MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 26/07/2020

SOMO: Mwanzo 41:41-45

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, leo tunaangalia juu ya “NEEMA YA MUNGU YATUWEZESHA” yote tunayofanikiwa kuyafanya hapa duniani pamoja na magumu yote tunayopitia neema ya Mungu peke yake ndio inayotuwezesha kuonekana tulivyo, hatuwezi kujivunia akili zetu wala nguvu zetu wenyewe ila wakati wote yote tuyafanyayo tujue kuwa ni Mungu ametuwezesha.
Waandishi na mafarisayo wao walikuwa ni watu wa kushika sheria sana na kujitahidi kwa nguvu zao kuonyesha kuwa wanafahamu juu ya usafi na uchafu wa mtu ila Yesu anapotokea kwao anataka kuwabadiisha namna ya kufiki na kutambua mapenzi ya Mungu na kuondokana na mapokeo ya wazee.
Kwa somo hili tunajifunza haya yafuatayo

1. ASILI YA KWELI YA UNAJISI.
• Wayahudi walikuwa na sheria mbalimbali juu ya vyakula wakionyesha vingine ni safi na vingine ni najisi na hata jinsi ya kujiandaa kula. Walipoona wanafunzi wa Yesu wanakula bila kunawa mikono waliwahesabu kuwa ni najisi.
• Yesu anawataka watu wake kuelewa kuwa unajisi wa kweli hauwezi kuasilishwa na nguvu za nje bali kwa nguvu za ndani.
• Kile unachokipokea na kukiingiza katika mwili wako ndio kinachosababisha nguvu ya kutoa kile kilichopo ndani yako hivyo tunapaswa kuwa makini zaidi.

2. UTAMADUNI/MAZOEA YANAWEZA KUKUFANYA USIMUELEWE YESU
• Wanafunziwakiwa ni miongoni mwa wayahudi kwa kusikia mafundisho ya Yesu juu ya UNAJISI kutokana na maelekezo na torati walizoishi nazo kwa muda mrefu (Walawi 11: 1 – 47, Mt 5:17 – 18) hawakuelewa fundisho la Yesu walifikiri kuwa amekosea na kutaka mafafanuzi zaidi.
• Yesu aliwashangaa kwa kuzingatia walichokizoea zaidi kuliko kuisikiliza sauti yake na kuelewa ukweli wa neno la Mungu kama ilivyo kwetu sasa watu wengi kutokana na mazoea ya maishahawasikilizi Mungu anawata kufanya nini.

3. MATOKEO MAZURI AU MABAYA YA MAISHA YA MTU YANATOKA MOYONI
• Moyo wa mwanadamu ndio unaoleta matokeo ya aina zote ya mwanadamu, yawe mazuri au mabaya. (mithali 4:23)
• Moyo ukiathiriwa na dhambi ndiko ambapo mabaya yote hutokea (Mhubiri 9:3, Yer 17:9) na huwa mwanzo wa maovu yote (Mk 7: 20 – 23)

HITIMISHO
Wote tunapaswa kuelekeza macho yetu na umakini wetu wote katika mioyo yetu na kuilinda isiingiliwe na dhambi na kusababisha sisi kuwa waasi mbele za Mungu. ( Efeso 4:17 – 24, 1Petro 4: 1-3,) Haya yote yanawezekana ikiwa tutakuwa watii kwa neno la Mungu wakati wote na kujifunza kwa Mungu ( Mdo 2:28, 22: 16)
Kwa akili zetu ni Ngumu ila neema ya Mungu iliyokuu sana Kwetu inatuwezesha kufanya yote.
AMEN

MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO 19/07/2020

Somo:HURUMA YA MUNGU

MASOMO
zaburi1:1-69
2Wakoritho7:5-10
Mathayo9:1-8*
UTANGULIZI
▶Jumapili ya leo tunajifunza juu ya huruma ya Mungu kwa wanadamu
▶Katika tafakari hii ya huruma za Mungu tumepewa kutoka injili ya mathayo9:1-8, ambapo tunamwona Yesu akiwa anaponya na kupoza wagonjwa ambapo kila alieponywa aliambiwa “umesamehewa dhambi zako” chukua godoro lako na uende zako
▶Kitendo hicho cha kusema “umesamehewa dhambi” zako kiliwaudhi mafarisayo wakaanza kusemezana wao kwa wao huyu ninani hata asamehe dhambi lakini wasitambue nini wana kisema.
▶Mafarisayo waliendelea kusemezana wao kwawao nanafsi zao kwamba Yesu anakufuru(anaasi) kusema kwa mgonjwa amesamehewa dhambi hii ili kuwa nikutotambua mamlaka ya Yesu duniani ama Kristu ninani.
▶Kupitia kisa hiki cha Mathayo9:1-8Tunajifunza mambo yafuatayo juu ya huruma ya Mungu

1.MATESO NA MASUMBUFU TUNAYOPITIA WAKRISTO NI KUTOKANA NA DHAMBI
▶Ndugu zanguni Wakristo Mungu anasema amejaa huruma na neema nyingi lakini utashangaa wakristo wengi wanapita katika magumu nikutokana na dhambi. Ukitaka kuishi maisha ya raha tunza Utakatifu wako.
▶ Kuna wakati unajikuta unapita kwenye majaribu mazito sana kumbe nikutokana na dhambi kumbe dawa ya kuishi maisha ya raha ni kukimbilia huruma za kristo Yesu
▶Tunamwona mwanamke aliopooza aliambiwa umesamehewa dhambi zake .

2.MAGONJWA MENGI HULETWA NA DHAMBI
▶Ukiangalia dunia ya sasa inakabiriwa na magonjwa mazito mfano ukimwi kama tutamua kufuata kanuni nasheria ambazo Mungu ameagiza hakika hatutoweza kupigwa na magonjwa ya ajabu
▶lakini kwa huruma yake anasema “atatuponya magonjwa yetu yote na ataukomboa uhai wetu na kaburi” kumbe hata kama tumemtenda dhambi Tuombe toba ili huruma yake iendelee kutembea nasi.

3.TUNATAKIWA KUTAFAKARI MASHAURI YETU MBELE ZA MUNGU
▶Wakati Yesu anaponya wagonjwa mafarisayo walianza kusema inakuaje anasamehe dhambi hili lili kuwa nishauri ambilo kwao waliona ni kufuru.
▶Wakristo wa leo ili kuikimbikia huruma ya Bwana tunatakiwa kulifuata shauri la Bwana tutakuwa salama maana ndimo huruma ya kristo hutembea kuwahudumia walio wake.(Zaburi1:1-6)

4.MUNGU PEKEE NDIO MFARIJI WA KWELI
▶Ndugu zangu washarika tunatakiwa tutambue kuwa Yesu kristo ndio mfariji pekee ama chaguo la kwanza la kukimbilia wengine huenda kutafuta faraja kwa wagaga,marafiki,na watu wengine lakini faraja yao ni ya mda tu kimbia sasa mbio mbele za kristo akufute machozi.2Wakoritho7:5-10
▶Nandiomaana anasema njooni kwangu msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzusha.

MWISHO
▶Siku ya leo tunaitwa na huruma hii katika Isaya 1:18 ya kwamba twende tukasemezane naye iliatubadirishe na kututengeneza haijalishi mwanzo wetu ulikuwaje
KUMBUKA:Mabadiriko huanzia ndani ya Moyo wako
▶Mungu anisaidie na akusaidie ili tuweze kutambua huruma yake maishani mwetu.
AMEN.

MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO 12/07/2020

SOMO: UFUASI NA UANAFUNZI

Yohana 6:66-71
Yeremia 1:17-19

UTANGULIZI
 Jumapili ya leo tunajifunza juu ya Ufuasi na Uanafaunzi
 UFUASI ni hali ya kufuata itikadi, mwenendo au kitu Fulani
 UANAFUNZI ni hali ya kuwa katika mafunzo
 Kwa maelezo haya mtu huwezi kuwa mwanafunzi kabla kuwa mfuasi, sababu lazima uwe na itikadi ambayo unataka kujifunza ili uweze kuwa mwanafunzi
 Mkristo ni mtu aliyekubali kumfuata Yesu Kristo na Yesu anamfanya kuwa mwanafunzi wake ili aweze kujifunza kwake(Yesu) ( Luka 9:62)
 Somo ambalo tunatafakari leo juu ya mada hii ni kutoka Yeremia 1:17 – 19
 Nabii Yeremia ni mfuasi na mwanafunzi wa Yesu ambapo katika mistari hii Mungu Mungu anamwambia Yeremia pamoja na sisi jinsi ya kuwa mfuasi na mwanafunzi mzuri kwake.

1. UFUASI NA UANAFUNZI UNAHITAJI UTII NA UAMINIFU
 Mtumishi mwaminifu wa Mungu anakuwa mtii kwa yote anayoelezwa na Mungu. Mtumishi asiyemwaminifu Mungu anasema mtu wa namna hiyoa ataadhibiwa sana
 Mungu anatutaka tuifanye kazi yake kama alivyotupa wito tulipokubali kuwa wafuasi na wanafunzi wake.

2. UFUASI NA UANAFUZNI UNAHITAJI UVUMILIVU NA USTAHIMILIVU
 Mkristo anao uwezo wa kukabiliana na changamoto zote anazokabiliana nazo kwa kulifahamu neno la Mungu (Mt 4: 1 – 11)
 Wanaokuchukia wasikuyumbishe wala kukurudisha nyuma katika ufuasu na uanafunzi wako kwa sababu ni wale ambao wanapinga kweli ya neno la Mungu ( Yn 15:18 – 25)
 Pamoja na upinzani wote mfuasi na mwanafunzi wa Yesu anapaswa kusimamia neno la Mungu katika uaminifu na utakatifu wake huku akilisema neno la Mungu bila upendeleo wowote.

3. UFUASI NA UANAFUZNI UNAHITAJI KUTOKUYUMBISHWA.
 Majaribu na vikwazo ni sehemu ya utumishi wetu, hivyo tusiogope maana Mungu yu pamoja nasi ( Yer 37:16, Yer 38:6)
 Mtumishi anayemtii Mungu lazima atashinda pamoja na changamoto zote atakazokutana nazo ( Rum 8:35 – 39)

HITIMISHO
 Mungu alikuja kwa watu wake na wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wake na hao ndio wale waliaminio jina lake.
 Mungu atusaidie ili tuwe wafuasi na wanafunzi waaminifu kwa Mungu wetu na tufanyike watoto wake.
AMEN.

MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 05/07/2020 SIKU KUU YA VIJANA

MASOMO
Zaburi 37:25-40
1samwel 17:38-45
Mathayo 11:25

Wazo la wiki:NGUVU YA VIJANA KATIKA KANISA
____________________________

Somo:MAISHA YA USHINDI YA KIJANA MKRISTO

Fungu:1 YOHANA 2: 12 – 17

UTANGULIZI
• Jumapili ya Leo Tunajifunza maisha ya ushindi ya kijana Mkristo. Yohana ambaye alianza huduma ya uanafunzi wa Yesu akiwa na umri mdogo tu wa miaka 16 na sasa amekuwa mzee na anawaandikia wakristo wote akiwapa ushauri jinsi ya kuendenda kwenye ulimwengu huu huku wakihakikisha kuwa wanaupata ufalme wa Mungu.

• Katika mistari hii tuliyoisoma katika waraka huu Yohana anawagawanya wasomaji wake katika makundi matatu

TOBA NI MWANZO WA ULINZI WA MUNGU KATIKA MAISHA YETU.
• Kundi la kwanza ni watoto ambao wao ndio wameupokea ukristo anawaambia kuwa safari yao ya Ukristo inaanza na msamaha wa dhambi na anawahakikishia kuwa uhusiano wao na Mungu umerudishwa kama uhusiano wa baba na mtoto.

• Kundi la pili na la kina baba, hawa ni wakristo wa muda mrefu anawaonyesha uhuhimu wa kuwa na kumbukumbu katika maisha yao na kujua kuwa hata kama wana uzoefu wa Kiroho namna gani huwezi kumshinda Mungu bado unapaswa kuendelea kumtegemea wakati wote.

• Kundi la tatu ni vijana, anazungumza na kundi hili akilionyesha kuwa lina nguvu, limekuwa na uwezo wa kumshinda shetani na neno la Mungu linakaa kwa wingi ndani yao.

• Sifa hizi ni sifa za kundi hili la vijana, kuwa wana nguvu, neno la Mungu linakaa ndani yao na limewawezesha kumshinda yule mwovu.

• Analiambia kundi hili kuwa mapambano yapo katika maisha yao ila uwezekano wa kushinda upo sababu wapo kwenye nafasi nzuri ya kushinda.

• Neno la Mungu lililopo kwa wingi ndani yao ni chanzo chema cha hekima ya kujua jinsi ya kumpinga yule mwovu. ( Lk 4:1 – 13, Mt 4:1 – 11)

• Makundi yote haya matatu Yohana anayataka, kwanza, yanapaswa kupendana na pili yanapaswa kuchukia mambo ya giza ambayo anayaita mambo ya dunia na anatutaka tujitenge mbali na dunia kwa sababu hatuwezi kupenda dunia na Mungu ( 1Yoh 2:15, Mt 6:24)

a. Ni Dunia gani anayoizungumzia Yohana?
b. Dunia hii ni ya aina gani?
c. Dunia hii ina sifa hani?
d. Je, tunaweza vipi kuishinda dunia hii?

NI DUNIA GANI ANAYOIZUNGUMZIA YOHANA?
• Yohana hazungumzii dunia hii iliyoumbwa na Mungu ( Mdo 17:24) wala kuhusu dunia ya utu wa mtu ( Yn 3:16)

• Dunia anayoitaja Yohana inatokana na neno Kosmos lenye maana ya utaratibu au mpango wa mfumo wa utaratibu wa mwanadamu

• Dunia hii ni mfumo wa mawazo na matendo yanayomhusu mtu katika jambo Fulani. MF. Juma yupo kwenye dunia ya siasa, maana yake Juma anajishughulisha na siasa zaidi.

• Dunia hii ni maisha na mpango wa mwanadamu vinavyotengenezwa bila kumkali Mungu na mapenzi yake na katika hali hiyo ni chini ya shetani

DUNIA HII NI YA AINA GANI?
• Dunia hii na tamaa zake zitapita sio za milele na yule anayeitegemea pia hatadumu (1Yoh 2:17) na hata kama mtu huyo anaonyesha kushinda sasa ila mwisho wake utafika ( Uf 20:7 – 10, uf 21:1- 4)

• Dunia hii inamshambulia mwanadamu katika ukamilifu wake ( 1Thes 5:23) Kiroho, kimwili na kisaikolojia. Anatushambulia kiroho ili tusimpende Mungu, kimwili ili tusiweze kuishi kwa ajili ya Mungu na kisaikolojia ili tushindwe kujifunza kwa Mungu. Mfano wakati wa anguko. ( Mwa 3)

a. Hawa aliona mti unapendeza macho na kumuondoa katika kumpenda Mungu(mashambulizi ya rohoni)
b. Mti Watamanika kwa Maarifa, hapo shetani anamuondoa Hawa katika kujifunza kwa Mungu( mashambulizi ya kisaikolojia)
c. Wafaa kwa chakula anamuondoa Hawa katika maisha ya kuishi kwa ajili ya Mungu na kumtegemea yeye (mashambulizi ya Kimwili)

DUNIA HII INA SIFA GANI?
Biblia inatueleza wazi sifa za Dunia hii
a) Dunia ya namna hii ina kiongozi wake ambaye ni shetani ( 2Kor 4:14, Yn 12:31)
b) Ni dunia ya uovu ( 1Yoh 5:19)
c) Dunia hii ina watoto wake ( Lk 16:8)
d) Dunia hii ina hekima yake yenyewe ( 1Kor 2:6)
e) Dunia hii ni chafu ( 2Pet 1:4)
f) Dunia hii ndio iliyomsulubisha Yesu ( 1Kor 2:8)

TUNAWEZAJE KUSHINDA DUNIA HII?
Ili kuwaeza kuishida dunia hii lazima upambane nayo kimwili, Kiroho na kisaikolojia (nafsi)
a) Njia ya kushinda ulimwengu huu kimwili ni kujitenga na dhambi(1Thes 5:22) Ruhusu hamu yako ya kuishi kwa ajili ya Mungu iongoze njia na kazi zako
b) Ili uweze kuishinda dunia hii kisaikolojia ( 1 Yoh 5:4b) Ruhusu hamu ya kujifunza kwa Mungu ikuze ufahamu wako na uelewa wako
c) Ili uweze kupambana Kiroho ni kujisalimisha kwa Mungu ( Yak 4:7) Ruhusu hamu ya kumpenda Mungu iongoze maamuzi yako.

HITIMISHO
• Tunapaswa kujua kuwa ulimwengu unapita ila Mungu atadumu nasi milele ( 1 Tim 6: 11 – 12)

MAHUBIRI YA JUMAPILI TAREHE 28/06/2020

Somo:NEEMA YA MUNGU ITUOKOAYO
Masomo:
Zaburi 59:1-9
Matendo 11:1-15
*Luka 8:26-39

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa ili kupata ahadi za Mungu tunapaswa kumtegemea Mungu.

“Kwa kuwa mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea” (Lk 19:10)

UTANGULIZI: Leo ikiwa ni siku ya tatu baada ya utatu tunaangalia mada izungumzayo juu ya Neema ya Mungu ambayo inatuwezesha sisi kuupata wokovu.

> Neema maana yake ni mafanikio aliyonayo mtu kutokana na majaaliwa ya mwenyezi Mungu au kwa juhudi zake mwenyewe.

> Hivyo:- tunaweza kusema kuwa leo tunazungumzia juu ya mafanikio aliyonayo mtu kutoka kwa mwenyezi Mungu ambayo yanaleta wokovu katika maisha ya mtu.

> Katika kutafakari Neema hii ya Mungu iletayo wokovu tumepewa kisa kutoka katika biblia Luka 8:26 – 39. Kisa hiki ambacho kimeelezwa hapa pia kimeelezwa katika kitabu cha mathayo 8:28-34 na kitabu cha Marko 5:1-20 ikizungumza habari ya mtu aliyepagawa na pepo wachafu ambao wamejitambulisha kwa jina la Legion maana yake ni jeshi kubwa la warumi lenye nguvu lililokwa na idadi ya wanajeshi 6000.

Katika kisa hiki unajifunza mambo yafuatayo:-

SHETANI NI MHARIBIFU

Mtu huyu ambaye amepagawa nna pepo tunaambiwa kuwa alikuwa Uchi, aliishi makaburini, na alikuwa akijikatakata na mawe (Marko 5:3) Shetani anapoingia kwetu hahurumii hata miilil yetu atatutaabisha na kuwa wahitaji wakati wote.

ULINZI WA KIBINADAMU HAUJITOSHELEZI

Mtu huyu alifungwa kwa pingu na hata kwa minyororo ila aliikata yote na wanadamu wakakata tama nay eye na kumuacha alivyo. Unaweza kutegemea wanadamu wanaweza kukusaidia ila ni kwa kitambo kidogo na utabaki katika shida yako.

BINADAMU WENGI WANAANGALIA KITU KULIKO UTU

Tunaelezwa kuwa baada ya mtu huyu kuponywa watu wa mji ule walimfukuza Yesu kwa sababu walipiga hesabu ya hasara ya nguruwe 2000 waliofia majini waliona mwenzao amepata hasara kubwa sasa hawakujua nani angefuata wakaogopasana wakaamua kumwambia aondoke kwao.

MUNGU ANAJISHUGHULISHA NA MAHITAJI YETU

Yesu alivyoona kuwa mtu huyu yupo uchi, anaishi makaburini mbali na watu na alikuwa akijikata mwili kwa mawe alijua kuwa anahitaji msaada hivyo aliona nguruwe hawana umuhimu kama mtu wake akayaelekeza mapepo kwa nguruwe na kumponya yule kijana. Mapepo yalikwepa kwenda kuzimu yakidani kuwa yakiingia kwa nguruwe yatakuwa salama ila baada ya kuingia nguruwe walikufa wote na mapepo bado yakaenda kuzimu.

UKIMKUBALI MUNGU UTAKUWA SALAMA

Baada ya mtu huyu kuponywa alitulia chini ya miguu ya Mungu akiwa amevaa nguo na akiwa na akili yake timamu. Amani ya kweli inapatikana kwa kumkubali Yesu

MEMA ANAYOKUTENDEA MUNGU ANATAKA UMTUMIKIE

Mtu aliyeponywa alitaka kandamana na Yesu ila yesu alimwambia aende kuelezea habari njema za Yesu kwa watu wa nyumbani kwake kwa kuwa eneo lile liikuwa ni eneoo la wapagani nao waone wema wake. Baraka tunazopata tunatumwa tukahubiri.

HITIMISHO

Bora kuwa mlinzi wa getini kwa Mungu kuliko kuwa mfalme au malkia nje ya Mungu sababu huko hakuna mafanikio ya kweli, mafanikio ya kweli yaletayo wokovu yanapatikana kwa Mungu tu.

MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 21/06/2020

siku ya 2 baada ya utatu

SOMO: TUKAE PAMOJA KWA UMOJA
MASOMO Yohana17:20-21
?Efeso 5:8-14
? Zaburi 133

UTANGULIZI
• Jumapili ya Leo ni sikukuu kubwa ya KKKT, tuanze mafundisho yetu ya leo kwa kumtakia ndugu yako heri ya siku kuu.
• Leo ni jumapili ambayo tunaazimisha kuunganika kwa makanisa saba ya Kilutheri Tanganyika ambayo ni:-
a) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Iraqw
b) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la kaskazini mwa Tanganyika
c) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kaskazini Magharibi mwa Tanganyika
d) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Kati mwa Tanganyika
e) Kanisa la kiinjili la Kilutheri la Kusini mwa Tanganyika
f) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Usambara Digo
g) Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Uzaramoni – Uluguru

• Makanisa haya saba yalipoungana yalikwa na washarika laki tatu (300,000) tarehe 19/06/1963 hadi kufikia leo hii kanisa moja la Kilutheri lina zaidi ya dayosisi 25 na waumini zaidi ya milioni sita. (6,000,000)
• Siku ya leo tunaadhimisha miaka mia moja na thelathini (133) ya ulutheri Tanzania.
• Mwaka huu neno linalosindikiza sikukuu hii ni kutoka YOHANA 17;20-21 ambalo linaendelea kukaza juu ya umoja katika kanisa.
• Mlango huu wa 17 ni mlango wenye sala ya Yesu, kwanza anaanza kwa kujiombea yeye mwenyewe, kisha anawaombewa wanafunzi wake na anahitimisha kwa kuwaombea waumini wote wawe na umoja.
• Kipengele tulichosoma kinatufundisha mambo kadhaa

1. YESU NDIE MWANZILISHI WA KANISA
• Aliwaita wanafunzi na kuwaandaa kwa kazi maalumu ya kulihubiri neno lake ( Marko 3:14)
• Aliwaandaa kuifanya kazi aliyokuwa anaifanya yeye mwenyewe
• Aliwataka wawe na umoja ili waweze kuwa na lengo moja
• Maswali ya kujiuliza sisi wenyewe
a) Wewe umeandaa watu wa kufanya kazi ambayo unaifanya?
b) Je, wewe katika kazi/ huduma unayoifanya unazingatia umoja? Au unatengeneza makundi?

2. LENGO LA YESU NI KUONA KANISA MOJA
• Mungu anawataka waumini wote wawe na umoja na kuweka tofauti zao pembeni(Yesu anajua kuwa tunazo tofauti ila tukubali kuziweka pembeni na kuwa na umoja katika lengo moja)
• Umoja huu anataka ufanane na umoja wa Mungu na Yesu yaani umoja usio wa Kinafiki, umoja ambao hauwezi kutenganishwa. ( Umoja wetu katika utofauti wetu ufanye hata watu kushangaa tumeweza vipi kuwa wamoja)
• Umoja huu uwe ni umoja uliofungwa katika upendo wa kweli ( Yohana 13:34 – 35)
• Swali la kujiuliza waumini wale wanaojitenga na ibada kama vile kutokuwa kundini na kuanzisha madhehebu mengine bado Yesu anawahesabu kama wanafunzi wake? Wengine hata kukwepa majukumu ya kazi za umoja kama vile sadaka za umoja nk ni wafuasi wa Yesu Kweli?

3. UMOJA WA KIKRISTO UWE UMOJA WENYE MALENGO
• Umoja huu unapaswa uwe umoja unaoendelea kukua kama tulivyoona historia ya kanisa letu.
• Umoja huu uwe ni umoja wenye imani moja
• Umoja huu uwe ni umoja unaoendeleza utukufu wa Mungu ulimwenguni kote.
• Umoja unaosogeza waumini wote kuwa familia moja, kijiji kimoja. Tukitambua kuwa Yesu ndie mwanzilishi wa utandawazi ( Matayo 28:19 – 20, Mdo 1:8)
• Kanisa la Kiinjili la Kilutheri kwa kutambua kwamba misioni ya Bwana Yesu inaendelea kukua na kupanuka imeendelea kujitahidi kuleta umoja kwa kuweka uwiano wa sadaka za umoja ili kukidhi hitaji hili ambazo zinafanya kazi ya:-
a) Kutuma wachungaji maeneo ya misioni ya ndani na nje ya nchi
b) Kuhisani masomo ya wanafunzi wanaotoka maeneo ya misioni
c) Kuendesha vituo vya kazi za umoja kama vile Ofisi kuu ya kanisa, Shule ya viziwi mwanga na Njombe, Radio sauti ya injili, Seminari ndogo ya Morogoro nk.
Mimi na wewe tumeshiriki vipi katika misioni hii ya Yesu?

HITIMISHO
• Roho mtakatifu atusaidie kutambua kusudi la Yesu kwa kanisa lake nasi kama wafuasi wa kweli tuungane kwa upendo kuliendeleaza kanisa la Mungu.
• Umoja ni silaha kubwa sana katika huduma yetu ya uinjilisti. Ubora wa ushirikiano wetu unawavuta watu wengi kwa Mungu na udhaifu wa umoja wetu unalitawanya kundi la Mungu na kulipoteza huku ushuhuda wetu ukiendelea kuwa dhaifu
• Tuwavute watu kwa Mungu kwa kudumisha umoja miongoni mwetu.
AMEN.

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 1 BAADA YA UTATU TAREHE 14/06/2020

MADA: MUNGU AU ULIMWENGU

MASOMO:
ZABURI 78: 17 – 22
YOHANA 7:40 – 52,
MATENDO YA MITUME 5: 34 – 42

SHABAHA: Wasilkilizaji waweze kutambua kuwa uchaguzi sahihi nu ule wa kuchagua Mungu kwa sababu wakati wote yupo sahihi.

UTANGULIZI
Biblia inatufundisha kuwa Mungu sio nguvu Fulani tu inayomuwezesha mwanadamu kufanya jambo Fulani bali ni nafsi hai na hili huonekana wazi mtu unapokubali kumjia yeye na kupata mahusiano na ushirika nae (Yn 17:3)

Mungu ni nafsi hai iliyojidhihirisha kwenye nafsi tatu ili kumsaidia mwanadamu asibaki tu na ujuzi mdogo au hisia tu.(Yer 1:1 – 3, 2Pet 1:21)

Mungu ni wa milele asiyetawaliwa. Hawezi kupimwa kwa kipimo cha wakati, kwa sababu yeye hana mwanzo wala mwisho (Zab 90:2, Isa 48:12, Yn 5:26) Hana haja ya kutoa hesabu mahali popote wala kwa kiumbe chochote na hana haja ya kutoa sababu kwa uamuzi wake wala kuelezea matendo yake (Zab 115:3, Mdo 4:48) ingawa katika neema yake mara nyingine anafanya hivyo (Mwa 18:17 – 19, Efe 1:9) Hekima yake haina kikomo na hivyo iko nje ya uwezo wa mwanadamu ( Zab 50: 10 – 13, Mdo 17:24 – 25) Jambo lolote analolitenda analitenda kwa sababu ameamua hivyo, wala si kwa sababu alilazimika kufanya hivyo (Efe 1:11)
Mungu ni mwenye enzi na mamlaka yote. Hakuna kikomo kuhusu kuwepo kwa Mungu au ujuzi wake. Jambo hili ni kweli kwa furaha na hofu. Kwa furaha sababu hakuna mtu amtegemeaye ataweza kutengwa naye; na kwa hufu kwa sababu hakuna dhambi inayoweza kufichwa mbele zake ( Zab 139: 1 – 12, Ebr 4:13).

Mungu habadiliki lakini anajibu na kuitikia, Mungu asiyebadilika maana yake hana kikomo wala mwanzo wala mwisho hivyo hana namna ya kuongeza au kupunguza hali na sifa zake. (Kut 34:6 – 7) kutokubadilika kwa Mungu kuna maana kuwa yeye ni thabiti katika matendo yake yote(Ebr 6:17 – 18, Yak 1:17)

Biblia inaeleza ulimwengu ni vitu vilivyoumbwa na Mungu au watu wanaoishi katika ulimwengu (Zab 90:2, 98:7,9) kwa sababu ya dhambi ulimwengu ulikuwa sehemu ambamo shetani anatawala katika maisha ya watu (Yn 12:31, Rum 5:12 1Yoh 5:19) mara nyingi biblia inasema juu ya ulimwengu kuwa ni jambo lililo ovu au kinyume cha Mungu (Yn 7:7, Yak 4:4). Ulimwengu katika maana hii ni jambo la wanadamu wenye dhambi pamoja na tabia mbaya zilizo alama za wanadamu wenye dhambi.

Mkristo hawezi kushinda majaribu ya ulimwengu kwa kutumia mbinu za ulimwengu. Njia moja tu ya kushida ulimwengu ni kutegemea nguvu ya Kristo, aliyemshinda shetani aliye mkuu wa ulimwengu huu (Yn 12:31, 1Yoh 5: 4 – 5)
Kwa kuzitegemea nguvu za Mungu wanadamu wanao uwezo wa kuushida ulimwengu na kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Wote tunaalikwa kati ya Ulimwengu na Mungu basi tuchague Mungu Huku tukifahamu haya ambayo neno la Mungu linatufunza katika somo nililolisoma kuwa:-

1. KAZI YA MUNGU HAIHITAJI KUJIHURUMIA KULIKO KUMTEGEMEA YEYE
 Wanafunzi wakiwa na ujasiri wa hali ya juu pamoja na kutambua wivu uliotawala kwa ajili ya mafanikio yao, huku wakiwa wamepigwa marufuku kali kufundisha kwa kutumia jina la Yesu na ufufuo wake na wakitambua mamlaka ya baraza lile na uwezo wa wanachoweza kuwafanyia hata kuwaua ila waliendelea kuwaeleza wazi kuwa wao ndio waliomuuua Yesu pasipo kujali nini kitawapata kutokana na ukweli huo.

 Hii ndio kazi ya wakristo wote kutokufungia macho uonevu unaojitokeza na kueleza ukweli wote kwa yeyote pasipo kujali chochote ambacho kinataka kukuondoa kwenye imani ya kumtegemea Mungu

2. UKIWA NA UHAKIKA NA NGUVU ZA MUNGU MAMBO YA DUNIA HAYAWEZI KUYUMBISHA IMANI YAKO
 Jumapili iliyopita tulijifunza juu ya Farisayo aitwae Nikodemu ambaye alikuwa mwanafunzi wa siri wa Yesu Kristo ambaye alikuwa mwalimu wa torati, tajiri na aliyeheshimika na sasa wanafunzi wake wanapoanza huduma tunakutana na Mfarisayo mwingine ambaye ni mwalimu wa torati, tajiri na aliyeheshimika sana ambaye anaonyesha anakuballiana na mafundisho ya Yesu na anatoa maamuzi ya hekima kuwa mambo amabyo yameanza ambayo asili yake sio Yesu Kristo basi hufa ila kama yameanzishwa na msingi wa Yesu Kristo kamwe hayawezi kuvunjika na ni hatari kupambana nayo. Na Ushauri huu unapokelewa.

 Yanaweza kutokea mambo ambayo huyaelewi ila kwa vile una uhakika na nguvu za Mungu basi mwachie Mungu mwenyewe ni hakimu mwenye haki.

3. HATUHITAJI KUWAOMBEA MABAYA ADUI ZETU
 Wanafunzi wanachapwa viboko na wanapoachiwa wanaondoka kwa furaha kuwa wamehesabiwa mateso kwa ajili ya Yesu na wanadumu wakiomba na kufundhisha juu ya uweza na Mungu huku wakitambua kuwa ulimwengu hauwezi kuwafanya chochote.

 Adui zetu wakikaza kutuudhi nasi tuzidi kuongeza kiasi cha furaha yetu tukitambua kuwa nguvu za Mungu zitatupatia haki yetu.

HITIMISHO
Mungu atuwezeshe tuweze kumtumikia kwa uaminifu na ujasiri pasipo kuogopeshwa na vitisho vya wote wanaoukataa ukweli pasipo kujihurumia sababu Mungu mwenyewe asiyetawaliwa wala kubadilika atatulinda daima.

MUHUTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 07/06/2020

MUHUTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 07/06/2020

SIKU YA UTATU MTAKATIFU: BABA, MWANA NA ROHO MTAKATIFU

ZABURI 118:24-29
1wakoritho3:10- 12,
YOHANA 3:1-15

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kutambua kuwa Mungu anapenda wote wawe na umoja kama yeye alivyo mmoja katika nafsi tatu.

1. UTANGULIZI
• Nitaanza somo letu leo kwa kueleza kwa Ufupi utatu ni nini.

2. UTATU NI NINI?
• Utatu mtakatifu ni hali ya kuwa Watatu katika umoja kamili. Jina hilo linatumika hasa kufafanulia imani ya Wakristo wengi kwamba Mungu pekee, ni nafsi tatu zisizotenganika kamwe Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

• Katika Biblia, Kwa agizo la Yesu watakaomuamini wanatakiwa kubatizwa kwa jina la hao watatu (Injili ya Mathayo28:19). Agizo hilo la mwisho lilifuata na kujumlisha mafundisho yake mbalimbali kuhusu Baba, kuhusu yeye mwenyewe kama Mwana na kuhusu Roho Mtakatifu.

• Ufafanuzi wa kitheolojia, Umoja wa Nafsi hizo unatokana na asili yake pekee, yaani Baba ambaye ndani mwake anamzaa Mwana kama mwanga toka kwa mwanga, kama Neno au Wazo lake (Hekima), tena anamvuvia Roho Mtakatifu kama Upendo ambao unamuunganisha na Mwana na kukamilisha umoja wao.

• Katika matamko rasmi ya Kanisa, Imani hiyo ilizidi kufafanuliwa hasa katika karne IV, mitaguso mikuu ya kwanza ilipochukua msimamo dhidi ya wazushi waliokanusha uungu wa Yesu na wa Roho Mtakatifu. Ilipata muundo wa kudumu katika Kanuni ya Imani ya Nikea-Konstantinopol iinayotumika hadi leo katika madhehebu mengi ya Ukristo.

• Kwa imani hiyo tunapaswa kusadiki hasa Utatu wa Mungu pekee, kwamba ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Milele yote Baba kwa jinsi alivyo ndani mwake anamzaa Mwana na kumvuvia Roho Mtakatifu, kama vile jua linavyotoa mwanga na joto lisitenganike navyo. Mwana, ambaye “ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake” (Eb 1:3), alisema: “Nimekuja kutupa moto duniani” (Lk 12:49). Naye Roho aliwashukia wafuasi wake “kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu” (Mdo 2:3-4).

• Mungu hagawanyiki hata kidogo, bali daima ni Umojakamili. “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” (Mk12:29). Tumuabudu yeye peke yake katika nafsi tatu, na Utatu wa nafsi katika Umoja wa hali yake, tusichanganye nafsi wala kugawa Umungu. Baba si Mwana wala Roho Mtakatifu. Mwana si Baba wala Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu si Baba wala Mwana. Lakini milele yote nafsi hizo tatu ni Mungu yuleyule pasipo tofauti ya kuzitenganisha: kila moja imo ndani ya nyingine. “Mimi na Baba tu umoja” (Yoh10:30).

• Tumejua kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu kwa sababu Baba aliwatuma kwetu Mwanae na Roho Mtakatifu. “Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, ‘Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye’” (Math 3:16-17). Naye akaagiza, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu” (Math 28:19). Ni nafsi tatu zenye jina moja, yaani Umungu mmoja tu.

• Umoja wa Mungu unategemea hasa kwamba Mwana na Roho Mtakatifu wanachanga Umungu wa Baba, ambaye wanatokana naye pasipo utengano wowote. Baba anajifahamu na kujipenda: wazo analojifahamu ndiye Mwana, upendo anaojipenda katika wazo hilo ndiye Roho Mtakatifu. “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yoh 17:24).

• Nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji, kila nafsi akiuchangia kulingana na sifa yake maalumu ndani ya Utatu. Baba Mwenyezi sifa yake ni Uwezo. Mwana kama Neno la Baba sifa yake ni Hekima. Roho kama Pumzi ya uhai ya Baba sifa yake ni Upendo. Katika Uwezo wake Baba anafanya yote kwa Hekima na Upendo, hasa katika utume wa Mwana aliyefanyika mtu na katika utume wa Roho kama paji. “Amin, amin, nawaambia: Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile” (Yoh 5:19).

4. MUNGU ANATAKA UMOJA WA KANISA UIGE MFANO WA NAFSI TATU ZA MUNGU
• Ule utukufu ambao Yesu alikuwa nao kabla hajaja duniani wa kumuona baba na Roho mtakatifu ambao anamuomba Baba amrudishie atakapo kuwa mbinguni ndio anaouomba utukufu huo ulikalie kanisa lake, wote wawe na Umoja na tabia zote za Ki- Mungu, tabia zilizo njema ambazo ni Upendo, Utakatifu, haki, rehema nk.

• Umoja wa nafsi za Mungu kama nilivyoeleza ni umoja ambao hautenganishwi kamwe hivyo ndivyo ambavyo Mungu anataka kuona kanisa lake linakuwa na umoja.
5. UMOJA TULIONAO MUNGU ANATAKA TUUIMARISHE ZAIDI
• Yesu anaomba umoja wetu upate kukamiika ili wanafunzi wajue kuwa Mungu anawapenda sana kama jinsi anavyompenda Yesu na wanapaswa kushikwa na upendo ule ule ambao Baba na Mwana wanao ili utukufu wake uzidi kudhihirika na ulimwengu ujue nguvu zake.

• Umoja ulionao na mwenzako kama mmoja wa kiungo cha kanisa la Mungu umetawaliwa na Upendo wa kweli? Mungu anatutaka pamoja na umoja pia tuwe na upendo wa Kweli miongoni mwetu.

6. UMOJA NA UPENDO WETU UTUWEZESHE KUITIMIZA KAZI YA MUNGU
• Yesu Kristo anawataka wanafunzi wake kuifanya kazi yake ambayo anaianzisha pale msalabani ya kumkomboa mwanadamu wawe wainjilisti wazuri katika kuifanya kazi ya Mungu na kulinda Umoja wa kanisa wakati wote wa huduma yao.

• Mungu anakutaka na wewe kuendelea kazi hii njema ya kuhakikisha kanisa linaongezeka kukua huku likidumisha umoja na Upendo.

7. HITIMISHO
• Mungu mmoja mwenye nafsi tatu atuwezeshe tuweze kuwa na umoja wa kweli ulio tawaliwa na Upendo Miongoni mwetu.

AMEN.

MAHUBIRI YA SIKU YA PENTEKOSTE (Holy spirit reveal) 31/05/2020

1.0 UTANGULIZI
 Jumapili ya Leo neno la Mungu linatukumbusha kuwa Roho mtakatifu ni Msaada wetu katika maisha yetu.
 Roho Mtakatifu anatuwezesha kila Mkristo, bila kuzingatia, umri,jinsia au hali ya mtu katika jamii, ili kutoa unabii, kuota ndoto, na kuona maono.
 Roho Mtakatifu anawashukia waumini wote ili kutusaidia kufanya kazi ya Mungu hapa duniani na kutulinda ( Kut 31:2 -3, Hes 11:29, Zab 51:11)
 Roho mtakatifu ni muhimu sana katika kanisa la Mungu kwa sababu anatusaidia kuishi maisha matakatifu na kutimiza mpango wa Mungu katika maisha yetu..
 Katika unabii ambao tumeusoma kutoka kitabu cha Yoel tunaona kuwa ulitimia siku ilie ya Pentekoste na Petro aliyarudia maneno haya (Mdo 2:16 – 21)
 Katika unabii huu tunajifunza mambo kadhaa

2.0 ROHO MTAKATIFU YUPO KUWASAIDIA WATU WOTE
 Yoel anatabiri kuwa Roho atawashukia watu wote na rika zote ili kuwasaidia, ili Mkristo uweze kusaidiwa unapaswa kutulia katika utakatifu na Roho Mtakatifu aweze kukupa Muongozo sahihi.
 Ukiwa umefanikiwa sana usiache kumtumikia Mungu kwa sababu bado kuna mazuri zaidi ya hayo yapo mbele yako ambayo Mungu amekuandalia.
 Ukiwa katika mateso, maumivu na changamoto za dunia usikate tamaa sababu bado kidogo kuna siku njema zinakuja ambazo Mungu amekuandalia.

3.0 HATARI IPO KWA WALE WATAKAOMKANA ROHO MTAKATIFU
 Yoeli anatukumbusha kuwa ipo siku ya Hukumu inayokuja mbele yetu na kwa wale maadui wote wa Mungu siku hiyo itakuwa mbaya sana kwao sababu yatatokea mambo mengi ya ajabu.

4.0 KILA ATAKAYEMKUBALI ROHO MTAKATIFU ATAOKOLEWA.
 Neno la Mungu linatuhakikishika kuwa pamoja na dhambi nyingi kuongezeka na watu kumuacha Mungu ila wapo watu ambao bado wataendelea kumtegemea Mungu na anasema hao wote ambao wataendelea kumtegemea wakimuita jina lake hakika atawaokoa.

5.0 HITIMISHO
 Kila Mmoja atulie katika maongozi ya Roho Mtakatifu ili tupate kulindwa na kuelekezwa katika maisha ya Utakatifu.
AMEN.

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA KABLA YA PENTEKOSTE EXAUD MAANA YAKE SIKIA KUOMBA KWETU TAREHE 24/05/2020

KKKT DAYOSISI YA KUSINI ,JIMBO LA NJOMBE, USHARIKA WA UWEMBA,MTAA WA MJIMWEMA

MADA: KUNGOJEA AHADI YA BABA

MASOMO:
ZABURI 42:8 – 11,
YAKOBO 5:13 – 15
*YOHANA 16: 1 – 13

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya Utakaso wetu kutuwezesha kufika mbinguni hivyo wasikilize maongozi yake.

UTANGULIZI
 Leo tunajifunza juu ya kungojea ahadi za Mungu ambazo ametuahidi kwa ajili ya upendo wake kwetu na pia kwa ajili ya maombi ambayo tumepeleka kwake ambayo tunauhakika kuwa ameyasikia na yupo tayari kutujibu kwa wakati ambao ni sahihi kwake.

 Katika somo hili la injili ya Yohana hapa Yesu anazungumza na wanafunzi wake akiwa na furaha kuwa anarudi kwa baba yake na huku wanafunzi wakiwa na huzuni kwa kuachwa na Yesu ila anaahidi kuwa atatupatia msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu.

 Katika mistari hii yote tuliyosoma tunaweza kuona mambo mengi amabyo yanaleta elimu kubwa sana kwetu ila nataka tuyaangalie haya machache kwa siku ya leo.

1. YESU KRISTO NI NGAO YETU MAISHANI
 Yesu akiwa anataka kuwapa habari wanafunzi wake kuwa atawaacha ila atawapa msaidizi anataka wanafunzi wake waelewe kuwa wakati akiwa nao chuki zote na adha zilielekezwa kwake kama kiongozi wao ila sasa anapoondoka watambue kuwa wao watabaki kama kiongozi hivyo chuki na adha zitaelekezwa kwao.

 Habari hii inawahuzunisha wanafunzi ila Yesu anataka kuwaandaa wajue kuwa watapitia hayo ila wakiwa nae kwa njia ya Roho Mtakatifu atakayewalea baadae basi wataweza kuvumilia.

 Maisha ya mtu aliye ndani ya Yesu Kristo yanaweza kupita katika chuki, dhiki na mateso ila ukiwa na Yesu atakuwezesha kuyastahimili yote na kuvuka salama.

 Maisha nje ya Yesu ni maisha yaliyo rahisi kushambuliwa na kuumizwa na hata kufa hivyo tusiondoke kwenye mikono salama ya Yesu Kristo.

2. ROHO MTAKATIFU NI MSAIDIZI AMBAYE KILA MTU ANAPASWA KUWA NAE.
Yesu anaahidi kuwa wanafunzi wake wasihuzunike sana sababu atawapa msaidizi ambaye atafanya mambo kadhaa katika maisha yao

a. Atawatetea na kupambana na wapinzani wao

b. Kuwafundisha na kuwasaidia kuelewa mambo ya sasa na baadae

 Ni kweli tunahitaji mtetezi na mfundishaji wa kweli iti tuwee kuelewa mambo yanayoendelea kwenye maisha yetu na ulimwenguni kwa ujumla.

 Yapo mengi yanayotuumiza na kututesa na yapo mengi ambayo tunajitahidi kuyaelewa ila bado hatujayaelewa hivyo msaidizi huyu tuliyeahidiwa ambaye ni Roho Mtakatifu ktujitahidi aweze kuwepo katika maisha yetu wakati wote.

3. HUZUNI HUTUONDOA KWENYE MPANGO WA MUNGU
Kuhuzunika sio kubaya ila kuhuzunika kunakopelekea mtu kupoteza matumaini huko ni njia ya kutuelekeza kuondoka kwenye mpango wa Mungu.

Tunawaona wanafunzi walikuwa na huzuni hadi wakashindwa kuona furaha ya Yesu kurejea kwa baba yake na pia wakawa hawaelewi waliyokuwa wanaambiwa na Yesu hivyo Yesu akawaambia itabidi niache kuzungumza nanyi hadi Roho Mtakatifu atakapowajia awafundisha yote yanayotoka kwangu.

a. Huzuni inaweza kukufanya ukawa mbinafsi na kujipendelea pasipo kutazama wengine na Baraka wanazoweza kupata kwa maamuzi wanayofanya kama wanafunzi walivyojifikiria wao tu na kushindwa kumfikiria Yesu Kristo

b. Huzuni inapelekea kushindwa kusikiliza sauti ya Mungu na hata kusababisha Mungu acheleweshe ujumbe ambao alitaka kukupa kama Yesu alivyofanya kwa wanafunzi wake.

4. SIKU ZOTE YESU NI MSHINDI
 Ulimwengu unaweza kufikiria umeshinda kwa kumtesa Yesu na wanafunzi wake lakini utalipa kwa dhambi zake wakati Mungu atakapotangaza hukumu.

 Ulimwengu utahukumiwa juu ya dhambi yake ya kutokumwamini Yesu Kristo ambaye hutupatia haki ya kweli kwa njia ya kifo, kufufuka na kupaa kwake kwenda mbinguni.

 Mwanzoni unaweza kufikiri umeshinda kwa kuwanyanyasa, kuwaonea na hata kuatesa watu wa Mungu lakini ukweli ni kuwa Mungu hatakubali ufanye hivyo wakati wote lazima atakufikisha kwenye hukumu hivyo tujitahidi kukaa na Yesu aliye mshindi wakati wote hata kama tunapitia magumu.

HITIMISHO
Mungu atusaidie tuendelee kudumu katika kumwamini yeye kwani yeye ndie anayeyajua maisha yetu atatulinda na kutushindia wakati wote.

AMEN