MAHUBIRI YA SIKU YA PENTEKOSTE (Holy spirit reveal) 31/05/2020

1.0 UTANGULIZI
 Jumapili ya Leo neno la Mungu linatukumbusha kuwa Roho mtakatifu ni Msaada wetu katika maisha yetu.
 Roho Mtakatifu anatuwezesha kila Mkristo, bila kuzingatia, umri,jinsia au hali ya mtu katika jamii, ili kutoa unabii, kuota ndoto, na kuona maono.
 Roho Mtakatifu anawashukia waumini wote ili kutusaidia kufanya kazi ya Mungu hapa duniani na kutulinda ( Kut 31:2 -3, Hes 11:29, Zab 51:11)
 Roho mtakatifu ni muhimu sana katika kanisa la Mungu kwa sababu anatusaidia kuishi maisha matakatifu na kutimiza mpango wa Mungu katika maisha yetu..
 Katika unabii ambao tumeusoma kutoka kitabu cha Yoel tunaona kuwa ulitimia siku ilie ya Pentekoste na Petro aliyarudia maneno haya (Mdo 2:16 – 21)
 Katika unabii huu tunajifunza mambo kadhaa

2.0 ROHO MTAKATIFU YUPO KUWASAIDIA WATU WOTE
 Yoel anatabiri kuwa Roho atawashukia watu wote na rika zote ili kuwasaidia, ili Mkristo uweze kusaidiwa unapaswa kutulia katika utakatifu na Roho Mtakatifu aweze kukupa Muongozo sahihi.
 Ukiwa umefanikiwa sana usiache kumtumikia Mungu kwa sababu bado kuna mazuri zaidi ya hayo yapo mbele yako ambayo Mungu amekuandalia.
 Ukiwa katika mateso, maumivu na changamoto za dunia usikate tamaa sababu bado kidogo kuna siku njema zinakuja ambazo Mungu amekuandalia.

3.0 HATARI IPO KWA WALE WATAKAOMKANA ROHO MTAKATIFU
 Yoeli anatukumbusha kuwa ipo siku ya Hukumu inayokuja mbele yetu na kwa wale maadui wote wa Mungu siku hiyo itakuwa mbaya sana kwao sababu yatatokea mambo mengi ya ajabu.

4.0 KILA ATAKAYEMKUBALI ROHO MTAKATIFU ATAOKOLEWA.
 Neno la Mungu linatuhakikishika kuwa pamoja na dhambi nyingi kuongezeka na watu kumuacha Mungu ila wapo watu ambao bado wataendelea kumtegemea Mungu na anasema hao wote ambao wataendelea kumtegemea wakimuita jina lake hakika atawaokoa.

5.0 HITIMISHO
 Kila Mmoja atulie katika maongozi ya Roho Mtakatifu ili tupate kulindwa na kuelekezwa katika maisha ya Utakatifu.
AMEN.

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA KABLA YA PENTEKOSTE EXAUD MAANA YAKE SIKIA KUOMBA KWETU TAREHE 24/05/2020

KKKT DAYOSISI YA KUSINI ,JIMBO LA NJOMBE, USHARIKA WA UWEMBA,MTAA WA MJIMWEMA

MADA: KUNGOJEA AHADI YA BABA

MASOMO:
ZABURI 42:8 – 11,
YAKOBO 5:13 – 15
*YOHANA 16: 1 – 13

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya Utakaso wetu kutuwezesha kufika mbinguni hivyo wasikilize maongozi yake.

UTANGULIZI
 Leo tunajifunza juu ya kungojea ahadi za Mungu ambazo ametuahidi kwa ajili ya upendo wake kwetu na pia kwa ajili ya maombi ambayo tumepeleka kwake ambayo tunauhakika kuwa ameyasikia na yupo tayari kutujibu kwa wakati ambao ni sahihi kwake.

 Katika somo hili la injili ya Yohana hapa Yesu anazungumza na wanafunzi wake akiwa na furaha kuwa anarudi kwa baba yake na huku wanafunzi wakiwa na huzuni kwa kuachwa na Yesu ila anaahidi kuwa atatupatia msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu.

 Katika mistari hii yote tuliyosoma tunaweza kuona mambo mengi amabyo yanaleta elimu kubwa sana kwetu ila nataka tuyaangalie haya machache kwa siku ya leo.

1. YESU KRISTO NI NGAO YETU MAISHANI
 Yesu akiwa anataka kuwapa habari wanafunzi wake kuwa atawaacha ila atawapa msaidizi anataka wanafunzi wake waelewe kuwa wakati akiwa nao chuki zote na adha zilielekezwa kwake kama kiongozi wao ila sasa anapoondoka watambue kuwa wao watabaki kama kiongozi hivyo chuki na adha zitaelekezwa kwao.

 Habari hii inawahuzunisha wanafunzi ila Yesu anataka kuwaandaa wajue kuwa watapitia hayo ila wakiwa nae kwa njia ya Roho Mtakatifu atakayewalea baadae basi wataweza kuvumilia.

 Maisha ya mtu aliye ndani ya Yesu Kristo yanaweza kupita katika chuki, dhiki na mateso ila ukiwa na Yesu atakuwezesha kuyastahimili yote na kuvuka salama.

 Maisha nje ya Yesu ni maisha yaliyo rahisi kushambuliwa na kuumizwa na hata kufa hivyo tusiondoke kwenye mikono salama ya Yesu Kristo.

2. ROHO MTAKATIFU NI MSAIDIZI AMBAYE KILA MTU ANAPASWA KUWA NAE.
Yesu anaahidi kuwa wanafunzi wake wasihuzunike sana sababu atawapa msaidizi ambaye atafanya mambo kadhaa katika maisha yao

a. Atawatetea na kupambana na wapinzani wao

b. Kuwafundisha na kuwasaidia kuelewa mambo ya sasa na baadae

 Ni kweli tunahitaji mtetezi na mfundishaji wa kweli iti tuwee kuelewa mambo yanayoendelea kwenye maisha yetu na ulimwenguni kwa ujumla.

 Yapo mengi yanayotuumiza na kututesa na yapo mengi ambayo tunajitahidi kuyaelewa ila bado hatujayaelewa hivyo msaidizi huyu tuliyeahidiwa ambaye ni Roho Mtakatifu ktujitahidi aweze kuwepo katika maisha yetu wakati wote.

3. HUZUNI HUTUONDOA KWENYE MPANGO WA MUNGU
Kuhuzunika sio kubaya ila kuhuzunika kunakopelekea mtu kupoteza matumaini huko ni njia ya kutuelekeza kuondoka kwenye mpango wa Mungu.

Tunawaona wanafunzi walikuwa na huzuni hadi wakashindwa kuona furaha ya Yesu kurejea kwa baba yake na pia wakawa hawaelewi waliyokuwa wanaambiwa na Yesu hivyo Yesu akawaambia itabidi niache kuzungumza nanyi hadi Roho Mtakatifu atakapowajia awafundisha yote yanayotoka kwangu.

a. Huzuni inaweza kukufanya ukawa mbinafsi na kujipendelea pasipo kutazama wengine na Baraka wanazoweza kupata kwa maamuzi wanayofanya kama wanafunzi walivyojifikiria wao tu na kushindwa kumfikiria Yesu Kristo

b. Huzuni inapelekea kushindwa kusikiliza sauti ya Mungu na hata kusababisha Mungu acheleweshe ujumbe ambao alitaka kukupa kama Yesu alivyofanya kwa wanafunzi wake.

4. SIKU ZOTE YESU NI MSHINDI
 Ulimwengu unaweza kufikiria umeshinda kwa kumtesa Yesu na wanafunzi wake lakini utalipa kwa dhambi zake wakati Mungu atakapotangaza hukumu.

 Ulimwengu utahukumiwa juu ya dhambi yake ya kutokumwamini Yesu Kristo ambaye hutupatia haki ya kweli kwa njia ya kifo, kufufuka na kupaa kwake kwenda mbinguni.

 Mwanzoni unaweza kufikiri umeshinda kwa kuwanyanyasa, kuwaonea na hata kuatesa watu wa Mungu lakini ukweli ni kuwa Mungu hatakubali ufanye hivyo wakati wote lazima atakufikisha kwenye hukumu hivyo tujitahidi kukaa na Yesu aliye mshindi wakati wote hata kama tunapitia magumu.

HITIMISHO
Mungu atusaidie tuendelee kudumu katika kumwamini yeye kwani yeye ndie anayeyajua maisha yetu atatulinda na kutushindia wakati wote.

AMEN

MAHUBIRI YA SIKU YA ALHAMISI YA KUKUMBUKA KUPAA KWA YESU KRISTO TAREHE 21/05/2020

KKKT DAYOSISI YA KUSINI, JIMBO LA KUSINI, NJOMBE MJINI,USHARIKA WA UWEMBA
MTAA WA MJIMWEMA luponde.

Masomo:
ZABURI 47:1 – 9,
EBRANIA 8:1 – 5,
*LUKA 24: 50 – 53.

MADA: KRISTO AMEPAA KATIKA UTUKUFU WAKE.

SHABAHA: Wasikilizaji watambue kuwa Mungu hupenda kutuona na furaha hivyo wazidi kumwamini ili aachilie Baraka zake kwao.

UTANGULIZI
 Leo ni siku muhimu sana kwa kanisa na kwa ukombozi wa mwanadamu kwani tunakumbuka Yesu baada ya kumaliza safari ngumu ya kutukomboa sasa anarudi kwa baba yake ili kuanza maandalizi ya makao yetu ya milele.

 Somo ambalo tumelisoma leo kutoka katika injili ya Luka linaelezea tukio la Yesu kunyakuliwa mbele ya wanafunzi wake kwenda mbinguni ambapo katika somo hili tunajifunza mambo mengi na leo naomba tuangalie haya machache.

1. MPANGO WA MUNGU KWETU WAKATI WOTE NI KUTUBARIKI
 Wanafunzi wa Yesu wakiwa wameshuhudia matendo mengi aliyoyatenda Yesu kabla ya kuteswa na kuuwawa na hata baada ya kufufuka wameshuhudia Baraka nyingi na ulinzi katika maisha yao, na sasa Yesu anawaacha anaondoka kwenda mbinguni lakini hata katika kuondoka kwake anaendelea kuwabariki wanafunzi wake.

 Tunaona wazi kuwa mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu ni kumbariki wakati wote hata ikiwa ni wakati wa dhiki, mateso, mahangaiko na hata wakati wa furaha kwa sababu hiyo tunapaswa kuweka tumaini letu kwake pasipo kuyumba wala kuyumbishwa.

2. BARAKA ZA MUNGU ZITUPELEKEE SISI KUMWABUDU WAKATI WOTE
 Wakati Yesu anaendelea kuwabariki wanafunzi wake na wakielewa wazi kuwa wanapokea Baraka, Baraka zile ziliwapelekea wao kumwabudu.

 Je, ulishawahi kubarikiwa? Baraka za Mungu ziliposhuka katika maisha yako wewe umefanya nini? Wanafunzi wanatuonyesha mfano mzuri kuwa Baraka za Mungu zinatutaka sisi kumwabudu wakati wote.

 Wapo ambao wanabarikiwa lakini hawaonekani katika kumwabudu Mungu si katika nyumba za ibada wala katika sala zetu za jumuiya. Hiyo ni kusema kuwa Mungu sizihitaji Baraka zako. Mungu atusaidie ili na sisi tusikiri hivyo. Hongereni ninyi mliohudhuria ibada ya leo.

3. BARAKA ZA MUNGU HULETA FURAHA MAISHANI
 Wanafunzi walipobarikiwa japokuwa walikuwa na huzuni ya Yesu kuondoka katikati yao Baraka zile ziliwafanya waelekee Yerusalemu kwa furaha.

 Wakati mwingine maisha yanaweza kuwa na huzuni ila huzuni hiyo isikuondoe katika furaha yako katika Yesu Kristo. Kumbuka mambo mema na Baraka za Mungu katika maisha yako ili uweze kuitunza furaha yako.

4. TUONYESHE FURAHA YETU YA KUPOKEA BARAKA ZA MUNGU KWA KUMSIFU DAIMA
 Tunaambiwa kuwa wanafunzi wa Yesu walidumu wakimsifu Mungu ndani ya Hekalu wakati wote.

 Katika hili tunaona jambo hili la kumuabudu Mungu linajitokeza mara mbili kuonyesha umuhimu wake na sasa anasema hekaluni. Wapo ambao wanasema kuwa wanamsifu Mungu wakiwa nyumbani kwao, ama wanaangalia video au wanasikiliza redio, sisemi kuwa hilo ni baya ila kama unazo nguvu na afya usiache kuhudhuria ibada kumwabudu na kumsifu Mungu wetu.

HITIMISHO
Mungu aliye na mpango mwema wa kutubariki wakati wote ili tudumu katika furaha basi tusiache kumsifu na Kumuabudu katika maisha yetu yote.

AMEN
Ev.John

MAHUBIRI YA SIKU YA 5 BAADA YA PASAKA TAREHE 17/05/2020 IITWAYO ROGATE MAANA YAKE OMBENI.

KKKT DAYOSISI YA KUSINI, JIMBO LA NJOMBE MJINI, USHARIKA WA UWEMBA, MTAA WA LUSITU.

MAHUBIRI YA SIKU YA 5 BAADA YA PASAKA TAREHE 17/05/2020 IITWAYO ROGATE MAANA YAKE OMBENI.

MASOMO: ZABURI 107:1 – 8, MARKO 10:46 – 52, *MATENDO YA MITUME 12:5 – 17

MADA: OMBENI KATIKA JINA LA YESU KRISTO

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kutambua kuwa wakiomba kwa Jina la Yesu Hakika watapokea majibu yao hivyo waelekeze maombi yao kwake.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, Jumapili ya leo tunajifunza juu ya kuomba kwa kutumia Jina la Yesu Kristo ambalo ndio msaada wetu wakati wote( Wafilipi 2: 9 – 11)

Kwa kuutazama ukweli huu tumepewa kujifunza kutoka kitabu cha maendo ya Mitume 12: 5 – 17 ambapo tunapata habari za Petro kufungwa gerezani na Kanisa linakutana vikundi vikundi na kumuomba Mungu anayeleta msaada wa kweli kwa kanisa na kwa Petro mwenyewe.

Katika habari hii tunaweza kujifunza haya yafuatayo:-

1. KATIKATI YA NDORUBA UKIWA MIKONONI MWA MUNGU ANAKUPA AMANI
 Hapa tunaona jinsi ambavyo Petro akiwa amefungwa gerezani katikati ya ulinzi Mkubwa, amefungwa minyororo kwenye miguu na kikono tena kwenye chumba cha ndani na siku chache zilizopita rafiki yake na mtumishi mwenzake Yakobo ndugu yake Yohana aliuwawa lakini yeye anapata Usingizi tena tunaambiwa alilala fofofo.

Usingizi una mafundisho mengi na siku ya leo tujifunze moja juu ya Usingizi

 Wakati wa matatizo, shida na dhiki ni vigumu sana kupata Usingizi ( Esta 6:1,Ayu 3:13)

 Mungu anaporuhusu Usingizi kwa mtu wake anataka kuleta mwanzo mpya (Mwa 2:21, 28:16,)

 Katikati ya dhoruba Mungu humpa rafiki yake Usingizi akitaka atulie na kuwa na amani tayari kupokea Baraka. (Zab 3:5,127:2)

 Kwa maelezo hayo unaona jinsi ilivyokuwa vigumu Petro kupata Usingizi ila kwa ajili Petro alijua kuwa maono yay eye kulijenga kanisa hayajakamilika na aliahidiwa na Mungu kuwa atalala akiwa mzee.

 Maisha yetu yamejaa dhoruba nyingi, mateso mengi na mahangaiko ila bado Mungu anabaki kuwa Mungu kwetu, ukiangalia hasa katika kipindi hiki cha Ugonjwa huu waCOVID – 19 mahangaiko ni mengi kila mahali ila tusiache kuelekeza imani yetu kwa Mungu yeye atatupa amani na matulizo ya kweli a Ushindi wa kutosha

2. MUNGU ANAPOANZA KUTENDA HUTENDA ZAIDI YA ULIYOTAZAMIA NA KUKUACHA KWENYE MSHANGAO
 Mungu anapofanya ukombozi katika maisha yetu sio kwamba anatushangaza sisi wenyewe bali hata wale waliotuzunguka wanabaki kushangaa.

 Wakati Petro amelala Mungu ameruhusu kanisa kuomba kwa ajili ya Petro na Petro anapookolewa anashangaa na kanisa lililokuwa linamuombea nalo linashangaa wote Petro na Kanisa wanapoona ukuu wa Mungu wanafikiria ni ndoto kumbe ni Mungu yupo kazini.

 Yapo mambo ambayo tunaona kuwa hayawezekani kabisa ila tukiingia kwenye maombi yanawezekana kwa kiwango ambacho hata sisi wenyewe hatuwezi kuamini ila ukweli unabaki kuwa Mungu ni mwaminifu kwetu na hataacha kututendea mazuri wakati wote tunapoelekeza tumaini letu kwake.

*3. MAOMBI HUFANYA YOTE YAWEZEKANE*
 Shetani anapokupata anahakikisha kuwa anafunga kila njia ambayo anaona inaweza kukusaidia kunusurika katika mikono yake. Tunaona Jinsi ambavyo Petro alivyokamatwa na kufungwa chumba cha ndani na hiyo ikawa haitoshi wakamfunga kwa minyororo na hiyo ikiwa bado haitoshi wakamuwekea na walinzi ila Kanisa linapoomba hakuna kifungo kinachozua Petro kuwa huru tena uhuru ulioleta uhai kwa kanisa.

 Kanisa tusichoke kuomba katika nyakati zote hata pale kwa akili zetu za kibinadamu tunapoona mambo hayawezekani ila kwa Mungu yanawezekana sana. OMBA, OMBA OMBA NA USICHOKE KUOMBA HADI HAPO MUNGU ATAKAPOJIBU MAOMBI YOTE SABABU HAKIKA ATAYAJIBU.

HITIMISHO
Mungu aliyemtoa mwanae wa pekee tuendelee kumtegemea tukilitaja jina lake ambalo kwa hilo tunapokea majibu yetu.
AMEN.

10/05/2020 KANTANTE DOMINION-MWIMBIENI BWANA WIMBO MPYA

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 4 BAADA YA PASAKA TAREHE 10/05/2020

MADA: MWIMBIENI BWANA WIMBO MPYA

MASOMO: ZABURI 100: 1 – 6, UFUNUO 15: 1 – 4, *ZABURI 69: 29 – 36

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa aina ya maisha wanayoishi haiondoi uwezo wa Mungu katika kuwaokoa wazidi kumtegemea.

UTANGULIZI
 Bwana Yesu asifiwe, Leo ni jumapili ambayo kila mtu awe mwenyewe, au katika familia, au katika kundi kwa pamoja tunaalikwa kumuimbia Mungu wimbo mpya.

 Upya wa wimbo sio maneno mapya yaliyotungwa katika umahiri wa kisanii bali ni moyo unaomaanisha kile unachokitamka katika hali unayopitia kwa matumaini makubwa kuwa Mungu atafanya.

 Katika kutafakari mada hii tunatafakari neno la Mungu kutoka kitabu cha Zaburi 69: 29 – 36 ambapo tunamuona muimba zaburi akitambua hali ya uhitaji na umsikini alionao ila haimzuii kuamini kuwa Mungu atamponya yeye, na wote wanaomtegemea na sio wanaomtegemea tu hata taifa lake litaokolewa hivyo ataendelea kuimba nyimbo za furaha ya matumaini na kumshukuru Mungu kwa wokovu aliompatia yeye, ndugu, jamaa na marafiki zake na hata taifa lake.

Katika kisa hiki tunajifunza mambo makuu yafuatayo:-

1. MUNGU HUBAKI KUWA MUNGU BILA KUJALI CHOCHOTE UNACHOPITIA
 Wakati mwingine katika maisha hufikiri kuwa tunapopitia katika hali zinazosababisha maumivu, wasiwasi na uhitaji labda Mungu ametuacha na hata watu wengine hujitahidi kuficha hali wanayopitia ila ukweli unabaki kuwa Mungu habadilishwi na hali unayoipitia bado anabaki kuwa Mungu.

 Mwimbaji wa Zaburi analionyesha hilo kuwa japokuwa ni maskini mhitaji mwenye wasiwasi na maumivu makali ambayo hakustahili ila hayupo tayari kutafuta msaada kwa mtu au kitu kingine chochote zaidi ya kumtafuta Mungu sababu ana uhakika kuwa kitakachomuokoa na kumuinua tena ni WOKOVU WA MUNGU PEKE YAKE

 Moyo wenye shukrani juu ya wokovu huu utajidhihirisha kwenye kumsifu Mungu (Moyo wenye shukrani wakati wote una wimbo wa kumtukuza Mungu.)

 Huduma za kiroho kama vile kumsifu Mungu(Kuimba nyimbo mbalimbali), Kumuabudu Mungu, kumuomba Mungu vina umuhimu zaidi ya sadaka.

2. MAISHA YA SIFA YANAIMARISHA IMANI ZA WAAMINIFU WANAOPITA KATIKA KIPINDI CHA MATESO
 Maisha ya kumsifu Mungu sio kwamba yanakuimarisha wewe peke yako na kukupatia wokovu bali wote amabo wanatazama jinsi Mungu anavyokuokoa nao wataimarika imani zao.

 Mungu ataweka tofauti kati ya watu wanaomtegemea na wale wasiomtegemea kwani yeye ni Mungu:-

a) Anayeleta furaha kwa wote wanaoonewa,

b) Hufufua mioyo iliyokata tamaa na matumaini,

c) Husikiliza maombi ya wahitaji wote,

d) Huwafungua wafungwa wote.

 Katika kipindi hiki tunachopitia changamoto ya ugonjwa huu wa COVID 19 na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu tubadili namna ya kukabiliana nao sio kila siku kupokea habari mbaya tu. Sasa tuelewe kwamba ugonjwa upo na unaua tena kwa haraka hivyo tuchukue tahadhari na tuendelee kumsifu Mungu. Niliona wakati Raisi wetu anaposema tuombe nchi nyingi zilimbeza sana ila sasa nimeanza kuziona nazo zinafuata utaratibu huu wa maombi.

 Maombi yameondoa hofu kwa watanzania na sasa imeanza kuambukiza na nchi nyingine kuwasaidia watu wake kuondoa wasiwasi. Sisi tuongeze bidii kumuomba Mungu na kumsifu daima.

3. MUNGU MWENYE UWEZO WA KUOKOA MTU MMOJA ANAO UWEZO WA KUOKOA TAIFA.
 Kama watu mbalimbali wanamsifu na kumuabudu Mungu na wokovu unatokea katika maisha yao, basi uwezo huo pai unaweza kutenda kazi katika taifa. Tunapoona taifa linataka kuanguka au tayari limeshaanguka tukimuita Mungu wetu kwa kweli atatusikia na kuliokoa taifa letu.

 Muimba zaburi anaeleza kuwa Mungu ataliokoa taifa la Yuda na watu watakaa na kumiliki, wale wanaomtumaini Mungu watarithi na wote wanao mtumaini hakika watakaa katika miji iliyookolewa.

 Wale kweli ambao wataelekeza tumaini lao kwa Mungu katika hali zote ni kweli nchi itaokolewa na watu watabaki hai kwa ajili ya kuishi wakimsifu Mungu.

HITIMISHO
Mungu hawezi kugeuzwa na hali yoyote ya kibinadamu bali wote wanaomtumainia hakika wataokolewa wao pamoja na familia zao na nchi yao.

AMEN.

03/05/2020 JUBILATE – MPIGIENI BWANA KELELE ZA SHANGWE MADA: MAISHA MAPYA NDANI YA KRISTO YESU

KKKT DAYOSISI YA KUSINI,JIMBO LA NJOMBE, USHARIKA WA UWEMBA,
MTAA WA MJIMWEMA

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 3 BAADA YA PASAKA TAREHE 03/05/2020

JUBILATE – MPIGIENI BWANA KELELE ZA SHANGWE

MADA: MAISHA MAPYA NDANI YA KRISTO YESU

MASOMO: ZABURI 107: 25 – 32, MATHAYO 9:14 – 17, *ISAYA 25: 1 – 8

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa Ndani ya Yesu yanapatikana maisha ya ushindi hivyo wamtegemee daima.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, Jumapili ya leo tunajifunza juu ya maisha mapya ndani ya Kristo Yesu. Kwa tafsiri yangu juu ya mada hii ni kuwa yapo Maisha ndani ya Yesu ambayo kila mmoja hapa anayo na pia kuna maisha mapya ndani ya Yesu Kristo ambayo baadhi yetu tunayo maisha hayo.

Naweza kusema Maisha ndani ya Yesu Kristo ni maisha yale ya mazoea ambayo unatambua kuwa Yesu yupo, na umesikia akitenda mambo ya ajabu lakini hilo halikuzuii wewe kutenda kwa kiburi, dharau na majivuno.

Na Maisha mapya ndani ya Yesu Kristo ni maisha yenye mabadiliko, maisha yanayomtegemea Mungu na kuziona nguvu zake zikitenda kazi. Yaani ni maisha yenye mafanikio yanayotambua kuwa Mungu ameahidi kutufundisha ili tuweze kupata faida. (Isaya 48:17)

Katika kusindikiza mada tuliyopewa leo ya Maisha Mapya ndani ya Kristo Yesu tumepewa neno la Mungu kutoka Isaya 25: 1 -8 ambapo tunajifunza mambo kadhaa ambayo ni:-

1. LENGO LA MUNGU KURUHUSU ADHABU KATIKA MAISHA YETU NI ILI TUKUMBUKE UWEPO WAKE NA KUMUABUDU.
Kama nilivyoeleza kwenye utangulizi kuwa maisha ndani ya Mungu ni maisha ya mazoea, sasa Mungu anapotaka kuondoa haya mazoea anaruhusu adhabu kidogo ili tuweze kumkumbuka na tumsifu.

Isaya hapa anazungunza katika wimbo wake wa shukrani kuwa Mungu ameviharibu vitu ambavyo wanadamu walivijenga kwa kiburi chao na uwezo wao, maisha yamekuwa ni uchungu mtupu na miji ya kifahari imekuwa magofu hakuna wakaaji kabisa na kwa hilo mataifa watishao wataogopa lakini lengo lake lipo kwenye ule mstari wa tatu ambalo ni ili watu walio hodari katika hali hii wabaki wakimtukuza Mungu.

Kipindi hiki ambacho tunapitia hatari hii ugonjwa huu wa Corona ni kipindi ambacho tunaona kweli maisha yamekuwa machungu, miji mikubwa inabaki kuwa magofu watu wake wanakufa kweli na hata kwetu na mataifa makubwa yanayotisha yannaogopa sana sitaki kusema hili ni pigo kutoka kwa Mungu ili tumrudie ila nasema kwa kupitia hili watu wengi wamemrudia Mungu na wale walio hodari hata katika shida hii hawataacha kumtukuza Mungu.

2. MAISHA MAPYA NDANI YA YESU KRISTO NI MAISHA YA MABADILIKO
Maisha mapya ndani ya Kristo Yesu ni maisha ambayo yanashuhudia mabadiliko kila siku ni maisha ambayo mtu anashuhudia nguvu za Mungu na kuzikiri kweli kweli.

Neno la Mungu katika Isaya linaonyesha wazi kuwa ni maisha ambayo yanatoa nafuu kwa wote wanaoteswa ( ni ngome kwa maskini mhitaji katika dhiki yake, mahali pa kukimbilia wakati tufani) kuwanyamazisha watesi wote wanaojishughulisha na maisha ya watu wa Mungu.(Wale wanaoshangilia kwa kututesa sababu wanaona wameshinda hakika watashushwa)

3. MABADILIKO YA KWELI YANALETA FURAHA KWA MUNGU INAYOLETA MAFANIKIO KATIKA MAISHA YETU
Kama nilivyoeleza tangu awali kuwa maisha mapya ndani ya Kristo Yesu ni maisha yanyoleta mabadiliko na mabadiliko hayo yanapokuwa ya kweli yanaleta mafanikio katika maisha yetu.

Neno la Mungu katika Isaya linaeleza wazi kuwa Mungu atafanya sherehe na wote wanaomtegemea na katika sherehe hiyo Mungu atafanya mambo kadhaa ambayo ni:-

a) Atawaharibu maadui zetu wote

b) Atafuta machozi yote

c) Ataondoa huzuni tote

d) Ataiondoa aibu yote iliyotukabili

e) Ataondoa kifo hata Milele.

Kipindi hiki tumeitwa sana katika kutubu ili Mungu atuondolee ugonjwa huu wa Covid-19 na tukihimizana kurejea kitabu cha Mambo ya Nyakati wa pili 7:14. Ukweli unabaki kuwa toba inahitaji mabadiliko ya kwelikweli ili mabadiliko hayo yaweze kutuondolea adui yetu huyu, kutufuta machozi, kutuondolea huzuni na hata aibu ambayo inaonekana kwetu kwa sababu tumeruhusu ibada kuendelea.

Mabadiliko ya kweli ya rohoni na mwilini. Mwilini tukifuata ushauri wa wataalamu kukabiliana na adui huyu mkubwa kwa sasa Covid -19 kama vile kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa, kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, kutokuwa na safari zisizokuwa na sababu ya msingi nk
Rohoni tukiendelea kumuomba Mungu kwa nguvu zetu zote na uwezo aliotujalia, tukitubu na kumkataa shetani na kazi zake zote na mambo yake yote.

HITIMISHO
Tuendelee kumtegemea Mungu na kumtumikia kwa uaminifu na hakika upya wa maisha yetu ndani ya Yesu Kristo utaonekana kwa mafanikio.
AMEN.
@Evjohn
0768386606