Category Archives: Majira ya utatu (Ordinary Time)

IBADA YA TAREHE 06 AGOSTI 2023 SIKU YA BWANA YA 9 BAADA YA UTATU

Somo:TUENENDE KWA HEKIMA
ZABURI 119:161–168; MATHAYO 10:5–15, MITHALI 1:1–7*
WIMBO: TMW 294
MAFAFANUZI
1. UTANGULIZI: Mithali 1:1
Kitabu kinaitwa Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa misemo ya hekima kuhusu hali halisi ya maisha ya kila siku yenye busara na haki ikigusa mada mbali mbali. Kitabu kinatoa mafundisho yenye mafumbo ambayo yalikuwa ya kawaida katika Maisha yao ya wakati ule. Ni misemo mifupi mifupi ambayo ni rahisi hata kuikariri. Kama vile Mfalme Daudi alivyo chimbuko la Zaburi katika Israeli ndivyo Mfalme Sulemani alivyo chimbuko la hekima katika Israeli. Inatajwa kuwa Sulemani aliandika Mithali 3,000 na nyimbo 1,005 wakati wa maisha yake (1 Wafalme 4:32–34). Na wakaenda Mataifa yote kwa Sulemani ili waisikie hekima yake.

Kitabu hiki kinaitwa Mithali za Mfalme Sulemani wa Israeli, lakini ni hakika kwamba Sulemani hakuziandika zote. Nyingine zinatajwa kuwa ziliandikwa na Aguri bin Yake (Mithali 30:1–33) na Mfalme Lemueli (Mithali 31:1–9), na wengine wametajwa kuwa wenye hekima bila kutajwa majina yao (Mithali 22:17 na 24:23). Mkazo ni kufundisha hekima ya jinsi ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Sura nne za kwanza ni mkazo juu ya asili ya hekima na umuhimu wake na sura zinazofuata ni mkusanyiko wa mistari miwili miwili mifupi yenye mithali zenye nguvu zinazogusa mambo mbali mbali ya maisha kama ndoa, upendo, uvivu, bidii ya kazi, maonyo kuhusu ulevi na uasherati.

Mfalme Sulemani alifahamika kwa umaarufu na upekee wa hekima ya ajabu. Sulemani alipopewa nafasi na Mungu katika ndoto ya kuomba jambo lolote atakalo, aliomba hekima ya kuliongoza taifa la Israeli na Mungu alijibu ombi lake (1 Wafalme 3:3–13). Zipo habari katika kitabu cha Wafalme wa kwanza zinazoonyesha jinsi alivyotumia hekima aliyopewa na Mungu. Mfano maarufu ni wa kesi ya wanawake wawili makahaba ambao walimgombania mtoto aliye hai wakimkataa aliye kufa (1 Wafalme 3:16–28).

2. MITHALI 1:2-7 KUSUDI KUU LA KITABU
Mwanzoni kabisa mwa kitabu Sulemani anaelezea kusudi la kitabu cha Mithali. Ni kujenga maisha ya uadilifu yanayofaa kimwili na kiroho. Kumpatia msomaji hekima, busara na maarifa ya Kimungu. Yanatajwa makusudi makuu matatu:

(a) Ili kuwapa wajinga werevu (Mithali 1:4).
Kuwapa wajinga, au watu wa kawaida werevu au busara. Hao ni watu wasio wasomi, hawa ndio wenye kiu ya kupokea mafundisho. Kitabu hiki kinapaswa kuwafundisha hawa wasio na uzoefu ili kujua nini cha kufanya na wafanye namna gani katika maisha yao. Na kijana atapata utambuzi au ufahamu hata kwa mambo ambayo hakuyafahamu. Sifa moja wapo kubwa ya watu wa kawaida (simple people) au ambao wametajwa kuwa wajinga ni wepesi. Mithali 14:15 inasema: Mjinga huamini kila neno, bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. Huyu mtu ni mwepesi au hata inaweza kusemwa kuwa ni mjinga, anaweza kuwa na maoni lakini akakosa hoja za nguvu.

(b) Kuwapa vijana maarifa na tahadhari (Mithali 1:4)
Vijana na wale watu wepesi wapo kuelekea utu uzima au kwenye hekima. Kitakachowapa tahadhari na uchaguzi sahihi katika maisha haya ni kukubali kufundishwa hekima. Hata nyakati za sasa kuna mambo mengi yanahitaji kuchambua kwa hekima na kuishi maisha ya tahadhari. Nyenzo ya kuishi maisha ya tahadhari ni hekima.

(c) Kuwaongezea elimu wenye hekima na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia (Mithali 1:5-6) waweze kuishi maisha ya uadilifu.

Kumbe kitabu cha mithali hakipo kwa ajili ya wajinga na wale wasio na uzoefu tu bali hata kwa wale wenye hekima. Kwa kupitia mafundisho ya mithali hizi wenye hekima wataongezewa elimu zaidi na zaidi. Mwenye ufahamu atafikia mashauri yenye njia, yanayomwezesha kutatua matatizo magumu kama ilivyokuwa na mfalme Sulemani alipoletewa kesi ya wale wanawake wawili waliogombania mtoto. Kumbe hakuna mwisho katika kutafuta maarifa na hekima.
Anasema mithali zinampelekea mtu kujua hekima na adabu, kutambua maneno ya ufahamu na kufundishwa matendo ya busara katika haki na hukumu na adili. Katika kujua hekima ifahamike kwa kizazi chetu kinaitwa cha habari na upeanaji wake (information age) lakini sio wengi katika kizazi hiki wanaotafuta hekima. Kujua maneno ya ufahamu maana yake yameandikwa yanapaswa kusomwa au kuangaliwa. Mithali 3:21 anasema Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, shika hekima kamili na busara.
Kujua hekima: Kuna tofauti kati ya hekima (wisdom) na maarifa (knowledge). Mtu anaweza kuwa na maarifa au ufahamu lakini asiwe na hekima. Kwani maarifa (knowledge) ni mkusanyiko wa ukweli wa mambo (facts about things) lakini hekima (wisdom) ni matumizi sahihi ya vile ambavyo tunavifahamu katika maisha yetu. Maarifa au ufahamu (knowledge) yanaweza kutuelezea namna mfumo wa utawala wa fedha lakini hekima ndiyo itasimamia matumizi sahihi ya fedha, kwa mfano kusimamia makisio ni hekima zaidi kuliko utaalamu. Shida yetu leo watu wengi wamejikuta wanatafuta fedha na sio hekima. Wengi tunaweka nguvu katika kupata elimu na sio hekima. Swali linakuja, hekima inatafutwaje? Mithali 1:7 na Zaburi 111:10 zinaweka wazi kuwa kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima. Kumbe hekima na maarifa vyanzo vyake ni kumcha Bwana. Na ukienda kwa Ayubu 28 unaona maelezo marefu kabisa.
Kufundishwa matendo ya busara/hekima
Mithali zipo kama shule au chuo cha hekima. Lakini tuingie chuoni tukiwa na moyo pamoja na akili wazi kupokea mafunzo. Tukifanya hivi haki, hukumu na adili/usawa vitatokea katika maisha yetu.

Lakini msingi mkuu wa hekima na maarifa ni kumcha Bwana ambacho ndicho chanzo cha maarifa yote (Mithali 1:7; Zaburi 111:10). Kitabu cha mithali kimeweka mkazo wake katika mambo halisi ya maisha na sio nadharia. Lakini kinatupa ukweli kwamba msingi ni fundisho la kitheologia kuwa maarifa na hekima yanatokana na kumcha Mungu, kuwa na hofu ya Mungu. Hofu ya Mungu ni kumjua Mungu, kujitoa kwa Mungu, kujinyenyekesha kwa Mungu.

3. TUENENDE KWA HEKIMA
Wiki iliyopita tuliongozwa na kichwa kinachosema uchaguzi wa busara na leo tunazunguzia hekima. Mara nyingi tunajikuta tunatumia maneno haya mawili kwa wakati mmoja, hekima na busara. Nimeeleza kwa kirefu tofauti zake katika kitabu cha Mafafanuzi ya Mahubiri ya mwaka 2020 ukurasa wa 199 na ukurasa wa 205. Kwa haraka utaona kuwa hekima ni pana kuliko busara. Hekima inasimama kama usukani wa kuendesha busara.

Somo letu linatuhimiza kuenenda kwa hekima katika dunia ambayo imebadilika mno katika mfumo wake. Mahusiano katika ndoa yameingia changamoto kubwa mno. Migogoro katika ndoa ni mingi. Ukiangalia kwa undani utagundua kuwa kuna vitu vya msingi vinakosekana. Maarifa ya maisha ya ndoa na hekima za Kimungu zimekosekana. Na mahali fulani imeelezwa kuwa ndoa za watu walioenda shule ndio zinaongoza kuleta shida, kumbe maarifa na elimu vimeshindwa kuleta maelewano katika ndoa. Biblia imeshatuambia chanzo cha maarifa na hekima ni kumcha Bwana. Mungu asipopewa nafasi halisi katika maisha yetu hakuna usalama.

Hata wale wanaoonekana kama wacha Mungu, watu wa dini sana wamepata shida hiyo hiyo kwa sababu ya kukosekana kwa misingi ya kweli ya neno la Mungu. Akili zimeshindwa kufundishika. Neno linasema: Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama (Zaburi 32:8). Mfano wa ndoa ni mmoja tu. Zipo changamoto nyingi zaidi ya hizo ambazo zinahitaji hekima za Mungu.

Kuna hitaji hekima katika malezi ya watoto na mahusiano kati ya wazazi na watoto, katika kutunza mazingira yetu, katika kutafuta na kutumia fedha.

Mambo yote haya kwa kutumia maarifa yetu hatuwezi kuyamudu, maana adui yupo kazini wakati wote. Tunahitaji uongozi wa Mungu. Na uzuri wake ni kwamba, ndani yetu huishi Roho wa Mungu. Huyu ndiye hekima yetu na mwongozo wetu kwa kila jambo. Maana yake, ili kuenenda kwetu kuwe kwa hekima, lazima tuhakikishe tupo na yeye aliye asili ya hekima. Mungu atusaidie tumpe nafasi Roho wake maana ni katika yeye tutakuwa na hekima na hivyo tutaweza kuenenda kwa hekima. Amen.

IBADA YA TAREHE 30 JULAI 2023 SIKU YA BWANA YA 8 BAADA YA UTATU

Somo:WEMA WA MUNGU WATUVUTA TUPATE KUTUBU
ZABURI 27:5-10; 2 KOR. 7:7-12;HOSEA 14:1-3*
WIMBO: TMW 149
MAFAFANUZI

1. UTANGULIZI

Ujumbe wa kitabu cha Nabii Hosea uliwasilishwa kwa njia ya kuigizwa katika Maisha ya nabii mwenyewe. Kwa mtazamo wa utumishi na ufuasi haikuwa njia rahisi ya kuwasilisha ujumbe. Nabii Hosea aliagizwa na Mungu kuoa mwanamke kahaba na kuzaa naye watoto. Mungu alisema anafanya hivyo kwa sababu nchi imefanya uzinzi mwingi. Mwanamke aliyemwoa aliitwa Gomeri (Hosea 1:2-3). Hata baada ya kuolewa na Nabii Hosea, Gomeri aliendelea kwenda kufanya uzinzi na wanaume wengine na Hosea aliendelea kumrudisha na hata kumnunua kwa fedha ( Hosea 3:2).

Katika mlango wa tatu nabii anafafanua alichoagizwa na Mungu kufanya na sababu za kufanya hivyo. Aliagizwa ampende mwanamke apendwaye na Rafiki yake naye ni mzinzi, kama vile Mungu awapendavyo wana wa Israel ingawa wamegeukia miungu mingine (Hosea 3:1).

Ndani ya ujumbe wa Hosea kuna onyo kwamba kama Israeli hataacha uzinzi (kuabudu miungu mingine) ataadhibiwa vikali. Lakini kumbuka, adhabu huwa na lengo la kumrekebisha mkosaji. Hukumu ndio shida. Labda mhukumu awe na huruma. Sura zinazofuata Hosea 4-13 zinahusu Mungu na Israeli asiye mwaminifu. Ndani yake sura za 4 na 5 zinazungumzia uzinzi ambao Israeli anaufanya kwa kuabudu miungu mingine. Sura ya 6 Efraimu alirudi kuadhibiwa. Njooni tumrudie Mungu maana yeye amerarua na yeye atatuponya (Hosea 6:1); Sura za 7-12 Israeli (Efraimu) atapona hukumu kama atamrudia Mungu anayempenda. Efraim ni kabila ambako wafalme wengi walitoka. Sura ya 13 Israeli atahukumiwa sasa na sura ya 14 inaonyesha kuwa Israeli ataokolewa baadaye.

Ukijumlisha ujumbe wa Hosea unakuwa tabia yao ya kutokuwa waaminifu ndio sababu ya hukumu itakayokuja. Hii sura ya mwisho ni ya matumaini kwa taifa lililotubu. Hosea aliitwa kuhudumu katika taifa lililochanganyikiwa na limepoteza maadili na uchaji. Alipewa wajibu mkubwa mno wa kuoa kahaba na yeye kubaki mwaminifu katika ndoa yake kama Mungu alivyo hata kama mke wake alikwenda kwa wanaume wengine.

Fikiria tu njia hii ya kuwasilisha uasi ambao umefanywa na wana wa Israeli angepewa mchungaji mmojawapo leo. Kwanza, yeye mwenyewe angesema hiyo sio sauti ya Mungu na wale wanaoogonzwa naye wengi wangetia mashaka kama kweli ni Mungu ameruhusu hilo.

2. HOSEA 14:1-3

Sura hii ya mwisho ya kitabu cha Hosea inakuja na kitu cha pekee baada ya kutupitisha kwenye ujumbe wa hukumu. Anakuja na ujumbe wa rehema. Rehema ni msaada unaoambatana na huruma. Mungu mwenyewe anatoa maelekezo namna ya kufanya toba ili kumrudia Mungu. Anaelekeza ili kufikia toba nini cha kusema na nini cha kufanya. Ujasiri wa kutubu unajengwa na utayari wa Mungu kuwapokea wenye dhambi wanaporudi. Mungu anasema nitawaponya kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo kwa maana hasira yangu imemwacha (Hosea 14:4,8). Pia zipo faraja kubwa ambazo ameziandaa kwa ajili ya Israeli anayetubu (Hosea 14:5,7). Ujumbe unahitimishwa kwa swali kwamba ni nani aliye na hekima na atayafahamu mambo haya? Na nani mwenye busara atakaye yajua? Ni maswali yanayotuhusu sisi sote katika ukweli wa kuyapokea haya (Hosea 14:9).

Hosea 14:1 Israeli mwenye dhambi anaitwa kurudi (kutubu).

Kumbe kila mtu anahitaji ujumbe wa toba hata walio ndani ya agano kama Israeli. Kwa hiyo hata Wakristo ndani ya kanisa wanahitaji ujumbe wa toba kila siku. Israeli mrudie Mungu wako kwa maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako. Na kurudi ni kurejesha uhusiano (fellowship) uliopotea au uliovunjika. Ulipotea au kuvunjika namna gani? Ni pale walipoanguka au kujikwaa kwa sababu ya kuabudu miungu mingine na kumwacha Mungu aliye hai ambaye anawapenda. Ndio picha ya ndoa ya Hosea na Gomeri. Wanarudi kwa njia gani? Ni kwa kutubu na kutengeneza.

Hosea 14:2 Chukueni maneno pamoja nanyi

Wanaporudi wameelekezwa maneno ya kwenda nayo ambayo ni kumwambia Bwana: Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema. Na hivyo ndivyo mtakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe.
Wanapomrudia Bwana hawaendi kimya kimya na lazima waende kama Bwana anavyotaka na anavyoelekeza. Hataki wafikiri tu mioyoni na kujisikia hatia ya dhambi bali wakiri maneno hayo kwa midomo yao. Wamwambie Mungu kwamba tunakupenda na kwamba tumekukosea. Hata katika mahusiano yetu mfano ya mume na mke huwa ina nguvu kumwambia mwenzi kwamba unampenda, hata kwenye viapo vya ndoa wenzi huwa wanakiri kwa midomo yao kueleza upendo wao na kujitoa kwao katika ndoa. Katika viapo hivyo tunabeba maneno pamoja nasi. Mtume Paulo katika Warumi 10:8-10 anasema mtu kwa moyo huamini hata kupata haki na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

Je, tunachukua maneno gani pamoja nasi?

Hayo maneno sahihi ya kwenda nayo tunayapata kutoka kwa Mungu mwenyewe katika neno lake. Mfano Mdo 3:19 tunaambiwa tubuni basi mrejee, ili dhambi zenu zifutwe. Na Mathayo 3:2 Yohana alihubiri tubuni mwache dhambi zenu. Na Yesu alianza huduma yake kwa kuagiza toba, Mathayo 4:17 tubuni.. Upo umuhimu wa kukiri maasi yetu kwa midomo yetu. Zaburi 32:5 c; Nalisema nitayakiri maasi yangu kwa Bwana. Katika toba kuna umuhimu mkubwa wa mtu kukiri kosa alilofanya. Katika mifumo mingi ya kanisa wapo watu waliopewa wajibu wa kuwasikiliza wengine wanapotengeneza mambo yao na Mungu. Kuna wachungaji waliokula kiapo cha kufanya hivyo. Kuna watu wanafundisha kuwa inatosha kumwambia Mungu makosa yako, sawa lakini kuna mahali hali na hatia ya dhambi haiishi hadi mtu amekiri kwa midomo yake. Shida ni pale ambapo huduma imeingiliwa na watu ambao hawana dhamana ya kufanya hilo na kusimama kama mawakili wa siri za Mungu au wale wenye dhamana wanapokengeuka na kuharibu huduma. Lakini ukweli utabaki kuwa katika toba upo umuhimu wa kukiri kwa midomo yetu.

Tunamwambia nini Mungu katika toba yetu?

Ondoa maovu yote na utupokee kwa rehema zako. Hata katika sala ya Bwana Yesu alitufundisha kukiri makossa yetu mbele za Mungu ili atusamehe. Tunaporudi kwa Mungu lazima tunyenyekee mbele zake na kukubali kwamba tumekosa, tumefanya dhambi na tunahitaji msaada wake. Tunamhitaji yeye tu hatuna lolote la kufanya Zaidi ya kujiachia mikononi mwake.

Na ndivyo tutatoa sadaka ya midomo yetu kama sadaka ya ng’ombe. Maana yake maneno yetu ya toba na sifa mbele za Mungu ni sadaka ya kuteketezwa mbele za Mungu. Katika toba hiyo tutakiri wazi na kutengeneza mambo matatu:
(a) Kukataa kutegemea mataifa ya kigeni (Ashuru). Mungu pekee yake ndiye mwokozi wetu.
(b) Tutaacha kutegemea uwezo wa kivita kama kutegemea farasi (Zaburi 20:7).
(c) Tutakataa kutegemea sanamu, kazi za mikono yetu bali tutamtegemea Mungu pekee yake.
Wito wa nabii Hosea katika kifungu hiki (Hosea 14:1-3) ni kuwaita Israeli kurudi kwa Mungu kwa moyo wa dhati. Amewapa maneno ya kuomba wanaporejesha uhusiano wao na Mungu. Mwana mpotevu katika Luka 15:11-32 yeye alipanga maneno ya kusema anaporudi nyumbani kwa baba.
Kitabu cha Hosea kinahusu mambo ya dhambi na hukumu lakini pia upendo na huruma za Bwana kwa watu wasiostahili kama ambavyo Gomeri hakustahili kuwa mke wa nabii. Na Upendo huo wa Mungu umeonyeshwa kwa njia ya ndoa hiyo ya nabii Hosea na mwanamke Gomeri. Ni picha inayoumiza moyo kwa mtazamo wa kibinadamu, je, kwa Mungu mtakatifu sio zaidi?

3.WEMA WA MUNGU WATUVUTA TUPATE KUTUBU

Kutokana na mafunzo ya kitabu hiki utagundua kuwa kumbe Mungu anapomtendea mema huyu mwanadamu aliye mwovu sio kwamba anataka aendelee kutenda uovu bali anataka avutwe na upendo wa Mungu na hivyo aweze kugeuka na kujinyenyekesha kwa toba.
Mungu atujalie tutambue hilo na kutumia neema hiyo ya nguvu ya toba.
Amen.

IBADA YA TAREHE 23 JULAI 2023,SIKU YA BWANA YA 7 BAADA YA UTATU

Somo:UCHAGUZI WA BUSARA
ZABURI 37:1-8; LUKA 10:38-42
MATENDO 6:1-6*
WIMBO: TMW 422
MAFAFANUZI

1. UTANGULIZI
Hadi wakati huu wafuasi wa Yesu walikuwa wachache sana, lakini siku ya Pentekoste waliongezeka waumini elfu tatu (3,000). Kwa mujibu wa mwandishi wa Kitabu cha Matendo, Mungu aliongeza wanafunzi kila siku (Mdo 2:47). Mitume wakaweka nguvu zao katika kuhubiri, kufundisha, kuomba na kuombea wagonjwa (Mdo 3:1-26; 5:12-15), wakaongezeka wafuasi wengine elfu tano (Mdo 4:4). Kanisa la mwanzo lilikuwa vizuri sana katika kutunza takwimu hadi lilijua watu wangapi wameokoka, na lini.
Kanisa lilifanya mambo yote kuwa shirika. Likatunza wajane na wahitaji wengine (diakonia). Kwa vile mitume waliweka kipaumbele na mkazo wao katika kuhubiri na kuomba, suala la usimamizi wa mambo ya huduma (diakonia ). Walitambua kuwa kipaumbele ni neno na maombi lakini suala la diakonia bado lilionekana kuwa muhimu. Ndio maana kulipojitokeza manung’uniko kanisa lilichukua hatua haraka sana kwani lilijiona kuwa lilipaswa kufuata mfano wa Yesu wa kuwahudumia wahitaji, lakini pia lilifahamu kuwa hisia za ubaguzi ni hatari zinaweza kuligawa kanisa.
2.WATUMISHI SABA WAWEKWA KUJIBU MANUNG’UNIKO YA KUNDI LA WAYAHUDI WA KIYUNANI (MDO 6:1-7)
Kifungu kinachotangulia somo letu na kinachomalizia mlango wa tano (Mdo 5:42) kinasema: Na kila siku ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema ya Yesu kwamba ni Kristo. Na kutokana na kazi hiyo kanisa lilikua na kuongezeka kila siku. Na tatizo tunalokutana nalo katika somo letu linaashiria kwamba kasi ya ukuaji wa kanisa ilikuwa kubwa mno hadi wakashindwa kutawala mabadiliko hayo makubwa, wakashindwa kutoa huduma kwa watu kama inavyotakiwa. Kukatokea manung’uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwamba wajane wao kwamba walisahauliwa katika huduma ya kila siku (daily service au Kiyunani kathemerinos diakonia).
Inaonekana kanisa lilikuwa limeweka mpango wa kuwasaidia wajane kupata mlo wa kila siku. Lakini kukatokea manung’uniko toka Wakristo ambao ni Wayahudi wa Kiyunani kwamba walisahauliwa kwenye mgawo wa chakula. Kwamba ni kweli au ilikuwa hisia tu hatujui. Kitu ambacho kinafahamika ni kwamba waliitisha mkutano wa jamii ya waaminio na kuwashirikisha changamoto hiyo na kutoa mapendekezo namna ya kulitatua. Kwa kuwa walikuwa wameweka vyote shirika (Mdo 4:34) inaonekana shida haikuwa kukosekana kwa chakula bali utaratibu wa kugawa. Lilikuwa suala la utawala na usimamizi.
Wale 12 wakaitisha mkutano na kushirikisha watu lile tatizo na pia wakaelekeza nini kifanyike. Hapa tunaona uamuzi wa busara kusikiliza tatizo na kulichukulia hatua mara moja. Wakagundua kuwa tatizo lile ni la utawala, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani (Mdo 6:2). Mitume walijua nini walikabidhiwa na Bwana Yesu (Mathayo 28:19-20; Mdo 1:8) walipewa wajibu wa kuhubiri na kufundisha neno na sio kugawa chakula au kufanya mambo ya utawala wa chakula. Haina maana kwamba kazi hiyo sio muhimu bali waliangalia vipaumbele vya wito wao na wajibu wa msingi.
Baadaye tunajifunza kuwa Kanisa lilifanya kazi kufuata vipawa mbali mbali ambavyo Mungu amevigawa ndani yake (Rumi 12:12-26; 1Kor. 12:27-31 na Efeso 4:11-16). Ni vema na ni muhimu kuheshimu vipawa ambavyo Mungu ametupa na kuwa waaminifu kwa wito wetu. Ingekuwa kosa kwa Mitume kuacha kuhubiri wakaanza kusimamia chakula. Mitume walijitambua kuwa hawakuitwa ili wawe kila kitu katika kanisa.
Mitume wakaelekeza kuwa basi chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili (Mdo 6:3). Wakataja sifa za hao wasimamizi au wadiakonia. Walitakiwa kushuhudiwa na watu kuwa na sifa ya wema, vinginevyo wasingeweza kuhudumu kwa ufanisi. Walipaswa kujawa na Roho Mtakatifu. Kazi yo yote kanisani inahitaji watu wenye Roho Mtakatifu na hekima za Mungu. Ushauri huu unafanana na ushauri ambao Yethro aliutoa kwa Musa (Kutoka 18:18-22). Kwa hiyo sifa hizo tatu za kushuhudiwa wema, kujawa Roho na hekima zinawahusu Makatibu wakuu, Watunza Hazina, watu wa utawala, madereva, makarani, nk. Mitume walisema watu wenye sifa hizo ndio wakabidhiwe jukumu hilo.
Mitume wakaeleza ni nini wao watajishughulisha. Wakasema sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile neno (Mdo 6:4). Wanajibainisha kuwa kipaumbele kwao ilikuwa maombi na neno la Mungu. Kwa hiyo walitoa muda wa kutosha kwa ajili ya maombi na neno. Uchaguzi wa busara ni kujua vipaumbele na kuvitekeleza.
Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote (Mdo 6:5a). Hapa ni kwamba kanisa zima lilifurahi sio tu wale Wayahudi wa Kiyunani ambao walinung’unika. Wote walifurahi kupona kwa mwili wa Kristo ambao ulikuwa umejeruhiwa kwa sehemu mojawapo ya viungo kujeruhiwa. Hapakuwa na ushindani wowote hoja ilipokelewa na kutengenezewa suluhu ya pamoja.
Wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, Filipo na Prokoro,na Nikanoni, na Timoni, na Permena na Nikolao mwongofu wa Antiokia (Mdo 6:5b). Hapa inaonekana Mitume hawakutaja mtu, waliacha mkutano wenyewe uchague watu. Na kwa kuangalia majina yote saba yana asili ya Kiyunani kwa hiyo ni kusema kama Wadiakonia wote walitoka upande wa wale walioonekana wajane wao kupunjwa. Hili inaonekana walilifanya kwa upendo kabisa. Kati ya hao Stefano ameelezewa kipekee na baada ya hapo tumesikia habari za Stefano mfia dini ila hatujasikia habari za wale waliobaki. Na kwa vile hatujasikia tena manung’uniko inawezekana kazi yao ya kusimamia utaratibu wa chakula ilifanikiwa vizuri.
Wakawaweka mbele ya Mitume (Mdo 6:6a). Baada ya wale watu saba kuchaguliwa ni kama waliwekwa mbele ya mitume ambao kwa wakati ule waliokuwa ndio mamlaka ya juu katika kanisa. Waliwekwa kama ili wawathibitishe. Hawa Mitume kama viongozi wa juu katika kanisa bado walikuwa wanafikika kwa urahisi ndio maana walielezwa tatizo lililo wakabili. Ni busara kufikika ili matatizo yawasilishwe mapema.
Mitume wakawaombea na kuwaweka mikono yao juu yao (Mdo 6:6b). Waliwekewa mikono ili kutumwa kwa kazi maalum (Mdo 13:3; 2 Timotheo 1:6). Waliwekewa mikono kuthibitisha uchaguzi ule na kuwatuma kazini. Hata nyakati za sasa katika kanisa watumishi wanawekewa mikono na kufanyiwa maombi wanapoingizwa katika kazi mbali mbali.
Neno la Mungu likaenea na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu, jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile imani (Mdo 6:7). Kama Mitume walivyosema kwamba wao watadumu kuhudumu neno na katika maombi, matokeo yake kanisa likakua haraka sana pale Yerusalemu na makuhani ambao walikuwemo maeneo ya ibada ambapo Mitume walihubiri nao wakaamini na kutii imani. Kwa hiyo mahubiri na mafundisho ya mitume yaliwaongoa hata Makuhani.
3.UCHAGUZI WA BUSARA
Jambo kubwa katika somo letu limekuwa ni juu ya manung’uniko yaliyotokea katika kanisa la mwanzo. Kundi moja lilijisikia kubaguliwa. Kwa busara na kufikika kwa Mitume walifaulu kugundua kuwa hawapo salama kwa sababu kuna kundi linanung’unika. Leo kuna manung’uniko mengi katika jamii, katika familia, katika kanisa na katika nchi yetu. Inahitajika busara ya viongozi katika maeneo hayo kutopuuza na wachukue hatua ya haraka. Na mahali pengine manung’uniko yanatokea kutokana na hisia za kutotendewa haki au kubaguliwa. Ili kuondoa hisia wataalam wa sheria walisema, sio tu kwamba haki itendeke katika jamii bali ionekane kuwa inatendeka.
Katika kutafuta suluhu la tatizo lililolikabili kanisa la mwanzo tunakutana na uchaguzi wa busara ufuatao:
✓Kwanza, kusikiliza manung’uniko na kuyafanyia kazi hata kama hayana msingi ni jambo la busara.
✓Pili, katika kutatua tatizo mitume walishirikisha watu, huo ni uongozi shirikishi.
✓Tatu, Mitume walielekeza sifa za watu wa kuchaguliwa kuwa wawe wenye ushuhuda mzuri, waliojawa na Roho na wenye hekima.
✓Nne, Mitume waliacha watu wachague wenyewe na sio kuwashinikiza.
✓Tano, Mitume walifahamu vizuri mno wito wao na vipaumbele. Wakaweka nguvu zao katika maombi na neno. Kusimamia chakula na fedha sio kwamba hazikuwa kazi muhimu bali waliangalia vipaumbele na kugawana vipawa.
Katika mambo haya matano mara nyingi viongozi wengi nyakati zetu yamekuwa changamoto. Hawasikilizi manung’uniko hadi yanageuka kuwa migogoro, hata wakitaka kutatua wachache wanashirikisha watu na wanafanikiwa, wale wanaofanya bila kushirikisha watu hawafaulu. Jambo jingine la busara ni kuzingatia sifa za wale wanaopewa kufanya kazi ndani ya kanisa. Na suala la mwisho ni juu ya vipaumbele. Ni kiasi gani kazi zetu tunazifanya kufuata vipaumbele. Kwa mfano watumishi wengi wa madhabahuni tumepata shida kuweka katika uwiano shughuli za maendeleo na uchumi, fedha na mipango na suala la maombi na neno. Mungu atusaidie sana.
Amen.
Ev.john -0768386606