MUHUTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 07/06/2020

MUHUTASARI WA MAHUBIRI YA LEO TAREHE 07/06/2020

SIKU YA UTATU MTAKATIFU: BABA, MWANA NA ROHO MTAKATIFU

ZABURI 118:24-29
1wakoritho3:10- 12,
YOHANA 3:1-15

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kutambua kuwa Mungu anapenda wote wawe na umoja kama yeye alivyo mmoja katika nafsi tatu.

1. UTANGULIZI
• Nitaanza somo letu leo kwa kueleza kwa Ufupi utatu ni nini.

2. UTATU NI NINI?
• Utatu mtakatifu ni hali ya kuwa Watatu katika umoja kamili. Jina hilo linatumika hasa kufafanulia imani ya Wakristo wengi kwamba Mungu pekee, ni nafsi tatu zisizotenganika kamwe Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

• Katika Biblia, Kwa agizo la Yesu watakaomuamini wanatakiwa kubatizwa kwa jina la hao watatu (Injili ya Mathayo28:19). Agizo hilo la mwisho lilifuata na kujumlisha mafundisho yake mbalimbali kuhusu Baba, kuhusu yeye mwenyewe kama Mwana na kuhusu Roho Mtakatifu.

• Ufafanuzi wa kitheolojia, Umoja wa Nafsi hizo unatokana na asili yake pekee, yaani Baba ambaye ndani mwake anamzaa Mwana kama mwanga toka kwa mwanga, kama Neno au Wazo lake (Hekima), tena anamvuvia Roho Mtakatifu kama Upendo ambao unamuunganisha na Mwana na kukamilisha umoja wao.

• Katika matamko rasmi ya Kanisa, Imani hiyo ilizidi kufafanuliwa hasa katika karne IV, mitaguso mikuu ya kwanza ilipochukua msimamo dhidi ya wazushi waliokanusha uungu wa Yesu na wa Roho Mtakatifu. Ilipata muundo wa kudumu katika Kanuni ya Imani ya Nikea-Konstantinopol iinayotumika hadi leo katika madhehebu mengi ya Ukristo.

• Kwa imani hiyo tunapaswa kusadiki hasa Utatu wa Mungu pekee, kwamba ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Milele yote Baba kwa jinsi alivyo ndani mwake anamzaa Mwana na kumvuvia Roho Mtakatifu, kama vile jua linavyotoa mwanga na joto lisitenganike navyo. Mwana, ambaye “ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake” (Eb 1:3), alisema: “Nimekuja kutupa moto duniani” (Lk 12:49). Naye Roho aliwashukia wafuasi wake “kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu” (Mdo 2:3-4).

• Mungu hagawanyiki hata kidogo, bali daima ni Umojakamili. “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” (Mk12:29). Tumuabudu yeye peke yake katika nafsi tatu, na Utatu wa nafsi katika Umoja wa hali yake, tusichanganye nafsi wala kugawa Umungu. Baba si Mwana wala Roho Mtakatifu. Mwana si Baba wala Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu si Baba wala Mwana. Lakini milele yote nafsi hizo tatu ni Mungu yuleyule pasipo tofauti ya kuzitenganisha: kila moja imo ndani ya nyingine. “Mimi na Baba tu umoja” (Yoh10:30).

• Tumejua kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu kwa sababu Baba aliwatuma kwetu Mwanae na Roho Mtakatifu. “Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, ‘Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye’” (Math 3:16-17). Naye akaagiza, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu” (Math 28:19). Ni nafsi tatu zenye jina moja, yaani Umungu mmoja tu.

• Umoja wa Mungu unategemea hasa kwamba Mwana na Roho Mtakatifu wanachanga Umungu wa Baba, ambaye wanatokana naye pasipo utengano wowote. Baba anajifahamu na kujipenda: wazo analojifahamu ndiye Mwana, upendo anaojipenda katika wazo hilo ndiye Roho Mtakatifu. “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yoh 17:24).

• Nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji, kila nafsi akiuchangia kulingana na sifa yake maalumu ndani ya Utatu. Baba Mwenyezi sifa yake ni Uwezo. Mwana kama Neno la Baba sifa yake ni Hekima. Roho kama Pumzi ya uhai ya Baba sifa yake ni Upendo. Katika Uwezo wake Baba anafanya yote kwa Hekima na Upendo, hasa katika utume wa Mwana aliyefanyika mtu na katika utume wa Roho kama paji. “Amin, amin, nawaambia: Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile” (Yoh 5:19).

4. MUNGU ANATAKA UMOJA WA KANISA UIGE MFANO WA NAFSI TATU ZA MUNGU
• Ule utukufu ambao Yesu alikuwa nao kabla hajaja duniani wa kumuona baba na Roho mtakatifu ambao anamuomba Baba amrudishie atakapo kuwa mbinguni ndio anaouomba utukufu huo ulikalie kanisa lake, wote wawe na Umoja na tabia zote za Ki- Mungu, tabia zilizo njema ambazo ni Upendo, Utakatifu, haki, rehema nk.

• Umoja wa nafsi za Mungu kama nilivyoeleza ni umoja ambao hautenganishwi kamwe hivyo ndivyo ambavyo Mungu anataka kuona kanisa lake linakuwa na umoja.
5. UMOJA TULIONAO MUNGU ANATAKA TUUIMARISHE ZAIDI
• Yesu anaomba umoja wetu upate kukamiika ili wanafunzi wajue kuwa Mungu anawapenda sana kama jinsi anavyompenda Yesu na wanapaswa kushikwa na upendo ule ule ambao Baba na Mwana wanao ili utukufu wake uzidi kudhihirika na ulimwengu ujue nguvu zake.

• Umoja ulionao na mwenzako kama mmoja wa kiungo cha kanisa la Mungu umetawaliwa na Upendo wa kweli? Mungu anatutaka pamoja na umoja pia tuwe na upendo wa Kweli miongoni mwetu.

6. UMOJA NA UPENDO WETU UTUWEZESHE KUITIMIZA KAZI YA MUNGU
• Yesu Kristo anawataka wanafunzi wake kuifanya kazi yake ambayo anaianzisha pale msalabani ya kumkomboa mwanadamu wawe wainjilisti wazuri katika kuifanya kazi ya Mungu na kulinda Umoja wa kanisa wakati wote wa huduma yao.

• Mungu anakutaka na wewe kuendelea kazi hii njema ya kuhakikisha kanisa linaongezeka kukua huku likidumisha umoja na Upendo.

7. HITIMISHO
• Mungu mmoja mwenye nafsi tatu atuwezeshe tuweze kuwa na umoja wa kweli ulio tawaliwa na Upendo Miongoni mwetu.

AMEN.