Category Archives: Uncategorized

JUMAPILI YA 11 BAADA YA UTATU 23/08/2020

Somo:TUWE WANYENYEKEVU
fungu;LUKA 21:28-33

Bwana Yesu asifiwe…..

Unyenyekevu ni nini? Unyenyekevu ni hali ya moyo na akili inayomfanya mtu ajikubali alivyo na awakubali wengine walivyo. Kwa njia ya unyenyekevu mtu anatambua analopaswa kutenda na analitenda na pia asilopaswa kulitenda na halitendi. Kwa njia ya unyenyekevu, mtu anawapa wengine nafasi ya kuwa wanavyotakiwa kuwa katika haki. Kwa njia ya unyenyekevu, tunakomesha vilema vyetu vyote vya majivuno, kiburi, maringo, kujionaona na kujikweza.

Fadhila ya unyenyekevu inachukuliwa kuwa ya msingi na kiongozi wa fadhila nyingine zote. Martin luther anaendelea kusema kuwa “Kimsingi ni katika unyenyekevu mtu anafanywa kuwa mfuasi wa Kristo, na kwa hilo roho inaandaliwa kuungana na Mungu.” Mambo yote ni lazima yapate msingi wake katika unyenyekevu. Unyenyekevu unachukua nafasi ya kwanza kwa vile, unafukuza majivuno.

Fadhila ya unyenyekevu inatudai kujishusha ili tuinuliwe. Inatufanya tujione si kitu ili tuonekane kuwa ni kitu. Inatufanya tuwajali zaidi watu kuliko kujijali na kujipendelea sisi wenyewe. Inatufanya tuoneshe upendo wetu zaidi kuliko kutaka kupendwa. Inatufanya tuwaheshimu zaidi wenzetu kuliko kutaka kuheshimiwa.

Kwa njia ya unyenyekevu, tunaweza kufundishwa, kuelekezwa, kuongozwa, kuonywa, kulindwa, kutetewa na kukuzwa kwa ujumla. Ni fadhila ya msingi sana katika maisha ya mahusiano ya kila siku katika familia na katika jumuiya yoyote ile ya watu. Hata marafiki wa kawaida tu, au wachumba wakikosa unyenyekevu basi mahusiano yao daima hayatakosa malumbano, matusi, dharau, ukandamizaji na kila aina ya mateso.

Pengine watu wengi hushindwa kuishi na sisi kwa sababu tunakosa unyenyekevu, na ndio maana, hatuonyeki, haturekebishiki hatupendeki, hatuelekezeki, hatufundishiki, daima tunajiona kuwa ndio wenye haki sana mbele za watu na mbele za Mungu. Kukosa unyenyekevu kunatutenga na fadhila za Mungu. Tazama yule mfarisayo aliyekosa unyenyekevu akajiona kuwa yeye ndiye mwenye haki sana. [Lk 18:9-14]

Familia isiyojua unyenyekevu, ni uwanja wa vita daima. Vita za maneno na za mikono hazitakwisha. Tangu mwanzo wa malezi watoto wafundishwe juu ya umuhimu wa unyenyekevu. Unyenyekevu ni tendo la kijasiri kwa sababu linakudai kujishusha, kukomesha maringo, kiburi, kujikweza na majivuno. Walio wanyenyekevu daima hupata kibali machoni pa Mungu. Neno linasema “…Mungu huwapinga wajikwezao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Yak 4:6).

Wazazi katika familia, wakinyenyekeana wao kwa wao hapo wanakuza zaidi upendo wao. Kiburi, maringo, dharau na majivuno, hufukuza upendo. Lakini unyenyekevu hukuza na kudumisha upendo. Inapotokea kwa sababu zozote wazazi wanaoneshana umwamba, hakuna anayetaka kujishusha hata pale linapotokea kosa au kwazo la wazi, hapo upendo na furaha ya maisha ya ndoa huingia katika dosari kubwa.

Ndoa nyingi zimeingia katika migogoro ya kudumu sio kwa sababu ya matatizo makubwa, hasha! Pengine ni makosa madogomadogo ya kawaida kabisa ya kibinadamu. Lakini kwa vile hakuna ile hali ya unyenyekevu, kuwa tayari kujishusha, kila mtu anataka kujionesha yeye ni zaidi, na yupo sahihi zaidi ya mwenzake; hapo ndipo mgogoro hukuzwa zaidi.

Hapa rai ya moja kwa moja tunaipeleka kwa wanandoa! Wanandoa tukitaka amani, utulivu na maelewano ndani ya ndoa zetu, tuwe wanyenyekevu. Tukomeshe vilema vya kiburi, dharau, kujiona na maringo. Unyenyekevu ni daraja ya kufikiana na kuafikiana. Ukiwa mnyenyekevu, hata pale unapopatwa na tatizo, mwenzi wako ni rahisi kukuelewa, kukupokea na kukuinua. Lakini ukikosa unyenyekevu, utamfanya mwenzio ashangilie ukipatwa na mabaya.

Unyenyekevu, ni kiti cha kutuweka katika mazungumzo yenye mwafaka daima. Bila unyenyekevu, kila neno utakalotamka litakuwa na virusi vya fujo. Wazazi tukiwa wanyenyekevu, watoto wetu wataiga mwenendo wetu wa unyenyekevu nao pia tutawafundisha unyenyekevu. Sisi wazazi ndio waalimu wa maadili katika Kanisa la nyumbani, basi, na tujitahidi kuwa wanyenyekevu.

Na mtume Paulo anaelekeza kuuambata unyenyekevu, kwani ndiyo njia ya kujenga usitawi. Anasema “msifanye chochote kwa moyo wa fitina au majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu ninyi kwa ninyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu, bali faida ya mwenzake” (Fil. 2:3-4).
MWISHO
Bwana, anatualika sisi sote tuwe wanyenyekevu akisema ”jifunzeni kutoka kwangu kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu”. (Mt. 11:29). Na pengine anatuasa akisema “Anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejushusha atakwezwa (Mt 23:12). Unyenyekevu ni ngazi ya kupanda juu, zaidi na zaidi.
“Mtiini Mungu mpingeni shetani naye ata wakimbia”
AMEN.
imeandaliwa na
mwinjilist John
#0768386606

MAHUBIRI YA SIKU YA 10 BAADA YA UTATU

SOMO: LUKA 19: 41  – 44

UTANGULIZI
• Mungu ametupa kibali kukumbushana kuwa HAKI HUINUA TAIFA BALI DHAMBI NI AIBU KW WATU WOWOTE, msemo huu ni hakika hebu tuangalie mistari hii “kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja, dhambi iliiingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi” (Warumi 5:12)

• Dhambi ya mtu mmoja ilitufanya watu wote tuwe wadhambi ndio maana jamani hiii kitu dhambi ni aibu kwa watu wowote wanaojihususha nayo. Zaidi hebu tuone na hii “Basi tena, kama kwa kosa moja, watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtm mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya haki”(Rumi 5: 18 – 19)

• Wewe ukitenda haki taifa zima linapata kuinuliwa kwa haki uliyoitenda. Kila mmoja ajitahidi kuhakikisha taifa lake linainuliwa.

• Kwa mwaka huu kanisa letu linatukumbusha kwa kupitia injili iliyoandikwa na Luka kuwa ili uweze kuliinua taifa lako unapaswa KUZITAMBUA SIKU

• Kisa hiki ni cha Yesu akiingia Yerusalemu kwa shangwe yeye aliulilia mji wa Yerusalemu kwa kutokufahamu siku na muda wake wa kujiliwa. Katika kisa hiki tunajifunza

1. MUNGU ANAHUZUNIKA KWA WEWE KUTOKUZINGATIA MUDA WAKO
• Yesu anapoukaribia Mji anaulilia na kusikitika kwa wao kutokutambua kuwa kwa kuja kwake walipaswa kwenda kumpokea kwa furaha kwa sababu kwa kuja kwake ilikuwa ndio ukobozi wa Israel.

• Siku ya kujiliwa ni siku ya kufurahi, kuabudu, kusifu na ni siku ya amani kwa watu wote.

• Kwa nini watu hawaoni wala kutambua umuhimu wa siku ya Mungu.

a. Kwa sababu wanaongozwa na viongozi vipofu ambao hawaoni yatakayotokea mbeleni.

b. Wengine hawaoni sababu ya nafasi walizonazo, kama vile cheo, mal ink

c. Wengine wamekosa kuiona siku ya Mungu kwa sababu ya kujiinua na kujiona wao wanathamani kuliko kumuabudu Mungu

• Hata sasa wapo watu hawatambui nguvu za Mungu wala hawaoni umuhimu wa kuhudhuria ibada, jumuiya na matukio ya kiibada kwa mojawapo ya sababu nilizozitaja hapo juu, viongozi wengine wamewafanya watu kuwaona wao na kuwaabudu wao kuliko Mungu.

2. IPO HASARA KUBWA KWA WALE WALIO MBALI NA MUNGU
• Kwa wa Israel kutokutambua nyakati kwa sababu mbalimbali Yesu anaona mabaya juu ya mji wao wa Yerusalemu kuwa

a. Hekalu litabomolewa
b. Mji wa Yerusalem kuharibiwa na uzuri wake kupoea
c. Maadui zake watatawala juu ya Yerusalemu

• Hayo yote yanatokea kwa sababu tu wameshindwa kutambua wakati wa kujiliwa kwao. Kutambua na kuheshimu uwepo wa Mungu utakuepusha na matatizo mengi.

• Tujitahidi kwa wingi kuhakikisha kuwa Mungu anakuwa pamoja nasi wakati wote. Tukiutambua wakati amani itatulia juu ya maisha yetu na juu ya familia na taifa letu kwa ujuma.

HITIMISHO
• Yesu akiwa ndani yetu, akawa kiongozi wetu kwa neema yake atatuwezesha kutenda haki kwa ajili yetu na kwa ajili ya taifa letu.

• Kutenda dhambi sio tu kunamchukiza Mungu na kutupati mauti bali pia inasababisha taifa kuwa katika mabaya na machukizo mbele ya Mungu.

• Tujitahidi wote kutenda haki kwa neema ya Mungu ili baraka zake zidumu nasi milele na aweze kututahadharisha juu ya kesho yetu.

AMEN
Ev.john

SIKU YA BWANA YA 9 BAADA YA UTATU

IBADA YA TAREHE 09 AGOSTI 2020

TUENENDE KWA HEKIMA
ZABURI 119:25-32; LUKA 12:44-48

MAHUBIRI: KOLOSAI 4:2-6

1. UTANGULIZI
Katika mafafanuzi/mahubiri ya juma lililopita tuliangalia uhusiano uliopo kati ya hekima na busara. Tukawa tumesema kwamba hekima ni pana kuliko busara na ipo kama usukani wa kuiendesha busara. Busara ni namna ya kuamua jambo kwa akili kufuata mazingira. Na pia tukasema busara ni hekima inavyoonekana katika matendo. Na mkazo wetu ulikuwa katika uchaguzi wa busara. Mimi katika mahubiri nilikaza nguvu ya uchaguzi (the power of choice) na nikasema hivi tulivyo ni matokeo ya uchaguzi, nikamnukuu Dkt. John C. Maxwell aliyeandika “life is full of choices and every choice you make, makes you” (maisha yamejaa uchaguzi na kila uchaguzi unaoufanya unakutengeneza wewe). Mwisho niliorodhesha kanuni 4 za kutuongoza tunapofanya uchaguzi ili hekima ijidhihirishe katika maisha yetu.

(a) Zingatia vipaumbele na utabiri matokeo ya uchaguzi wako. Vipaumbele vinaongozwa na tunu ulizo nazo, maono na dhamira (values, vision and mission). Maana, changamoto mara nyingi sio kuchagua kati ya baya na jema bali kati ya zuri na zuri zaidi.

(b) Usikubali hisia zikuongoze. Epuka kufanya uchaguzi ukiwa na furaha sana ama huzuni/hasira
(c) Fikiria njia mbadala nyingi kabla ya kufanya uchaguzi na maamuzi.

(d) Jifunze kusikiliza dhamiri (Roho Mtakatifu). Je, unasikia amani moyoni na lile unalochagua? Amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu (Kolosai 3:15).

Leo tunaambiwa tuenende kwa hekima mbele za wasioamini. Na somo letu Kolosai 4:2-6 ligusa suala la uinjilisti tunaweza kufanya kwa njia ya wengine kwa kuwaombea (4:2-4) au tunaweza kufanya wenyewe moja kwa moja kwa kuuendea ulimwengu (4:5-6). Mungu anatutaka tuwe makini na maisha ya sala binafsi na pia namna ya kuhusiana na watu wa dunia hii, namna ya kuishi katika ulimwengu kwa hekima.

2. DUMUNI KATIKA KUOMBA
Yesu aliwahi kufundisha pia juu ya kuomba bila kukoma katika Luka 11:5-10. Mtu aliyefikiwa na rafiki usiku wa manane akiomba asaidiwe mikate kwa ajili ya mgeni, Yesu anasema ataamka kwa vile hataki kuendelea kusumbuliwa. Na pia katika Luka 18:1-8 Yesu alitoa mfano wa kadhi aliyemsaidia mwanamke mjane kwa kuona anamsumbua kila siku kuomba amsaidie.

Paulo akawahimiza Wakolosai kuendelea kuomba kwa bidii kama yeye alivyowaombea pia (Kolosai 1:3-8). Na anaposema dumuni katika kuomba tafsiri nyingine zinatupeleka kwenye maana ya kuwa uwe na nguvu (be strong). Uwe na juhudi kubwa. Huwezi kuendelea katika maombi kama huna pumzi na juhudi katika maombi. Ni kupambana, ni vita ya kuangusha ngome za Shetani.
Maombi sio tukio la mara moja katika maisha ya mkristo. Maombi ni jambo la kila siku mbele za Mungu (1 Thesalonike 5:17).

3. MKESHE KATIKA KUOMBA NA KUSHUKURU

Paulo anawahimiza Wakolosai kuwa macho, kukesha. Hii ni lugha ya kiulinzi au kiaskari. Walinzi hodari husimama usiku mzima ili kuhakikisha lindo lao lipo salama. Kwa hiyo wanapaswa kuwa macho wakati wa maombi wasilale usingizi. Mara nyingi mwana maombi anakumbana na uchovu wa mwili na hivyo kumfanya alale usingizi wakati wa kuomba.

Yesu aliwahimiza wanafunzi wake kukesha katika maombi katika matukio mawili muhimu. Pale alipokuwa nao mlimani katika tukio la kugeuka sura (Luka 9:28-33), Petro, Yakobo na Yohana walilemewa na usingizi na kushindwa kuomba. Mahali pengine ni katika Bustani ya Gethsemani (Mathayo 26:36 -46). Walilala na akawauliza, je, hamkuweza kukesha nami hata saa moja? (26:40).

Ipo vita wakati wa maombi. Unaweza kufikiri ni vita kati ya maombi na usingizi, lakini kama unaona rohoni, kuna nguvu nyuma yake. Hakuna wajibu unaweza kufanyika kwa ufanisi bila maombi. Lakini kila uombapo kuna upinzani! Pamoja na kuomba walipaswa kumshukuru Mungu.

Maombi siyo ”Mungu nipe hiki na kile na kile! Tunasogea mbele zake kwa shangwe na shukrani kwa Mungu. Katika shukrani tunamshukuru Mungu kwa namna alivyo na atendavyo. Ukuu wake, uaminifu wake, upendo wake, neema yake, hekima yake, na mengine mengi! Bila Mungu kututendea kwa namna atendavyo, hatuwezi kudumu hata siku moja.

Katika maombi, tunaomba ufalme wake uje. Ufalme wa Mungu ukija, tunapata mahitaji yetu na kwa namna Mungu aonavyo inafaa. Tunapoomba tunashukuru sio kwa sababu tumepata tayari, bali kwa sababu tunaamini kuwa tunapata, maana Mungu ni mwaminifu. Shukrani inatuhakikishia kuwa tunamwendea Mungu tunayemwamini kuwa anajibu.

4. MTUOMBEE MUNGU ATUFUNGULIE MLANGO WA NENO TUNENE SIRI YA KRISTO
Wakolosai wanahimizwa kuomba kwa ajili ya viongozi wao wa kiroho. Viongozi wa kiroho wasipopata neema au kibali machoni pa Mungu watakwamisha shughuli za kiroho. Paulo hakuwahimiza kuomba kwa ajili ya mahitaji yake binafsi bali Mungu afungue mlango kwa neno la Mungu, yaani fursa ya kuhubiri injili, tena ili anene siri ya injili impasavyo sio kama atakavyo yeye. Hapa kuna siri kubwa! Sio kila anayesimama mimbarani na kuhubiri anahubiri Neno la Mungu. Kwa hiyo Paulo anaomba Wakolosai wamwombee ili ahubiri Neno la Mungu. Paulo anasema kuwa alikuwa kifungoni kwa sababu ya uaminifu wa kuhubiri injili ya Kristo na alikuwa tayari kupokea matokeo ya uaminifu huo hata kupata vifungo zaidi. Ukihubiri Neno la Mungu katika kweli yake, wakuu wa giza kupitia watumishi wao watatikisika na kupanga njama za kukuangamiza! Ukiweza soma habari za Danieli. Au jifunze vizuri upinzani uliokuwepo katika huduma ya Bwana Yesu. Lakini wajapojipanga kwa upinzani wa aina yoyote ile, kuna nguvu ya Mungu itujiayo katika maombi! Katika maombi tunajadiliana na kusemezana na Mungu. Mungu huja kututia nguvu na kufanyika ngao yetu.

5. ENENDENI KWA HEKIMA MBELE YA WASIO AMINI/ULIMWENGU
Paulo anawakumbusha Wakosolai kuwa maisha ya kiroho sio tu kujifungia ndani kwa maombi bali wanahitaji kuishi hekima yao kwa vitendo, kuwa na busara kama tulivyojadili somo lililopita. Hii itawaongoza namna ya kuongea na kuishi. Kwa wakati ule, tayari kulikuwa na picha mbaya kuhusu ukristo. Lakini kwa njia ya hekima na mwenendo wao walitakiwa kuiondoa ile picha mbaya na kuuonesha ulimwengu uzuri ulio katika Bwana unaodhihirika katika maisha ya Wakristo. Mienendo yetu ni mahubiri yanayoishi. Tunapaswa kumdhihirisha Yesu Kristo katika maisha yetu pia, sio maneno tu!

6. MUUKOMBOE WAKATI
Neno kuukomboa wakati linabeba maana zifuatazo: kutumia wakati kwa njia nzuri kabisa (making the best use of time) kutumia kwa makini kila fursa inayojitokeza (making the most of every opportunity), au kutumia kwa ufanisi kila wakati unalionao (make effective use of our time). Mtume Paulo kwa Waefeso 5:15-20 anasema enendeni kwa hekima mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu na wasiwe wajinga. Kila nafasi katika maisha ni muhimu lazima itumike kwa ukamilifu wote na kwa manufaa. Ndio maana imesemwa kuwa wakati ni mali. Kiroho ni kama alikuwa anawaambia kuwa wakati ni mfupi tusikubali mtu afe bila kumjua Yesu. Lakini hata wakati huu wenye mabadiliko makubwa ya kiuchumi, muda ni moja kati ya rasilimali muhimu sana katika kuleta maendeleo. Wanaojua wanatumia vizuri. Kwa bahati mbaya wapo watu ambao hawajaelewa thamani ya muda hawatunzi muda mahali wanapo hitajika.

Kuna mtu alisema hivi: nilipokuwa mtoto sikuwa na cha kufanya zaidi ya kutambaa na kusubiri nisaidiwe hiki na kile, wakati huo muda ulikuwa unatambaa. Nilipokuwa kijana nilianza kuona hili na lile, nikawa ninaongea pia, lakini muda ulianza kutembea. Nilipokuwa mtu mzima tayari ninajua maana ya maisha, nilianza kushughulika na mambo muhimu, muda ulikuwa unakimbia kweli. Nimekuwa mzee, ninataka nirekebishe nilipokesea, muda umepaa! Haupo tena! Mhubiri anasema vizuri: ”Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako kabla hazijaja siku utakaposema…” (Mhubiri 12:1). Usipotumia wakati vizuri, utakuja kujuta!
Bwana Yesu alionesha kuwa wana wa ulimwengu, yaani walio wa ufalme wa giza wanajua kuutumia wakati (Luka 16:8). Lakini wana wa nuru ni wazito kweli! Kwa nini wana wa ulimwengu wanajua kuukomboa wakati? Mkuu wao anajua kuwa anao muda mfupi sana! Kwa hiyo amejipanga vya kutosha na watumishi wake wanamtii! Watu wa Mungu, tusipoukomboa wakati, tutapoteza dira. Mambo mengi yataharibika na hivyo tutamletea hasara Bwana wetu pasipo sababu! Lazima tuenende kwa hekima na kuuomboa wakati!

7. MANENO YENU YAJAE NEEMA NA MUNYU NA MPATE KUJUA JINSI YA KUJIBU
Njia nyingine ya kumtangaza Kristo ilikuwa ni kwa njia ya usemi wao. Anasema maneno yao yawe na neema na munyu. Yawe na chumvi ambayo kazi yake ni kutunza kitu kisiharibike na kutia ladha nzuri. Na busara (hekima iliyo katika matendo) ingewawezesha hata kujua jinsi ya kumjibu kila mtu. Walipaswa kujibu kufuata mafundisho ya biblia sio kwa jinsi wanavyojifahamu. Na kwa vile walidhaniwa kuwa wajinga wasio na akili, basi kwa njia ya usemi wao wangedhihirisha kuwa sio watu wa kawaida. Walitakiwa kutafuta neema ya kuwa wazungumzaji wazuri.

8. JUMLISHO
Kuenenda kwa hekima katika ulimwengu ulioanguka sio rahisi. Yesu alipokuwa anawatuma wanafunzi kwenda kuhubiri aliwaambia, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kuweni na hekima kama nyoka lakini wanyenyekevu kama njiwa. Kondoo wakati wote yupo na mchungaji wake. Bwana Yesu anatutaka tujue kuwa peke yetu hatuwezi. Ndio maana hapa Paulo anakaza kuomba na kuombeana. Mbwa mwitu wapo kila mahali, tena hata mahali tunapodhani tupo salama. Bila Mungu kutufumbua macho, hatutastahimili. Tunamhitaji Bwana wakati wote. Ndio maana tunaambiwa tuenende kwa hekima. Hekima ya kweli hutoka kwa Bwana. Tukiwa na Bwana, tunahakikishwa hekima. Atatuwezesha kunena na kutenda kama itupasavyo. Lililo kuu katika kuenenda kwetu, tuukoboe wakati. Maana tupo kwa kitambo. Muda hautusubiri. Basi Mungu aliyetuita atuwezeshe kuenenda kwa hekima nyakati zote. Amen

Na mchg. Dkt. George Mark Fihavango
Askofu
From Mwinjilist Joseph Mshana

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 8 BAADA YA UTATU

Somo:UCHAGUZI WA BUSARA

Masomo:
Zaburi 37:1-8
Marko 1:40-45
Mathayo8:11-13

UTANGULIZI
✏ Siku ya leo tunajifunza juu ya uchaguzi wa busara natumepewa injili mbili Marko 1:40-45; Mathayo 8:11-13. Uchaguzi ni kitendo chaku angalia ama kuoanisha kipi kinafaa ama kipihakifai.
✏Busara ni hekima au maamuzi sahihi
✏Sasa UCHAGUZI WA BUSARA maana yake ni kitendo cha kuangalia kipi kinafaa tena kwahekima.Maana unaweza ukachagua nakuona kinafaa lakini ukakosa hekima kwenye uchaguzi wako bado utakiacha kinacho faa zaidi kuliko hicho ulicho kichagua.Katika injili mbili za leo pamoja na zaburi tunajifunza mambo yafuatayo kutokana na kichwa hichi cha UCHAGUZI WA BUSARA;
1.HEKIMA KATIKA UCHAGUZI NI MWANZO WA MAFANIKIO
✏ Unaposoma injili ya Marko1:40-45 tunamwona mtu mwenye ukoma alimwendea Yesu akisema “Ukitaka, waweza kunitakasa” kwakauli hiyo alitumia hekima ya hali ya juu kumwomba Yesu amtakase kwamba kama Yesu mapenzi yake nikumuona mzima bas amtakase kama simapenzi yake amuache
✏Sisi kanisa la leo kuna mambo yanahitaji uchaguzi wenye hekima ndani yake ilituweze kufanikiwa kwa mfano unapomchagua kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako tambua huyo Bwana hataki mtu mzembe FANYA KAZI KWA BIDII
✏Lakini pia familia yenye mafanikio huatanguliwa na hekima ndani yao baba akiwa naheshima kwa mama na watoto watafanya hivo kwasababu baba amechagua fungu jema nala baraka

2.MATAIFA WATATUTANGULIA KUINGIA MBINGUNI KABLA YETA SISI TULIO OKOKA.
✏Biblia inasema katika Mathayo 8:12″bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”
✏Yesu ananza kwakusema watakuja watu kutoka mashariki na magharibi kaskazini na kusini watakuja kuketi kwa ibarahim,isaka,na Yakobo maana yake walioamini nawasio amini wote wataenda mbio kila moja njia yake lakini wale waliowagiza(wana waufalme mathayo8:13) ndio anasema watatupwa nje katika ufalme wagiza sasa kwanini tulioamini tutatupwa nje ni kwasababu ndani yetu wengi tumemchagua kristo lakini tunashwindwa kwend sawasawa na kanuni zake wengi tumekuwa wasengenyaji na mambo mengi laini mataifa wengine hawasali lakini wanajikita katika kutenda mema nandio maana tusipo kaasawa watatuzidi hata sisi
✏Ndugu zangu nawasihi tufanye kazi ya Mungu kungalibado mchana tuachague natufanye maamuzi saa hii wasitushinde wasio amini sisi tunanguvu zaidi yao.
3.NJIA ZETU NA MIPANGO YETU TUNAPASWA KUMKABIDHI BWANA
✏Mwimba zaburi anatuambia katika zaburi 37; 5 “Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya”
✏Kumbe sisi tunaomwamini kristo tunatakiwa kumchagua Kristo kuwa kiongozi wa mipango yetu nanirahisi tu nikukabidhi na kutumaini( kutarajiA au kuwa naimani) naye nilizima afanye tu sasa sasa kwanini watu wengi tunamkabidhi lakini hafanyi kwasababu;
✏Tumekuwa tunaishi maisha ya changanya changanya hatujachagua ninani wakusimamia mipango hiyo ingawaje wengine wanaileta kanisani lakini wakitoka wanaenda kwa waganga nandiomaana haifanikiwi kumbe sisi tulio amini tunapaswa kukabidhi na kuamini au kutumaini tu mwisho tusiongeze mengine yasiyo na mantiki
✏Tuanaambiwa kitarajiwacho kikikaiwa moyo huugua ni kwamba Unapo mkabidhi Bwana mipango yako tambua kuwa anafanya kwa mapenzi yake hapelekeshwi na yeyote hivyo jenga moyo wa UVUMILIVU
4.RIDHIKA NA HALI ULIYO NAYO
✏Ukisoma Zaburi 37:6 ” Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri”
✏Unajua mda wingine Mungu huwa anakuweka kwenye zone(sehemu) furani ili ujifunze sasa watu wengi tunapokuwa kwenye eneo hili huwa tunachagua hukumu mfano anapitishwa kwenye gumu fulani imani inashuka kanisani haendi anaacha kabisa kumbe swala ni kumuamini tu yeye ataitokeaza haki yako kama nuru
✏Mungu anatabia ya kujitukuza katika ya pito unalopitia hivyo mpendwa unapopitishwa kwenye gumu ama pito fanya uchaguzi wa busara usikurupuke maana anasema”Ataitokeza haki yako kama nuru,……”
MWISHO
✏Wito wangu kwenu naombeni mfanye maamuzi sahihi siku ya leo kama neno la Mungu linavyosema katika Joshua 24:15 “inasema chagueni hivemaeo mtakaye mtukatika”
AMEN.

MUHTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 26/07/2020

SOMO: Mwanzo 41:41-45

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, leo tunaangalia juu ya “NEEMA YA MUNGU YATUWEZESHA” yote tunayofanikiwa kuyafanya hapa duniani pamoja na magumu yote tunayopitia neema ya Mungu peke yake ndio inayotuwezesha kuonekana tulivyo, hatuwezi kujivunia akili zetu wala nguvu zetu wenyewe ila wakati wote yote tuyafanyayo tujue kuwa ni Mungu ametuwezesha.
Waandishi na mafarisayo wao walikuwa ni watu wa kushika sheria sana na kujitahidi kwa nguvu zao kuonyesha kuwa wanafahamu juu ya usafi na uchafu wa mtu ila Yesu anapotokea kwao anataka kuwabadiisha namna ya kufiki na kutambua mapenzi ya Mungu na kuondokana na mapokeo ya wazee.
Kwa somo hili tunajifunza haya yafuatayo

1. ASILI YA KWELI YA UNAJISI.
• Wayahudi walikuwa na sheria mbalimbali juu ya vyakula wakionyesha vingine ni safi na vingine ni najisi na hata jinsi ya kujiandaa kula. Walipoona wanafunzi wa Yesu wanakula bila kunawa mikono waliwahesabu kuwa ni najisi.
• Yesu anawataka watu wake kuelewa kuwa unajisi wa kweli hauwezi kuasilishwa na nguvu za nje bali kwa nguvu za ndani.
• Kile unachokipokea na kukiingiza katika mwili wako ndio kinachosababisha nguvu ya kutoa kile kilichopo ndani yako hivyo tunapaswa kuwa makini zaidi.

2. UTAMADUNI/MAZOEA YANAWEZA KUKUFANYA USIMUELEWE YESU
• Wanafunziwakiwa ni miongoni mwa wayahudi kwa kusikia mafundisho ya Yesu juu ya UNAJISI kutokana na maelekezo na torati walizoishi nazo kwa muda mrefu (Walawi 11: 1 – 47, Mt 5:17 – 18) hawakuelewa fundisho la Yesu walifikiri kuwa amekosea na kutaka mafafanuzi zaidi.
• Yesu aliwashangaa kwa kuzingatia walichokizoea zaidi kuliko kuisikiliza sauti yake na kuelewa ukweli wa neno la Mungu kama ilivyo kwetu sasa watu wengi kutokana na mazoea ya maishahawasikilizi Mungu anawata kufanya nini.

3. MATOKEO MAZURI AU MABAYA YA MAISHA YA MTU YANATOKA MOYONI
• Moyo wa mwanadamu ndio unaoleta matokeo ya aina zote ya mwanadamu, yawe mazuri au mabaya. (mithali 4:23)
• Moyo ukiathiriwa na dhambi ndiko ambapo mabaya yote hutokea (Mhubiri 9:3, Yer 17:9) na huwa mwanzo wa maovu yote (Mk 7: 20 – 23)

HITIMISHO
Wote tunapaswa kuelekeza macho yetu na umakini wetu wote katika mioyo yetu na kuilinda isiingiliwe na dhambi na kusababisha sisi kuwa waasi mbele za Mungu. ( Efeso 4:17 – 24, 1Petro 4: 1-3,) Haya yote yanawezekana ikiwa tutakuwa watii kwa neno la Mungu wakati wote na kujifunza kwa Mungu ( Mdo 2:28, 22: 16)
Kwa akili zetu ni Ngumu ila neema ya Mungu iliyokuu sana Kwetu inatuwezesha kufanya yote.
AMEN