MAHUBIRI YA SIKU YA ALHAMISI YA KUKUMBUKA KUPAA KWA YESU KRISTO TAREHE 21/05/2020

KKKT DAYOSISI YA KUSINI, JIMBO LA KUSINI, NJOMBE MJINI,USHARIKA WA UWEMBA
MTAA WA MJIMWEMA luponde.

Masomo:
ZABURI 47:1 – 9,
EBRANIA 8:1 – 5,
*LUKA 24: 50 – 53.

MADA: KRISTO AMEPAA KATIKA UTUKUFU WAKE.

SHABAHA: Wasikilizaji watambue kuwa Mungu hupenda kutuona na furaha hivyo wazidi kumwamini ili aachilie Baraka zake kwao.

UTANGULIZI
 Leo ni siku muhimu sana kwa kanisa na kwa ukombozi wa mwanadamu kwani tunakumbuka Yesu baada ya kumaliza safari ngumu ya kutukomboa sasa anarudi kwa baba yake ili kuanza maandalizi ya makao yetu ya milele.

 Somo ambalo tumelisoma leo kutoka katika injili ya Luka linaelezea tukio la Yesu kunyakuliwa mbele ya wanafunzi wake kwenda mbinguni ambapo katika somo hili tunajifunza mambo mengi na leo naomba tuangalie haya machache.

1. MPANGO WA MUNGU KWETU WAKATI WOTE NI KUTUBARIKI
 Wanafunzi wa Yesu wakiwa wameshuhudia matendo mengi aliyoyatenda Yesu kabla ya kuteswa na kuuwawa na hata baada ya kufufuka wameshuhudia Baraka nyingi na ulinzi katika maisha yao, na sasa Yesu anawaacha anaondoka kwenda mbinguni lakini hata katika kuondoka kwake anaendelea kuwabariki wanafunzi wake.

 Tunaona wazi kuwa mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu ni kumbariki wakati wote hata ikiwa ni wakati wa dhiki, mateso, mahangaiko na hata wakati wa furaha kwa sababu hiyo tunapaswa kuweka tumaini letu kwake pasipo kuyumba wala kuyumbishwa.

2. BARAKA ZA MUNGU ZITUPELEKEE SISI KUMWABUDU WAKATI WOTE
 Wakati Yesu anaendelea kuwabariki wanafunzi wake na wakielewa wazi kuwa wanapokea Baraka, Baraka zile ziliwapelekea wao kumwabudu.

 Je, ulishawahi kubarikiwa? Baraka za Mungu ziliposhuka katika maisha yako wewe umefanya nini? Wanafunzi wanatuonyesha mfano mzuri kuwa Baraka za Mungu zinatutaka sisi kumwabudu wakati wote.

 Wapo ambao wanabarikiwa lakini hawaonekani katika kumwabudu Mungu si katika nyumba za ibada wala katika sala zetu za jumuiya. Hiyo ni kusema kuwa Mungu sizihitaji Baraka zako. Mungu atusaidie ili na sisi tusikiri hivyo. Hongereni ninyi mliohudhuria ibada ya leo.

3. BARAKA ZA MUNGU HULETA FURAHA MAISHANI
 Wanafunzi walipobarikiwa japokuwa walikuwa na huzuni ya Yesu kuondoka katikati yao Baraka zile ziliwafanya waelekee Yerusalemu kwa furaha.

 Wakati mwingine maisha yanaweza kuwa na huzuni ila huzuni hiyo isikuondoe katika furaha yako katika Yesu Kristo. Kumbuka mambo mema na Baraka za Mungu katika maisha yako ili uweze kuitunza furaha yako.

4. TUONYESHE FURAHA YETU YA KUPOKEA BARAKA ZA MUNGU KWA KUMSIFU DAIMA
 Tunaambiwa kuwa wanafunzi wa Yesu walidumu wakimsifu Mungu ndani ya Hekalu wakati wote.

 Katika hili tunaona jambo hili la kumuabudu Mungu linajitokeza mara mbili kuonyesha umuhimu wake na sasa anasema hekaluni. Wapo ambao wanasema kuwa wanamsifu Mungu wakiwa nyumbani kwao, ama wanaangalia video au wanasikiliza redio, sisemi kuwa hilo ni baya ila kama unazo nguvu na afya usiache kuhudhuria ibada kumwabudu na kumsifu Mungu wetu.

HITIMISHO
Mungu aliye na mpango mwema wa kutubariki wakati wote ili tudumu katika furaha basi tusiache kumsifu na Kumuabudu katika maisha yetu yote.

AMEN
Ev.John

One thought on “MAHUBIRI YA SIKU YA ALHAMISI YA KUKUMBUKA KUPAA KWA YESU KRISTO TAREHE 21/05/2020”

  1. nime barikiwa sana na andiko lako hili hakika umetufungua fahamu wengi juu ya baraka ambazo Mungu anaachilia kwetu kila wakati

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *