IBADA YA TAREHE 22 FEBRUARI 2026* SIKU YA BWANA YA 6 KABLA YA PASAKA (INVOCAVIT – MUNGU ANAITA NAMI NAITIKA)

SOMO:KATIKA YESU KILA JARIBU LINA MLANGO WA KUTOKA
ZABURI 139:11-16;
MATHAYO 4:1-11
*SOMO LA MAHUBIRI: DANIELI 3:19-23*
WIMBO: TMW 86
*UTANGULIZI*
Nebukadreza mfalme wa Babeli aliishinda Yerusalemu na kuwachukua watu mateka wakiwepo kutoka katika nyumba ya kifalme, huu ulikuwa wakati wa Mfalme Yehoyakimu wa Yuda, pia vyombo vya nyumba ya Bwana vilichukuliwa hadi Babeli. Hii ilikuwa hukumu ya Mungu kwa uasi wa ufalme wa Yuda. Kwa upande mwingine huu ulikuwa mwanzo wa mpango wa Mungu ndani ya uhamisho (Danieli 1:1-2). Mateso na majaribu hayamaanishi kwamba Mungu hayupo. Mfalme Nebukadreza akamwagiza Ashpenazi Mkuu wa matoashi amtafutie vijana wa Kiebrania wenye vinasaba vya kifalme, wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la kifalme. Ili wafundishwe lugha ya Wakaldayo, elimu ya kifalme, na utamaduni mpya. Vijana hawa wanne hata majina yao yalibadilishwa kama jaribio la kubadili utambulisho wao wa kiimani lakini ilishindikana walibaki na Imani yao (Danieli 1:3-7). Vijana hao ni: Danieli – Belteshaza Hanani – Shadraka Mishaeli – Meshaki Azaria – Abednego Hawa vijana walionesha msimamo usiokuwa wa kawaida walikataa kula chakula cha kifalme walichoagizwa walishwe miaka mitatu wao wakala mtama na maji na afya zao zikawa nzuri kuliko wale vijana waliokula chakula cha mfalme. Mungu aliwapa neema na hekima na mwisho wa siku walipoingizwa mbele ya mfalme kwa usaili walionekana kuwa bora mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake (Danieli 1:-20). Ilitokea kwamba mfalme aliota ndoto ambayo ilifadhaisha roho yake na usingizi kumwacha. Alitoa amri ya kuitwa kwa waganga, wachawi, wasihiri na wakaldayo ili watoe tafsiri ya ndoto ambayo alikuwa ameisahau. Wakaldayo wakajibu na kusema kuwa Hapana mtu duniani awezaye kulionesha neno hili la mfalme kwa maana Hapana mfalme wala bwana aliyetaka neno kama hili. Ni neno la ajabu analotaka mfalme, hakuna awezaye kumwonesha mfalme neno hilo ila miungu wasio na kikao Pamoja na mwenye mwili. Mfalme akakasirika mno akatoa amri ya kuua wenye hekima wote wa Babeli (Danieli 2:1-12). Wenye hekima wakawa wanatafuta kuuawa na Danieli na wenzake ambao hawakuwepo wakati wale wengine wanashindwa akawa anawatafuta Pamoja na wenzake ili wauawe. Danieli akamuuliza Arioko Akida wa walinzi wa mfalme aliyetumwa kuwaua, akasema, mbona amri ya mfalme inau kali hivi? Akaomba aingie kwa mfalme na akaomba apewe muda wa Kwenda kutafuta hiyo tafsiri. Danieli akawapasha Habari wenzake watatu kwamba waombe rehema na kupewa tafsiri au siri ya ile ndoto. Usiku Danieli akapewa ile ndoto ambayo mfalme aliota Pamoja na tafsiri yake. Mfalme Aliona sanamu kubwa. Kichwa cha dhahabu – Babeli (Ufalme wa Nebukadreza). Kifua na mikono yake ya fedha – Ufalme unaofuata. Tumbo na viuno vyake vya shaba – ufalme mwingine Miguu ya chuma nyayo zake nusu chuma na nusu udongo – Falme zinazogawanyika. Maana yake falme hizi ni za muda na dhaifu. Jiwe lililochongwa bila mikono, liliipiga sanamu miguu ikavunja vipande vipande huu ni ufalme wa Mungu wenye nguvu na utadumu milele (Danieli 2:13-45). Mfalme Nebukadreza akamtukuza Mungu akampa Danieli cheo cha kuwa mkuu juu ya Uliwali wote na mkuu wa wote wenye hekima wa Babeli na Danieli akawaombea nafasi wale wenzake watatu (Danieli 2:46-49). Tunapoanza na masilimulizi ya sura ya tatu inaonekana kuwa mfalme Nebukadreza aliazimia kupinga maelekezo ya Mungu ambayo yalitolewa na Danieli katika tafsiri ya ndoto. Aliamua kutengeneza sanamu ya dhahabu tupu kama kuashiria kuwa ufalme wake hautakoma kinyume na ujumbe wa ndoto. Nebukadreza aliamuru watu wote waabudu sanamu ile na kutofanya hivyo ilitafsiriwa kama kosa la uhaini (treason). Watu wote walitii isipokuwa watatu (Shadraka, Meshaki na Abednego). Kufuatia habari zilizopo sura ya pili, Danieli alipandishwa cheo na hivyo akawa anatumika ikulu, kwa hiyo hakujumuika nao. Huu ulikuwa mtihani wao na Danieli alipewa mtihani wake peke yake baadaye (Danieli 6). Inaonekana watu walikuwa wanawafuatilia wakagundua kuwa hawa jamaa wamegoma kuabudu sanamu, wakapeleka taarifa kwa mfalme Nebukadreza. Inaonekana kulikuwa na wivu wa kisiasa kwani hawa wageni walipewa nafasi za utawala. Nebukadreza hakutaka kuwachukulia hatua kwa maneno ya kusikia akawaita na kuwahoji. Je, ni kweli mmekataa kuabudu sanamu? Akawapa nafasi ya kufanya hivyo na kwamba wakikataa watatupwa kwenye tanuru la moto ili aone ni mungu yupi atakaye waokoa na mkono wake na pia na tanuru la moto. Na hapa ndipo alipokosea kumhusisha Mungu katika hoja zake. Wakamjibu kuwa hawakuwa na haja ya kujitetea, kosa wanalijua lakini Mungu wanayemtumikia atawaokoa na tanuru na mkono wa mfalme. Wakasema wazi kuwa hawakuwa tayari kutumikia miungu ya Nebukadreza wala kuabudu sanamu yake (Danieli 3:1-18). Ndipo linafuata somo letu la mahubiri (Danieli 3:19 -23). Mfalme Nebukadreza akastaajabu, akainuka haraka, akauliza kuwa je, hatukutupa watu watatu wakiwa wamefungwa? Mbona anaona watu wanne wamefunguliwa, wanatembea Katikati ya moto na hauna madhara na yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Akawaita Shadraka, Meshaki na Abednego kuwa ni watumishi wa Mungu aliye juu kuwa watoke nje. Nebukadreza akamhimidi Bwana na kuweka amri kwa kila kabila za watu, kila taifa na kila lugha kuwa yeyote atakaye nena neno lolote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, Meshaki na Abednego atakatwa vipande vipande na nyumba zao kufanywa jaa kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii. Kisha akawapandisha vyeo katika wilaya ya Babeli (Danieli 3:24-30). 2. *DANIELI 3:19-23 HASIRA YA MFALME NA MOTO MKALI DHIDI YA SHADRAKA, MESHAKI NA ABEDNEGO* Shadraka, Meshaki na Abednego walikataa kuabudu sanamu ya Mfalme Nebukadreza kwa sababu ya uaminifu wao kwa Mungu mmoja, aliye hai na ndiye pekee anapaswa kuabudiwa. Mfalme akawatisha juu ya uamuzi wao na kwamba angewachoma moto. Bado walikaza uamuzi wao na kutamka wazi kwamba moto hauna nguvu juu ya nguvu za Mungu. Mfalme kwa hasira akaamuru tanuru lichochewe mara saba kuliko kawaida. Hasira ya Nebukadreza inadhihirisha uasi wa mwanadamu dhidi ya Mungu. Hasira ya mfalme ilitokana na ushuhuda wa kishujaa uliotolewa na wale vijana watatu. Kabla hawajatoa msimamo wao mkali juu ya Imani yao katika Mungu aliye hai alikuwa akiwasemesha kama watoto wake. Hawakuona aibu kumshuhudia Mungu wao. Mfalme akatumia tanuru ambayo inasimama kama ishara ya hukumu, mateso, mauti. Kwa hakika tunaweza kuona kivuli cha msalaba katika tukio hili. Kwani hata Yesu alihukumiwa na mamlaka za dunia hii kama akina Shadraka, Meshaki na Abednego walivyohukumiwa. Baada ya moto huo mkali kuandaliwa walitafutwa vijana wenye nguvu, wakawafunga watumishi wa Mungu na kuwatupa katika tanuru la moto, wale waliowabeba Shadraka, Meshaki na Abednego moto uliwalamba wenyewe wakafa. Mle ndani wakaonekana akina Shadraka, Meshaki na Abednego wakiwa huru hawajafungwa tena. Mfalme alishangaa mno kwani halikuwa tukio la kawaida. Katika tafsiri ya toleo la Septuagint inasema, mfalme alishituka kusikia wale vijana wanne wakiimba nyimbo za sifa ndani ya tanuru. Moto ulikula Kamba zilizowafunga lakini haukugusa nguo zao wala nywele wala hata harufu tu ya moto hawakuwa nayo. Mle ndani akina Shadraka, Meshaki na Abednego hawakuwa peke yao walikuwa na mtu wa nne aliyeonekana kuwa ni mwana wa Mungu. Kumbe Yesu aliingia nao katika tanuru. Sio lazima Mungu akaepushe na majaribu au mateso wakati mwingine anakwenda na wewe, usiogope hupo peke yako. Hatuna uhakika kama akina Shadraka, Meshaki na Abednego walijua kuwa wapo Pamoja na Yesu mle ndani ya tanuru ya moto. Kwa hiyo tuwe tunaona au hatuoni Yesu yupo Pamoja nasi. Mfuasi wa Kristo pia ana tanuru za aina mbali mbali ambazo anakutana nazo katika maisha. Kuna tanuru ambazo mtu mwenyewe anajitengenezea, zipo ambazo zinatengenezwa na Shetani na nyingi zinaandaliwa na Mungu. Kwa hiyo Mungu anaweza kutuokoa kutoka katika majaribu au akatuwezesha kubeba au kushinda jaribu hilo.
3.*KATIKA YESU KILA JARIBU LINA MLANGO WA KUTOKA*
Habari za vijana wanne Danieli, Shadraka,Meshaki na Abednego zinatuonesha kuwa vijana hawa walikuwa Hodari na wenye ufanisi mkubwa tangu kuitwa kwao. Ufanisi wao haukuwa kwa sababu ya elimu tu wala nafasi zao nzuri serikalini bali ulitokana na msingi wa kiroho ambao uliongoza maisha yao yote. Ushindi wao juu ya majaribu haukupatikana katika siku moja bali ulishuhudia aina ya watu walivyo na jinsi walivyoishi na Mungu. (a) Walikuwa wameandaliwa toka nyumbani na mfalme alitafuta watu wenye sifa. (b) Walikuwa na uamuzi moyoni juu ya kumtii Mungu. Danieli na wenzake waliazimia moyoni kutojitia unajisi na vyakula vya mfalme hata kama vilionekana kuwa vyenye sifa wao wakala mtama na kunywa maji (Danieli 1:8). Kwa hiyo mafanikio yao yalianza moyoni kwa uhusiano sahihi na wauaminifu na Mungu. (c) Walidumisha maisha ya utakatifu na hofu ya Mungu Katikati ya maisha ya kipagani. Shadraka, Meshaki na Abednego waliposhurutishwa kusujudia sanamu walikataa hata walipotishwa na tanuru la moto. Walichagua kuwa waaminifu kwa Mungu na kuuacha usalama wa maisha yao mikononi mwa Mungu (Danieli 3). (d) Walikuwa watu wa maombi na kumtegemea Mungu kila siku. Maisha ya ushindi hayaanzi na mbinu bali na uhusiano. Danieli alipata ushindi kwa sababu aliishi mbele za Mungu kila siku (Danieli 6:10). Danieli hakuanza kuomba baada ya tishio bali aliomba kama ilivyokuwa desturi yake na akaendelea hata baada ya amri ya kutokuomba kutangazwa. Hatuanzi kuomba baada ya kuingia majaribuni tunahitaji kuishi maisha ya maombi. (e) Mungu alisimama upande wao. Moto haukuwaunguza (Danieli 3) na simba hawakumwangamiza Danieli (Danieli 6). Mungu hatuzuii tusipitie majaribu bali anapita nasi katika majaribu. Alienda na akina Shadraka ndani ya tanuru la moto, alienda na Danieli ndani ya tundu la simba na kuwafumba vinywa vyao. Mungu hakungoji nje bali anaenda Pamoja nawe. Majaribu ni njia ya kuuendea ushindi. Ndio maana wapo ambao hufika kwenye ushindi na wengine hurudia njiani. (f) Walitumia ujuzi na karama zao kwa utukufu wa Mungu. Hawa vijana wanne walikuwa na hekima, maarifa na nafasi za juu katika serikali kule Babeli lakini walielekeza utukufu kwa Mungu sio kwao. Katika somo letu tunajifunza kuwa Kristo yupo na watu wake katika moto. Yesu hatuokoi akiwa mbali kama mtazamaji bali anaingia katika mateso, anaingia mwenyewe katika tanuru la moto uliokolezwa mara saba. Majira haya tumeanza safari ya Kwaresma tangu jumatano ya majivu (18/02/2026), ni majira ya kutafakari mateso ya Bwana Yesu, kutubu dhambi na kujifunza juu ya tumaini la msalaba. Neno letu limetupeleka Babeli kwenye tanuru la moto ambako vijana wale watatu walikataa kusujudia sanamu, wala miungu ya Wakaldayo. Walikuwa tayari kupitia mateso hata kifo kwa ajili ya Imani yao. Kipindi hiki cha kwaresma tunamwona yule Yesu ambaye alikuwa na wale vijana ndani ya tanuru la moto, anauendea msalaba kwa ajili ya ukombozi wetu wanadamu. Kuonekana kwake ndani ya tanuru ulikuwa udhihirisho wa Yesu kabla hajazaliwa katika mwili. Uwepo wa Yesu ndani ya tanuru la moto ni ujumbe kwamba Mungu hayuko mbali na mateso ya watu wake. Haangalii toka toka mbinguni bali alifanyika mwili na kupita nasi katika mateso. Mungu anaingia ndani ya moto wa dhambi ambazo zilitutesa, hii ndio injili ya Kwaresma, ukombozi kwa njia ya msalaba. Pamoja na Yesu ndani ya tanuru akina Shadraka walikuwa huru wakitembea, hawajafungwa na wala hawakuungua. Moto upo lakini hauwezi kutuangamiza, kifo kipo lakini Yesu ni mshindi w amauti, mateso yapo lakini sio mwisho kwa sababu Yesu yumo ndani ya moto Pamoja nasi. Ujumbe wa msalaba unasema, Yesu huokoa si kwa kuondoa mateso kwanza, bali kwa kuwa Pamoja nasi ndani yake. Tukiangalia masomo yetu yote matatu tuliyopewa katika kalenda Zaburi 139:11-16; Mathayo 4:1-11 na Danieli 3:19-23 yote yanatutaka tuelekeze macho yetu kwenye siri ya ushindi wa Mungu Katikati ya giza, majaribu na moto. *Zaburi 139:11-16* Mungu alimwona Daudi na kumuandaa kabla ya vita. Hakuna giza linaloweza kumficha mtu mbele za Mungu. Mungu alimuumba mtu kwa jinsi ya ajabu tangu tumboni na kupanga siku zake zote. Kabla ya jaribu halijaja Mungu tayari anajua na ameandaa ushindi. Tumeumbwa kwa jinsi ya ajabu kiasi kwamba maarifa hayo hatuwezi kuyafikia na kuyaelewa. Kwa hiyo kwa kufuata Zaburi yetu hatuingii vitani, majaribuni peke yetu bali tunaingia tukiwa tunajulikana na Mungu. Mungu hutuandalia mlango wa kutoka kabla hatujaingia. Yeye hutangaza mwisho tangu mwanzo (Isaya 46:10). *Mathayo 4:1-11.* Yesu anajaribiwa jangwani, tena alipelekwa na Roho Mtakatifu. Alipata majaribu matatu: Jaribu la mwili, mkate; jaribu la kujionesha aruke kutoka hekaluni na jaribu la mamlaka na umiliki bila msalaba. Yesu alichukua mamlaka kwa njia ya msalaba na kumiliki vyote (Waefeso 1:18-23). Katika majaribu hayo yote Yesu alishinda kwa Neno la Mungu kila mara akisema, Imeandikwa … Kama Yesu alishinda kwa neno, na sisi hatuwezi kushinda kwa nguvu zetu bali kwa Neno ambalo pia ni Yesu mwenyewe. Katika somo la Danieli *(Danieli 3:19-23)* tumeona wale vijana wakiwa na mtu wa nne ndani ya moto. Mungu haji kabla ya jaribu, huingia ndani ya jaribu Pamoja nasi. Kumbe moto ambao ulipanga kutuangamiza unageuka kuwa mahali pa ufunuo wa uwepo wa Mungu na mahali pa Mungu kutukuzwa na kuabudiwa na watu wote.
Uwe na Kwaresma nje