KKKT DKU SIKU YA BWANA YA 7 KABLA YA PASAKA

*IBADA YA TAREHE 15 FEBRUARI 2026*
SIKU YA BWANA YA 7 KABLA YA PASAKA (QUINQUAGESIMA/ESTOMIHI)

*YESU AIENDEA NJIA YA MATESO YERUSALEMU*
ZABURI 48:1-8; RUMI 11:25-27

*SOMO LA MAHUBIRI: MATHAYO 17:22-23*
WIMBO: TMW 415
MAFAFANUZI

1. *UTANGULIZI*
Katika Injili ya Mathayo Yesu anatabiri juu ya mateso, kifo na kufufuka kwake mara tatu. Hii inaonesha kuwa mateso na kifo cha Yesu hayakutokea kwa bahati mbaya bali yalikuwa sehemu kamili ya mpango wa Mungu wa wokovu. Utabiri huu unajitokeza katika Mathayo 16:21–23; 17:22–23; 20:17–19. 

Utakachokiona katika utabiri huo ni kwamba, hata kama alizungumza habari za kutiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani, kuteswa na kuuawa, bado kila mara alimaliza na kufufuka kwake. Maneno mengine yaliweza kukosekana, kwa baadhi ya tabiri; lakini kila mara kufufuka kumejitokeza. Hii ina maana kwamba, hata kama mateso ilikuwa lazima, Yesu alikuwa anatazama mbele kwenye matokeo ya hayo yote. Hapuuzii uwepo wa mateso dhihaka na kifo, lakini anaona kwamba hayo yanatumika kumfikisha kwenye utukufu. Na katika kuyasema, hafichi. Anaweka wazi kuwa yatampata, Yeye mwenyewe, si mwingine. Mkazo huo ulikuwa wa muhimu ili kutimiza unabii wa Isaya 53  kuteswa kwa masihi (the Suffering Messiah). Na hii ina maana kubwa katika theologia. Kuwa mfuasi wa Yesu hakumwepushi mtu na mateso au changamoto, bali kuna mthibiitsha kuwa yeye ni nani hata anapkuwa katika mateso. Na uthibitisho hapo ni kwamba, mateso yajapokuwa makali kiasi gani, ushindi upo. 

Wanafunzi walipaswa kujifunza maana ya ufuasi lakini hilo lilifichwa machoni pao, aliwaambia mtu akitaka kunifuata ajikane nafsi yake auchukue msalaba wake (Mathayo 16:24). 

*Mathayo sura ya 17 in sehemu kuu tatu:* 
(a)  *Mathayo 17:1-13 Utukufu wa Yesu unaofunuliwa*
Mistari nane ya kwanza inahusu Yesu kugeuka sura (17:1-8). Yesu alionekana katika utukufu wa hali ya juu sana na sauti ya Baba ikathibitisha utambulisho huo. Hiki kilikuwa kilele cha ufunuo wa Yesu. Halafu yanafuata mafundisho kuhusu Eliya/Yohana Mbatizaji  (17:9-13). Yesu ni Mwana wa Mungu na utimilifu wa torati na manabii. Lakini hali halisi ni mateso. Yohana mbatizaji alikuja wakamtesa. Vivyo hivyo watamtenda Mwana wa Adamu. 

(b) *Mathayo 17:14-21 Udhaifu wa Wanafunzi na dai la Imani*
Waliposhuka bondeni wanafunzi waliendelea kushuhudia hali halisi ya dunia, kijana aliteswa na pepo na wanafunzi waliteswa na Imani ndogo. Kwa hiyo wale wanafunzi watatu waliorudi na Yesu toka mlimani walikutana na maumivu ya dunia ambayo walitamani kuyakimbia waliposema wajenge vibanda 3. 
Wanafunzi 9 waliobaki bondeni wakati Yesu ameenda mlimani na wanafunzi 3 walishindwa kutoa pepo. Ndipo Yesu akatoa fursa hiyo kufundisha kuwa Imani ni kama chembe ya haradali. Nguvu ya huduma haitoki kwa mwanadamu bali inatoka kwa Mungu kupitia Imani. 

(c)  *Mathayo* *17:22* – *27* Njia ya Msalaba na Maisha ya wanafunzi duniani

Sehemu hii inahusu utabiri wa Yesu juu ya kuteswa, kufa na kufufuka kwake. Halafu ilifuata habari ya kodi na uhuru wa mwana. Kwa hiyo utukufu wa Yesu unaelezwa kwa njia ya msalaba. Na msalaba ni alama ya unyenyekevu na mateso. Kazi ya yake  ni kumfanya mtu anyenyekee kwenye kila mfumo. Kwa watawala – mtu awe mnyenyekevu; katika kuutumia uhuru wake, asijiinue, napo pia awe mnyenyekevu. Kazi ya mateso na msalaba ni kumleta mtu kwenye ukuu wa kweli – yaani ukuu wenye unyenyekevu na uliojaa upendo.  

Mathayo 17:22-23 tunakutana na siri ya mpango wa Mungu juu ya wokovu na hiki ndicho kitovu cha sura ya 17. Baada ya kuona utukufu pale mlimani, mateso ya dunia, udhaifu wa imani ya wanafunzi, Yesu anafunua sababu ya yote hayo na suluhisho lake. Hii ni njia ya msalaba na ufufuo. Kung’aa kusingeeleweka na mateso ya dunia yangetupeleka kukata tamaa na kukosa matumaini .
Mathayo 17:24-27 ni aina ya maisha ya wanafunzi baada ya kujua siri hiyo kuu. Wanaishi kwa unyenyekevu, wanalipa kodi ili kutowakwaza wengine, wanatumia uhuru wao kwa kwa unyenyekevu unaotokeza upendo na uwajibikaji.
2. *MATHAYO* *17:22* – *23* *UTABIRI* *WA* *PILI*
Walipokusanyika (walipokaa) Galilaya Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana. Hili si tangazo la kawaida, wala si tangazo la hofu na kushindwa bali ni taarifa ya mpango wa kazi ulioko mbele yao. Wao walikuwa hawaoni, kwa hiyo anawaambia mapema: msishituke, mpango unaofuata ni huu. Taarifa hii ilikuwa inawaandaa kisaikolojia. Na Kitheologia tunasema, ikiwa mtu anazunguka huko na huko akisema habari ya kifo chake na kufufuka kwake hata kabla havijatokea, ama ni kichaa au ni Mwana wa Mungu. Na kwa habari ya Yesu, alikuwa anawaambia jambo ambalo walikuwa hawajui. Hata kama mimi nipo katika mwili, ”Mwana wa Adamu”, mimi nina asili ya uungu. Hasemi kwa maneno, lakini maana ya kazi na ratiba anayoonesha inaibua hayo.

*Mwana wa Adamu*
Kwa mara ya kwanza habari ya Mwana wa Adamu inaonekana katika Danieli 7:13-14. Danieli anaona maono ya mbinguni, ambako kuna viumbe wa rohoni. Hata hivyo, kuna jambo la peke, anamwona mtu mwenye mwonekanekano au mfano wa mwanadamu – ndio maana ya Mwana wa Adamu. Danieli haelezi kirefu. Lakini alichokiona kimekuja kuwa wazi katika Yesu Kristo. Mungu ameuchukua mwili na kwa huo anatumia kuwakomboa wanadamu. Kwa huo atakuwa miongoni mwa watu – Mungu pamoja nasi; kwa huo atateswa. Alishuka na kunyenyekea lakini kunyenyekea kwake kumekuwa sababu ya wokovu kwa ulimwengu. Maana kama angebaki katika roho, hakuna mtu angethubutu kuunyosha mkono wake na kumtesa. Na hii ndio siri ya Kimasihi, na hapa neno Mwana wa Adamu limekuwa jina linaloficha siri kuu. Kuielewa unahitaji utulivu. Anajiita Mwana wa Adamu makusudi – anaficha asili yake halisi.

*Mwana wa Adamu anakwenda,* hili linaonesha kuwa ni safari ya makusudi kuuendea msalaba. Mungu katika mwili (Mwana wa Adamu) anakwenda msalabani. Kwa asili mwanadamu hukimbia hatari lakini Yesu anakaza uso kuyaendea mateso. Anayaendea mateso kwa upendo mkubwa wa kujitoa kwa sababu anajua nini anachofanya. Amekuja Kutenda mapenzi ya Baba, anajitoa kwa ajili ya rafiki zake ambao wana dhambi sio watakatifu. Yohana 15:13 Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Asingeweza kuyafanya hayo kama asingekuwa Mungu. Na sisi hatuwezi kujitoa kwa ajili ya wengine, Mungu asipokuwa ndani yetu. Hatuwezi kama ndani yetu hakuna Kristo.
*Anakwenda kutiwa au kukabidhiwa* (Kiyunani – paradidosthai). Anakaribia kukabidhiwa mikononi mwa wanadamu. Si tu kwamba atasilitiwa bali anakabidhiwa kwa makusudi yaliyomo katika mpango wa Mungu. Ni mpango wa Mungu unaotendeka kupitia mikono ya waovu. Yesu hasukumwi na mwanadamu bali anakabidhiwa kulingana na mpango wa Mungu wa wokovu (Isaya 53; Mdo 2:23). Ndio maana hili halikuweza kutendeka hadi wakati wa Mungu ulipotimia.
*Watamwua:* Hii inasisitiza kuwa tukio hilo ni la uhakika sio uwezekano. Hata kama Petro alijitahidi kusema, Hasha, hilo halikupati wewe alikuwa anapingana na mpango wa Mungu ambao ulikuwa lazima kwa vile hapakuwa na njia nyingine ya kuleta wokovu isipokuwa kupitia kifo cha Yesu, ndio maana alimwambia nenda nyuma yangu Shetani.
*Siku ya tatu atafufuka:* Mungu Baba ndiye aliyemfufua. Kufa na kufufuka kwa Yesu ndio msingi wa Imani yetu. Hata Kiri zetu za Imani ya Mitume na Nikea zinasimama katika Imani hiyo ya kwamba aliteswa, akafa na siku ya tatu alifufuka kutoka kwa wafu. Hata mahubiri ya Petro (Mdo 2; 3; 4) yalijengwa katika Habari za kufa na kufufuka kwa Yesu. Mtume Paulo katika 1 Korintho 15:3-4 kwamba alikufa na kufufa kama yaneyavyo maandiko (15:14) anaonesha kuwa bila kufa na kufufuka kwa Yesu, Imani yetu ni bure. Je, kanisa la leo mkazo wa mafundisho yake upo wapi? Ikiwa tutaacha kusisitiza haya, ni wazi kwamba tunajenga kwenye msingi usio sahihi.
*Wanafunzi wakasikitika sana au kupita kiasi:* Hawakuelewa ufufuo hadi Yesu alipokufa na kufufuka ndipo macho yao yalifumbuliwa. Walikuwa na uhusiano wa karibu na Yesu na wasijue hatima yake.

3. *YESU AIENDEA NJIA YA MATESO YERUSALEMU.*
Hii ni jumapili ya mwisho kabla ya majira ya Kwaresma (Quinquagesima). Kanisa linaanza kuelekeza macho toka utukufu Kwenda msalabani. Kutoka miujiza Kwenda mateso yaletayo ukombozi wa kudumu, wokovu kamili katika kifo na ufufuo wa Yesu. Jumapili hii ya mwisho ni lango la kuingia majira ya Kwaresma. Ni majira ya kuacha kutazama miujiza na kuanza kutazama msalaba. Ni wakati wa kutangaza kuwa injili ya wokovu ni ya neema katika Yesu Kristo kwa njia ya Imani. Kwa hiyo taarifa ya safari ya Yesu sio ya huzuni bali injili ya neema inaanza kufunguka na kujidhihirisha, tunaelekea utukufu wa juu kabisa wa Yesu. Lakini Yesu alitamka jambo ambalo wanafunzi hawakutaka kulisikia kabisa. Yesu anaenda kufa Yerusalemu! Mfalme au Masihi aende kufa.

Ndio hii ndio habari njema, Yesu anaenda mwenyewe, hakukimbia wala kujificha . Huu ndio upendo wa kweli. Alilipa gharama ya wokovu wetu kwa njia ya kifo chake msalabani. Hii inatukumbusha kuwa dhambi ni mbaya sana, hukumu ya Mungu ni ya kweli, lakini neema za Mungu ni kuu zaidi. Yesu anauendea msalaba sio kwamba hakuwa na hofu bali aliishinda hofu bali alikuwa anatii mapenzi ya Mungu, alijua thamani ya safari yake, kumwaga damu ili kumwokoa mwanadamu ambaye alimkosea Mungu akawa hana njia ya kujiosha mwenyewe, alihitaji neema, kulipiwa gharama.

Siku ya tatu atafufuka, tunasikia sauti ya pasaka ndani ya tangazo la kifo. Mateso sio mwisho wala kifo sio mwisho wa ushindi wa Yesu. Hii inatukumbusha sisi kuwa siku ya tatu ipo, huenda tunapitia mateso, maumivu, kukata tamaa Mungu ana siku ya tatu kwa ajili yetu.
Wanafunzi walisikitika kupita kiasi, waliona kama ni mwisho wa ufuasi wao walioutaabikia miaka 3, waliona msalaba bila ufufuo, hata kama walikuwa wamesikia akiusema. Kumbe kuna wakati tunaweza kusikia jambo, lakini tusielewa kabisa lina maanisha nini. Na mara nyingi tunakutana na mambo na hatuyaelewi yanamaanisha nini.

Tunapoingia majira ya Kwaresma tuutazame msalaba kama daraja la kutuvushia kwenye utukufu. Na kwa sababu peke yetu hatuwezi kuvuka, majira ya Kwaresma yanatuita kwenye unyenyekevu na toba. Ni majira yanayotuambia kuwa tuache dhambi ili tuupokee wokovu. Macho yetu yasibakie kwenye vitu tulivyo navyo sasa, bali yatazame kwenye matokeo ya utii ulioanzishwa na Yesu, na kisha ukaja kwetu. Kwaresma inatukumbusha kuwa Yesu alitii mapenzi ya Baba akawa sababu ya wokovu kwa wale watakaotii mapenzi ya Baba. Kipindi hiki cha Kwaresma kinatukomaza zaidi katika kutembea njia ya utii. Basi na tutembee pamoja na Yesu kwenye njia ya utii – kuna kusalitiwa (tena na watu wetu wa karibu), kuna kuteswa, na kuna kuuawa; lakini huo sio mwisho wa habari. Baada ya hayo yote, kuna utukufu na huo ndio utukufu wa kweli. Tukielekeza macho yetu kwenye utukufu huo, mapito na mateso ya wakati huu hayatatuzui kwa lolote. Mungu atujalie kutembea kwa ujasiri katika njia ya msalaba ambao Yesu anauendea.
Amen.