ambavyo Petro alivyokamatwa na kufungwa chumba cha ndani na hiyo ikawa haitoshi wakamfunga kwa minyororo na hiyo ikiwa bado haitoshi wakamuwekea na walinzi ila Kanisa linapoomba hakuna kifungo kinachozua Petro kuwa huru tena uhuru ulioleta uhai kwa kanisa.

 Kanisa tusichoke kuomba katika nyakati zote hata pale kwa akili zetu za kibinadamu tunapoona mambo hayawezekani ila kwa Mungu yanawezekana sana. OMBA, OMBA OMBA NA USICHOKE KUOMBA HADI HAPO MUNGU ATAKAPOJIBU MAOMBI YOTE SABABU HAKIKA ATAYAJIBU.

HITIMISHO
Mungu aliyemtoa mwanae wa pekee tuendelee kumtegemea tukilitaja jina lake ambalo kwa hilo tunapokea majibu yetu.
AMEN.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *