JUMAPILI YA 11 BAADA YA UTATU 23/08/2020

Somo:TUWE WANYENYEKEVU
fungu;LUKA 21:28-33

Bwana Yesu asifiwe…..

Unyenyekevu ni nini? Unyenyekevu ni hali ya moyo na akili inayomfanya mtu ajikubali alivyo na awakubali wengine walivyo. Kwa njia ya unyenyekevu mtu anatambua analopaswa kutenda na analitenda na pia asilopaswa kulitenda na halitendi. Kwa njia ya unyenyekevu, mtu anawapa wengine nafasi ya kuwa wanavyotakiwa kuwa katika haki. Kwa njia ya unyenyekevu, tunakomesha vilema vyetu vyote vya majivuno, kiburi, maringo, kujionaona na kujikweza.

Fadhila ya unyenyekevu inachukuliwa kuwa ya msingi na kiongozi wa fadhila nyingine zote. Martin luther anaendelea kusema kuwa “Kimsingi ni katika unyenyekevu mtu anafanywa kuwa mfuasi wa Kristo, na kwa hilo roho inaandaliwa kuungana na Mungu.” Mambo yote ni lazima yapate msingi wake katika unyenyekevu. Unyenyekevu unachukua nafasi ya kwanza kwa vile, unafukuza majivuno.

Fadhila ya unyenyekevu inatudai kujishusha ili tuinuliwe. Inatufanya tujione si kitu ili tuonekane kuwa ni kitu. Inatufanya tuwajali zaidi watu kuliko kujijali na kujipendelea sisi wenyewe. Inatufanya tuoneshe upendo wetu zaidi kuliko kutaka kupendwa. Inatufanya tuwaheshimu zaidi wenzetu kuliko kutaka kuheshimiwa.

Kwa njia ya unyenyekevu, tunaweza kufundishwa, kuelekezwa, kuongozwa, kuonywa, kulindwa, kutetewa na kukuzwa kwa ujumla. Ni fadhila ya msingi sana katika maisha ya mahusiano ya kila siku katika familia na katika jumuiya yoyote ile ya watu. Hata marafiki wa kawaida tu, au wachumba wakikosa unyenyekevu basi mahusiano yao daima hayatakosa malumbano, matusi, dharau, ukandamizaji na kila aina ya mateso.

Pengine watu wengi hushindwa kuishi na sisi kwa sababu tunakosa unyenyekevu, na ndio maana, hatuonyeki, haturekebishiki hatupendeki, hatuelekezeki, hatufundishiki, daima tunajiona kuwa ndio wenye haki sana mbele za watu na mbele za Mungu. Kukosa unyenyekevu kunatutenga na fadhila za Mungu. Tazama yule mfarisayo aliyekosa unyenyekevu akajiona kuwa yeye ndiye mwenye haki sana. [Lk 18:9-14]

Familia isiyojua unyenyekevu, ni uwanja wa vita daima. Vita za maneno na za mikono hazitakwisha. Tangu mwanzo wa malezi watoto wafundishwe juu ya umuhimu wa unyenyekevu. Unyenyekevu ni tendo la kijasiri kwa sababu linakudai kujishusha, kukomesha maringo, kiburi, kujikweza na majivuno. Walio wanyenyekevu daima hupata kibali machoni pa Mungu. Neno linasema “…Mungu huwapinga wajikwezao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Yak 4:6).

Wazazi katika familia, wakinyenyekeana wao kwa wao hapo wanakuza zaidi upendo wao. Kiburi, maringo, dharau na majivuno, hufukuza upendo. Lakini unyenyekevu hukuza na kudumisha upendo. Inapotokea kwa sababu zozote wazazi wanaoneshana umwamba, hakuna anayetaka kujishusha hata pale linapotokea kosa au kwazo la wazi, hapo upendo na furaha ya maisha ya ndoa huingia katika dosari kubwa.

Ndoa nyingi zimeingia katika migogoro ya kudumu sio kwa sababu ya matatizo makubwa, hasha! Pengine ni makosa madogomadogo ya kawaida kabisa ya kibinadamu. Lakini kwa vile hakuna ile hali ya unyenyekevu, kuwa tayari kujishusha, kila mtu anataka kujionesha yeye ni zaidi, na yupo sahihi zaidi ya mwenzake; hapo ndipo mgogoro hukuzwa zaidi.

Hapa rai ya moja kwa moja tunaipeleka kwa wanandoa! Wanandoa tukitaka amani, utulivu na maelewano ndani ya ndoa zetu, tuwe wanyenyekevu. Tukomeshe vilema vya kiburi, dharau, kujiona na maringo. Unyenyekevu ni daraja ya kufikiana na kuafikiana. Ukiwa mnyenyekevu, hata pale unapopatwa na tatizo, mwenzi wako ni rahisi kukuelewa, kukupokea na kukuinua. Lakini ukikosa unyenyekevu, utamfanya mwenzio ashangilie ukipatwa na mabaya.

Unyenyekevu, ni kiti cha kutuweka katika mazungumzo yenye mwafaka daima. Bila unyenyekevu, kila neno utakalotamka litakuwa na virusi vya fujo. Wazazi tukiwa wanyenyekevu, watoto wetu wataiga mwenendo wetu wa unyenyekevu nao pia tutawafundisha unyenyekevu. Sisi wazazi ndio waalimu wa maadili katika Kanisa la nyumbani, basi, na tujitahidi kuwa wanyenyekevu.

Na mtume Paulo anaelekeza kuuambata unyenyekevu, kwani ndiyo njia ya kujenga usitawi. Anasema “msifanye chochote kwa moyo wa fitina au majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu ninyi kwa ninyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu, bali faida ya mwenzake” (Fil. 2:3-4).
MWISHO
Bwana, anatualika sisi sote tuwe wanyenyekevu akisema ”jifunzeni kutoka kwangu kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu”. (Mt. 11:29). Na pengine anatuasa akisema “Anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejushusha atakwezwa (Mt 23:12). Unyenyekevu ni ngazi ya kupanda juu, zaidi na zaidi.
“Mtiini Mungu mpingeni shetani naye ata wakimbia”
AMEN.
imeandaliwa na
mwinjilist John
#0768386606

One thought on “JUMAPILI YA 11 BAADA YA UTATU 23/08/2020”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *