All posts by Evangelist John(Charles)

Usharika wa uwemba wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania dayosis ya kusini karibu mbarikiwe pamoja nasi

MAHUBIRI YA SIKU YA ALHAMISI YA KUKUMBUKA KUPAA KWA YESU KRISTO TAREHE 21/05/2020

KKKT DAYOSISI YA KUSINI, JIMBO LA KUSINI, NJOMBE MJINI,USHARIKA WA UWEMBA
MTAA WA MJIMWEMA luponde.

Masomo:
ZABURI 47:1 – 9,
EBRANIA 8:1 – 5,
*LUKA 24: 50 – 53.

MADA: KRISTO AMEPAA KATIKA UTUKUFU WAKE.

SHABAHA: Wasikilizaji watambue kuwa Mungu hupenda kutuona na furaha hivyo wazidi kumwamini ili aachilie Baraka zake kwao.

UTANGULIZI
 Leo ni siku muhimu sana kwa kanisa na kwa ukombozi wa mwanadamu kwani tunakumbuka Yesu baada ya kumaliza safari ngumu ya kutukomboa sasa anarudi kwa baba yake ili kuanza maandalizi ya makao yetu ya milele.

 Somo ambalo tumelisoma leo kutoka katika injili ya Luka linaelezea tukio la Yesu kunyakuliwa mbele ya wanafunzi wake kwenda mbinguni ambapo katika somo hili tunajifunza mambo mengi na leo naomba tuangalie haya machache.

1. MPANGO WA MUNGU KWETU WAKATI WOTE NI KUTUBARIKI
 Wanafunzi wa Yesu wakiwa wameshuhudia matendo mengi aliyoyatenda Yesu kabla ya kuteswa na kuuwawa na hata baada ya kufufuka wameshuhudia Baraka nyingi na ulinzi katika maisha yao, na sasa Yesu anawaacha anaondoka kwenda mbinguni lakini hata katika kuondoka kwake anaendelea kuwabariki wanafunzi wake.

 Tunaona wazi kuwa mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu ni kumbariki wakati wote hata ikiwa ni wakati wa dhiki, mateso, mahangaiko na hata wakati wa furaha kwa sababu hiyo tunapaswa kuweka tumaini letu kwake pasipo kuyumba wala kuyumbishwa.

2. BARAKA ZA MUNGU ZITUPELEKEE SISI KUMWABUDU WAKATI WOTE
 Wakati Yesu anaendelea kuwabariki wanafunzi wake na wakielewa wazi kuwa wanapokea Baraka, Baraka zile ziliwapelekea wao kumwabudu.

 Je, ulishawahi kubarikiwa? Baraka za Mungu ziliposhuka katika maisha yako wewe umefanya nini? Wanafunzi wanatuonyesha mfano mzuri kuwa Baraka za Mungu zinatutaka sisi kumwabudu wakati wote.

 Wapo ambao wanabarikiwa lakini hawaonekani katika kumwabudu Mungu si katika nyumba za ibada wala katika sala zetu za jumuiya. Hiyo ni kusema kuwa Mungu sizihitaji Baraka zako. Mungu atusaidie ili na sisi tusikiri hivyo. Hongereni ninyi mliohudhuria ibada ya leo.

3. BARAKA ZA MUNGU HULETA FURAHA MAISHANI
 Wanafunzi walipobarikiwa japokuwa walikuwa na huzuni ya Yesu kuondoka katikati yao Baraka zile ziliwafanya waelekee Yerusalemu kwa furaha.

 Wakati mwingine maisha yanaweza kuwa na huzuni ila huzuni hiyo isikuondoe katika furaha yako katika Yesu Kristo. Kumbuka mambo mema na Baraka za Mungu katika maisha yako ili uweze kuitunza furaha yako.

4. TUONYESHE FURAHA YETU YA KUPOKEA BARAKA ZA MUNGU KWA KUMSIFU DAIMA
 Tunaambiwa kuwa wanafunzi wa Yesu walidumu wakimsifu Mungu ndani ya Hekalu wakati wote.

 Katika hili tunaona jambo hili la kumuabudu Mungu linajitokeza mara mbili kuonyesha umuhimu wake na sasa anasema hekaluni. Wapo ambao wanasema kuwa wanamsifu Mungu wakiwa nyumbani kwao, ama wanaangalia video au wanasikiliza redio, sisemi kuwa hilo ni baya ila kama unazo nguvu na afya usiache kuhudhuria ibada kumwabudu na kumsifu Mungu wetu.

HITIMISHO
Mungu aliye na mpango mwema wa kutubariki wakati wote ili tudumu katika furaha basi tusiache kumsifu na Kumuabudu katika maisha yetu yote.

AMEN
Ev.John

MAHUBIRI YA SIKU YA 5 BAADA YA PASAKA TAREHE 17/05/2020 IITWAYO ROGATE MAANA YAKE OMBENI.

KKKT DAYOSISI YA KUSINI, JIMBO LA NJOMBE MJINI, USHARIKA WA UWEMBA, MTAA WA LUSITU.

MAHUBIRI YA SIKU YA 5 BAADA YA PASAKA TAREHE 17/05/2020 IITWAYO ROGATE MAANA YAKE OMBENI.

MASOMO: ZABURI 107:1 – 8, MARKO 10:46 – 52, *MATENDO YA MITUME 12:5 – 17

MADA: OMBENI KATIKA JINA LA YESU KRISTO

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kutambua kuwa wakiomba kwa Jina la Yesu Hakika watapokea majibu yao hivyo waelekeze maombi yao kwake.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, Jumapili ya leo tunajifunza juu ya kuomba kwa kutumia Jina la Yesu Kristo ambalo ndio msaada wetu wakati wote( Wafilipi 2: 9 – 11)

Kwa kuutazama ukweli huu tumepewa kujifunza kutoka kitabu cha maendo ya Mitume 12: 5 – 17 ambapo tunapata habari za Petro kufungwa gerezani na Kanisa linakutana vikundi vikundi na kumuomba Mungu anayeleta msaada wa kweli kwa kanisa na kwa Petro mwenyewe.

Katika habari hii tunaweza kujifunza haya yafuatayo:-

1. KATIKATI YA NDORUBA UKIWA MIKONONI MWA MUNGU ANAKUPA AMANI
 Hapa tunaona jinsi ambavyo Petro akiwa amefungwa gerezani katikati ya ulinzi Mkubwa, amefungwa minyororo kwenye miguu na kikono tena kwenye chumba cha ndani na siku chache zilizopita rafiki yake na mtumishi mwenzake Yakobo ndugu yake Yohana aliuwawa lakini yeye anapata Usingizi tena tunaambiwa alilala fofofo.

Usingizi una mafundisho mengi na siku ya leo tujifunze moja juu ya Usingizi

 Wakati wa matatizo, shida na dhiki ni vigumu sana kupata Usingizi ( Esta 6:1,Ayu 3:13)

 Mungu anaporuhusu Usingizi kwa mtu wake anataka kuleta mwanzo mpya (Mwa 2:21, 28:16,)

 Katikati ya dhoruba Mungu humpa rafiki yake Usingizi akitaka atulie na kuwa na amani tayari kupokea Baraka. (Zab 3:5,127:2)

 Kwa maelezo hayo unaona jinsi ilivyokuwa vigumu Petro kupata Usingizi ila kwa ajili Petro alijua kuwa maono yay eye kulijenga kanisa hayajakamilika na aliahidiwa na Mungu kuwa atalala akiwa mzee.

 Maisha yetu yamejaa dhoruba nyingi, mateso mengi na mahangaiko ila bado Mungu anabaki kuwa Mungu kwetu, ukiangalia hasa katika kipindi hiki cha Ugonjwa huu waCOVID – 19 mahangaiko ni mengi kila mahali ila tusiache kuelekeza imani yetu kwa Mungu yeye atatupa amani na matulizo ya kweli a Ushindi wa kutosha

2. MUNGU ANAPOANZA KUTENDA HUTENDA ZAIDI YA ULIYOTAZAMIA NA KUKUACHA KWENYE MSHANGAO
 Mungu anapofanya ukombozi katika maisha yetu sio kwamba anatushangaza sisi wenyewe bali hata wale waliotuzunguka wanabaki kushangaa.

 Wakati Petro amelala Mungu ameruhusu kanisa kuomba kwa ajili ya Petro na Petro anapookolewa anashangaa na kanisa lililokuwa linamuombea nalo linashangaa wote Petro na Kanisa wanapoona ukuu wa Mungu wanafikiria ni ndoto kumbe ni Mungu yupo kazini.

 Yapo mambo ambayo tunaona kuwa hayawezekani kabisa ila tukiingia kwenye maombi yanawezekana kwa kiwango ambacho hata sisi wenyewe hatuwezi kuamini ila ukweli unabaki kuwa Mungu ni mwaminifu kwetu na hataacha kututendea mazuri wakati wote tunapoelekeza tumaini letu kwake.

*3. MAOMBI HUFANYA YOTE YAWEZEKANE*
 Shetani anapokupata anahakikisha kuwa anafunga kila njia ambayo anaona inaweza kukusaidia kunusurika katika mikono yake. Tunaona Jinsi ambavyo Petro alivyokamatwa na kufungwa chumba cha ndani na hiyo ikawa haitoshi wakamfunga kwa minyororo na hiyo ikiwa bado haitoshi wakamuwekea na walinzi ila Kanisa linapoomba hakuna kifungo kinachozua Petro kuwa huru tena uhuru ulioleta uhai kwa kanisa.

 Kanisa tusichoke kuomba katika nyakati zote hata pale kwa akili zetu za kibinadamu tunapoona mambo hayawezekani ila kwa Mungu yanawezekana sana. OMBA, OMBA OMBA NA USICHOKE KUOMBA HADI HAPO MUNGU ATAKAPOJIBU MAOMBI YOTE SABABU HAKIKA ATAYAJIBU.

HITIMISHO
Mungu aliyemtoa mwanae wa pekee tuendelee kumtegemea tukilitaja jina lake ambalo kwa hilo tunapokea majibu yetu.
AMEN.

10/05/2020 KANTANTE DOMINION-MWIMBIENI BWANA WIMBO MPYA

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 4 BAADA YA PASAKA TAREHE 10/05/2020

MADA: MWIMBIENI BWANA WIMBO MPYA

MASOMO: ZABURI 100: 1 – 6, UFUNUO 15: 1 – 4, *ZABURI 69: 29 – 36

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa aina ya maisha wanayoishi haiondoi uwezo wa Mungu katika kuwaokoa wazidi kumtegemea.

UTANGULIZI
 Bwana Yesu asifiwe, Leo ni jumapili ambayo kila mtu awe mwenyewe, au katika familia, au katika kundi kwa pamoja tunaalikwa kumuimbia Mungu wimbo mpya.

 Upya wa wimbo sio maneno mapya yaliyotungwa katika umahiri wa kisanii bali ni moyo unaomaanisha kile unachokitamka katika hali unayopitia kwa matumaini makubwa kuwa Mungu atafanya.

 Katika kutafakari mada hii tunatafakari neno la Mungu kutoka kitabu cha Zaburi 69: 29 – 36 ambapo tunamuona muimba zaburi akitambua hali ya uhitaji na umsikini alionao ila haimzuii kuamini kuwa Mungu atamponya yeye, na wote wanaomtegemea na sio wanaomtegemea tu hata taifa lake litaokolewa hivyo ataendelea kuimba nyimbo za furaha ya matumaini na kumshukuru Mungu kwa wokovu aliompatia yeye, ndugu, jamaa na marafiki zake na hata taifa lake.

Katika kisa hiki tunajifunza mambo makuu yafuatayo:-

1. MUNGU HUBAKI KUWA MUNGU BILA KUJALI CHOCHOTE UNACHOPITIA
 Wakati mwingine katika maisha hufikiri kuwa tunapopitia katika hali zinazosababisha maumivu, wasiwasi na uhitaji labda Mungu ametuacha na hata watu wengine hujitahidi kuficha hali wanayopitia ila ukweli unabaki kuwa Mungu habadilishwi na hali unayoipitia bado anabaki kuwa Mungu.

 Mwimbaji wa Zaburi analionyesha hilo kuwa japokuwa ni maskini mhitaji mwenye wasiwasi na maumivu makali ambayo hakustahili ila hayupo tayari kutafuta msaada kwa mtu au kitu kingine chochote zaidi ya kumtafuta Mungu sababu ana uhakika kuwa kitakachomuokoa na kumuinua tena ni WOKOVU WA MUNGU PEKE YAKE

 Moyo wenye shukrani juu ya wokovu huu utajidhihirisha kwenye kumsifu Mungu (Moyo wenye shukrani wakati wote una wimbo wa kumtukuza Mungu.)

 Huduma za kiroho kama vile kumsifu Mungu(Kuimba nyimbo mbalimbali), Kumuabudu Mungu, kumuomba Mungu vina umuhimu zaidi ya sadaka.

2. MAISHA YA SIFA YANAIMARISHA IMANI ZA WAAMINIFU WANAOPITA KATIKA KIPINDI CHA MATESO
 Maisha ya kumsifu Mungu sio kwamba yanakuimarisha wewe peke yako na kukupatia wokovu bali wote amabo wanatazama jinsi Mungu anavyokuokoa nao wataimarika imani zao.

 Mungu ataweka tofauti kati ya watu wanaomtegemea na wale wasiomtegemea kwani yeye ni Mungu:-

a) Anayeleta furaha kwa wote wanaoonewa,

b) Hufufua mioyo iliyokata tamaa na matumaini,

c) Husikiliza maombi ya wahitaji wote,

d) Huwafungua wafungwa wote.

 Katika kipindi hiki tunachopitia changamoto ya ugonjwa huu wa COVID 19 na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu tubadili namna ya kukabiliana nao sio kila siku kupokea habari mbaya tu. Sasa tuelewe kwamba ugonjwa upo na unaua tena kwa haraka hivyo tuchukue tahadhari na tuendelee kumsifu Mungu. Niliona wakati Raisi wetu anaposema tuombe nchi nyingi zilimbeza sana ila sasa nimeanza kuziona nazo zinafuata utaratibu huu wa maombi.

 Maombi yameondoa hofu kwa watanzania na sasa imeanza kuambukiza na nchi nyingine kuwasaidia watu wake kuondoa wasiwasi. Sisi tuongeze bidii kumuomba Mungu na kumsifu daima.

3. MUNGU MWENYE UWEZO WA KUOKOA MTU MMOJA ANAO UWEZO WA KUOKOA TAIFA.
 Kama watu mbalimbali wanamsifu na kumuabudu Mungu na wokovu unatokea katika maisha yao, basi uwezo huo pai unaweza kutenda kazi katika taifa. Tunapoona taifa linataka kuanguka au tayari limeshaanguka tukimuita Mungu wetu kwa kweli atatusikia na kuliokoa taifa letu.

 Muimba zaburi anaeleza kuwa Mungu ataliokoa taifa la Yuda na watu watakaa na kumiliki, wale wanaomtumaini Mungu watarithi na wote wanao mtumaini hakika watakaa katika miji iliyookolewa.

 Wale kweli ambao wataelekeza tumaini lao kwa Mungu katika hali zote ni kweli nchi itaokolewa na watu watabaki hai kwa ajili ya kuishi wakimsifu Mungu.

HITIMISHO
Mungu hawezi kugeuzwa na hali yoyote ya kibinadamu bali wote wanaomtumainia hakika wataokolewa wao pamoja na familia zao na nchi yao.

AMEN.

03/05/2020 JUBILATE – MPIGIENI BWANA KELELE ZA SHANGWE MADA: MAISHA MAPYA NDANI YA KRISTO YESU

KKKT DAYOSISI YA KUSINI,JIMBO LA NJOMBE, USHARIKA WA UWEMBA,
MTAA WA MJIMWEMA

MAHUBIRI YA SIKU YA BWANA YA 3 BAADA YA PASAKA TAREHE 03/05/2020

JUBILATE – MPIGIENI BWANA KELELE ZA SHANGWE

MADA: MAISHA MAPYA NDANI YA KRISTO YESU

MASOMO: ZABURI 107: 25 – 32, MATHAYO 9:14 – 17, *ISAYA 25: 1 – 8

SHABAHA: Wasikilizaji waweze kuelewa kuwa Ndani ya Yesu yanapatikana maisha ya ushindi hivyo wamtegemee daima.

UTANGULIZI
Bwana Yesu asifiwe, Jumapili ya leo tunajifunza juu ya maisha mapya ndani ya Kristo Yesu. Kwa tafsiri yangu juu ya mada hii ni kuwa yapo Maisha ndani ya Yesu ambayo kila mmoja hapa anayo na pia kuna maisha mapya ndani ya Yesu Kristo ambayo baadhi yetu tunayo maisha hayo.

Naweza kusema Maisha ndani ya Yesu Kristo ni maisha yale ya mazoea ambayo unatambua kuwa Yesu yupo, na umesikia akitenda mambo ya ajabu lakini hilo halikuzuii wewe kutenda kwa kiburi, dharau na majivuno.

Na Maisha mapya ndani ya Yesu Kristo ni maisha yenye mabadiliko, maisha yanayomtegemea Mungu na kuziona nguvu zake zikitenda kazi. Yaani ni maisha yenye mafanikio yanayotambua kuwa Mungu ameahidi kutufundisha ili tuweze kupata faida. (Isaya 48:17)

Katika kusindikiza mada tuliyopewa leo ya Maisha Mapya ndani ya Kristo Yesu tumepewa neno la Mungu kutoka Isaya 25: 1 -8 ambapo tunajifunza mambo kadhaa ambayo ni:-

1. LENGO LA MUNGU KURUHUSU ADHABU KATIKA MAISHA YETU NI ILI TUKUMBUKE UWEPO WAKE NA KUMUABUDU.
Kama nilivyoeleza kwenye utangulizi kuwa maisha ndani ya Mungu ni maisha ya mazoea, sasa Mungu anapotaka kuondoa haya mazoea anaruhusu adhabu kidogo ili tuweze kumkumbuka na tumsifu.

Isaya hapa anazungunza katika wimbo wake wa shukrani kuwa Mungu ameviharibu vitu ambavyo wanadamu walivijenga kwa kiburi chao na uwezo wao, maisha yamekuwa ni uchungu mtupu na miji ya kifahari imekuwa magofu hakuna wakaaji kabisa na kwa hilo mataifa watishao wataogopa lakini lengo lake lipo kwenye ule mstari wa tatu ambalo ni ili watu walio hodari katika hali hii wabaki wakimtukuza Mungu.

Kipindi hiki ambacho tunapitia hatari hii ugonjwa huu wa Corona ni kipindi ambacho tunaona kweli maisha yamekuwa machungu, miji mikubwa inabaki kuwa magofu watu wake wanakufa kweli na hata kwetu na mataifa makubwa yanayotisha yannaogopa sana sitaki kusema hili ni pigo kutoka kwa Mungu ili tumrudie ila nasema kwa kupitia hili watu wengi wamemrudia Mungu na wale walio hodari hata katika shida hii hawataacha kumtukuza Mungu.

2. MAISHA MAPYA NDANI YA YESU KRISTO NI MAISHA YA MABADILIKO
Maisha mapya ndani ya Kristo Yesu ni maisha ambayo yanashuhudia mabadiliko kila siku ni maisha ambayo mtu anashuhudia nguvu za Mungu na kuzikiri kweli kweli.

Neno la Mungu katika Isaya linaonyesha wazi kuwa ni maisha ambayo yanatoa nafuu kwa wote wanaoteswa ( ni ngome kwa maskini mhitaji katika dhiki yake, mahali pa kukimbilia wakati tufani) kuwanyamazisha watesi wote wanaojishughulisha na maisha ya watu wa Mungu.(Wale wanaoshangilia kwa kututesa sababu wanaona wameshinda hakika watashushwa)

3. MABADILIKO YA KWELI YANALETA FURAHA KWA MUNGU INAYOLETA MAFANIKIO KATIKA MAISHA YETU
Kama nilivyoeleza tangu awali kuwa maisha mapya ndani ya Kristo Yesu ni maisha yanyoleta mabadiliko na mabadiliko hayo yanapokuwa ya kweli yanaleta mafanikio katika maisha yetu.

Neno la Mungu katika Isaya linaeleza wazi kuwa Mungu atafanya sherehe na wote wanaomtegemea na katika sherehe hiyo Mungu atafanya mambo kadhaa ambayo ni:-

a) Atawaharibu maadui zetu wote

b) Atafuta machozi yote

c) Ataondoa huzuni tote

d) Ataiondoa aibu yote iliyotukabili

e) Ataondoa kifo hata Milele.

Kipindi hiki tumeitwa sana katika kutubu ili Mungu atuondolee ugonjwa huu wa Covid-19 na tukihimizana kurejea kitabu cha Mambo ya Nyakati wa pili 7:14. Ukweli unabaki kuwa toba inahitaji mabadiliko ya kwelikweli ili mabadiliko hayo yaweze kutuondolea adui yetu huyu, kutufuta machozi, kutuondolea huzuni na hata aibu ambayo inaonekana kwetu kwa sababu tumeruhusu ibada kuendelea.

Mabadiliko ya kweli ya rohoni na mwilini. Mwilini tukifuata ushauri wa wataalamu kukabiliana na adui huyu mkubwa kwa sasa Covid -19 kama vile kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa, kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, kutokuwa na safari zisizokuwa na sababu ya msingi nk
Rohoni tukiendelea kumuomba Mungu kwa nguvu zetu zote na uwezo aliotujalia, tukitubu na kumkataa shetani na kazi zake zote na mambo yake yote.

HITIMISHO
Tuendelee kumtegemea Mungu na kumtumikia kwa uaminifu na hakika upya wa maisha yetu ndani ya Yesu Kristo utaonekana kwa mafanikio.
AMEN.
@Evjohn
0768386606

ASKOFU SHOO,MUNGA NA MALASUSA WATOA NENO JUU YA COVID19

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo pamoja na Maaskofu Dk. Alex Malasusa na Stephen Munga
wametoa maagizo kwa washarika katika kuukabili ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Dayosisi wanazoziongoza Maaskofu hao pia wameagiza Wakristo kuoba kwa bidii juu ya ugonjwa huo.

Mkuu wa Kanisa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, aliesme kuwa pamoja na yote yanayoendela kamwe Kanisa hilo halitaacha kumuabudu Mungu.

“Naomba ifahamike kuwa, pamoja na yote endapo ugonjwa huu utaendelea japo siyo ombi letu, tupo tayari kufanya mabadiliko ya taratibu zetu za Ibada lakini hatutuacha kumwabudu Mungu,” alisema Askofu Dk. Shoo.

Akihubiri kwenye Ibada ya kumuingiza kazini Mkuu mpya wa jimbo la Hai, Mch. Biniel Mallyo Askofu Dk. Shoo alisema kuwa huu ni wakati wa kumkaribia Mungu, kwa kuwa inaonekana kwa nguvu na akili za kibinadamu, hatuwezi zaidi ya kimkimbilia yeye.

“Niwasihi kila mmoja wetu kuacha hofu na tung’ang’ane kwa kufanya maombi ya toba kwa Mungu wetu,” alisema Askofu Dk. Shoo.

Mkuu huyo wa Kanisa aliwapa matumaini Watanzania, akieleza kuwa ugonjwa huo utapita maana Mungu amesema atatulinda dhidi ya mauti na magonjwa.

Aliwasihi Wakristo kuwaombea watumishi wa sekta ya afya ili wasiathirike pindi wanapotoa huduma kwa wale waliothibitika kuugua ugonjwa huo.

Aidha Askofu Shoo alisema Kanisa hilo litafanya maombi maalum yanayofanana ili kumsihi Mungu aliepushe Taifa na ongezeko la virusi vya corona na katika Ibada hiyo makundi mbalimbali yalifanya maombi maalumu ya kuomba toba kwa Mungu.

MUNGA ATAKA MAOMBI YA KUFUNGA

Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (DKMs), Dk. Stephen Munga ameandika waraka maalumu ambao umesambazwa kwenye Sharika zote za Dayosisi hiyo, juu ya hatua za kuchukua kuhusiana na ugonjwa huo unaotajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa ni janga la dunia.

“Ninaandika waka huu kwenu nikijua kwamba ulimwengu kwa ujumla na Taifa letu linapita katika kipindi kigumu cha mapambano dhidi ya gonjwa la COVID 19,” alisema Askofu Dk. Munga kupitia waraka huo.

Kupitia waraka huo, Askofu Dk. Munga alinukuu maneno ya Mungu kutoka kitabu cha Yeremia 17: 14 unaosema; “Uniponye ee Bwana nami nitaponyeka, uniokoe nami nitaokoka kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.”

Aidha Mkuu huyo wa DKMs alionya juu ya watu wanaopuuza ugonjwa huo na kuwatahadharisha kuwa makini na manabii wa uongo wanaotaka waone kuwa ugonjwa huo siyo kitu. “Ieleweke kwamba tunashughulika na janga.”

Alitoa wito wa maombi kwa wanakanisa na kutubu katika kipindi hichi cha kwaresma.

“Nawaalika wana DKMs kuungana na watakatifu wengine hapa Tanzania na duniani katika kuomba na kufunga,” ulisema waraka wa Askofu na kuongeza;

“ Tena kwa sababu tumo katika kipindi cha Kwaresima hembu tukumbushwe kuingia ndani zaidi katika roho ya toba.

Tumuombe Mungu msamaha wa dhambi zetu, msamaha wa dhambi za Taifa letu na dhambi ya ukengeufu wa ulimwengu wa kumuacha Mungu na kujivunia maarifa na nguvu za wanadamu,” iliongeza sehemu ya waraka huo wa Askofu Dk. Munga.

Askofu Munga alisema kuwa maombi hayo yafanyike katika siku zote zilizobaki za majira ya Kwaresma ba kuhitimishwa katika siku ya pili ya Pasaka.

MALAUSA: TOMBE KWA ROHO, TUOMBE KWA AKILI

Naye Askofu Dk. Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliwaambia washarika wa Dayosisi hiyo kuwa ni lazima wajitunze kwa kuzingatia wataalamu wa afya wanavyosema.

“Tusisubiri viongozi wa serikali ndiyo watuambie namna ya kutunza hekalu la Bwana, sisi ni lazima tutunze usafi wetu, kwa hiyo tunapoambiwa kunawa, tusisalimiane hayo ni mambo ambayo sisi tunatakiwa tuwe mstari wa mbele na kuwa mabalozi wa kuyafanya hayo.

“Tunaposema kuwa tunapunguza makusanyiko ya katikati ya wiki siyo kwamba hatutaki Ibada, lakini kwa sababu ya hali halisi ilivyo imebidi tusimame kidogo si kwamba hatuzipendi na si kwamba hatutaki kumuabudu Mungu lakini tuombe kwa roho na tuombe kwa akili,” alisema Askofu Dk. Malasusa.

Mkuu wa DMP alisema ni wakati wa kuomba kwa roho na akili na pale hali itakapokuwa njema watu wataendelea kukutana.

RAIS WA WALUTHERI ATOA NENO

Corona ambayo imetikisa dunia pia imefanya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (FMKD-LWF) nalo kuandika barua maalumu kwa makanisa yake wanachama duniani kote kusisitiza jambo hilo la maombi.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Rais wa Fungamano hilo Askofu Mkuu Dk. Filibus Musa na Katibu Mkuu Dk. Martin Junge FMKD imewataka wanachama wake kusimamia mstari wa kitabu cha 2Tim 1:2 unaosema Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na moyo wa kiasi.

“Huu ni wakati wa kuendelea kuamini uwepo wa huruma za Mungu katika maisha ya mwanadamu. Tunao ujasiri tukijua kuwa Mungu hatuachi kamwe, hata kama itamaanisha kupitia mateso ya msalaba.

“Tunauona msalaba wa Yesu Kristo kama alama ya nguvu na tumaini letu. Tunaalika makanisa wanachama kuombeana hasa kwa nchi na makanisa ambayo yako katika kiini cha mlipuko wa virusi hivyo,” ilisema barua hiyo.

FMKD imeorodhesha maombi 12 ambayo wanachama wake watayaomba juu ya ugonjwa huo.

Mojawapo ya maombi hayo yalisema; “Uwe msaada wetu hasa wakati huu ambapo virusi vya corona vinazidi kusambaa ulimwenguni, uponye wagonjwa, uzisaidie na kuzilinda familia zao na marafiki ili wasiathirike. Ee Mungu, sikia kilio chetu.”

Makanisa na watumishi mbalimbali wa Mungu wanaendela kutoa wito wa kuomba juu ya ugonjwa huo ambao kwa hapa nchini tayari umesababisha kifo cha mtu mmoja huku wagonjwa wakiwa 20 ambao 17 kati yao, kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wanaendele vizuri wawili wakiwa wamepona.

COVID-19 ilianzia nchini China Desemaba mwaka jana na hadi sasa imeenea dunia nzima.

MJUE ADUI YAKO.

Watu wengi tuna hasira, uchungu, ghadhabu, maumivu, mapambano, chuki na kisasi na mashindano mengi moyoni, tukiamini kabisa kuna watu waliotusababishia hali hiyo, watu tunawaona wabaya, maadui, tunawaita wakarofi na majina mengi tuwezavyo kuwaita. Wanaweza kuwa watu wa mbali ama wa karibu, aweza kuwa mke au mume, mchumba au rafiki, jirani, mfanyakazi mwenzako, ama yeyote yule unayehisi kakukosea.
Lakini leo nataka nikuambie adui yako mkubwa wala si huyo unayemdhani, huyo ni msaidizi tu wa adui yako, adui yako yuko ndani yako mwenyewe, anayekuumiza, anayekutukana, anayekuadhibu, anayekunyanyasa yuko ndani yako na kwa kuwa umeshindwa kummudu ndio maana hasira zako na lawama zako umezihamishia kwa msaidizi wa adui yako ambaye ndio yule unayemdhania.

Umewahi jiuliza? Kabla hujachukia ndani yako lazima kuna sauti mbili zilishindana, moja ikakuambia usichukie nyingine ikakuambia haiwezekani utaonekana mjinga, ile sauti iliyoshinda ya ubaya ndiyo adui yako mkubwa, maana kinyume cha hapo wala usingefanya maamuzi hayo. Umemuadhibu bure mtu wa mbali lakini ulipaswa kumwadibisha mtu wako wa ndani kwa wema na hapo ungeweza kujisamehe kabla hujaadhibu unayedhani kakukosea.

Adui wa ndani ni mbaya kuliko wa nje, maana kama nje kukiharibika utakimbilia ndani kupata usalama, ila ndani kukiharibika jua huna pa kukimbilia, na huyo adui akikushinda kabisa atakuua au kukusababishia madhara mengi kiakili na kiafya, NDIO MAANA USISHANGAE MTU KAJIUA AU KAJIDHURU JUA KASHINDWA VIBAYA NA ADUI YAKE WA KARIBU AMBAYE NI YEYE MWENYEWE.

Biblia haijakosea inaposea LINDA SANA MOYO WAKO, KULIKO YOTE UYALINDAYO, MAANA HUKO NDIKO ZITOKAKO CHEMICHEMI ZA UZIMA. najua mpaka sasa adui wa ndani bado anakushawishi uupuuze ujumbe huu, ni lazima umshinde kama kweli unataka amani ya ndoa yako, kazi yako, jirani yako, ndugu zako nk. Ukimshinda adui wa ndani hakuna adui nje kamwe ila ukishindwa na adui wa ndani basi kila atakayekugusa iwe bahati mbaya au makusudi basi atakuwa adui yako.

Mungu akupe kuelewa haya

KIPIMO CHA IMANI

Tangu nimeokoka nimebahatika kusikia mafundisho mengi sana mazuri kuhusu imani, wakati mwingine nilijifunza kuwa huhitaji imani kubwa kung’oa mlima, na nilipoijaribu imani ndogo kung’oa mlima, mlima uliishinda imani yangu ndogo. Je! Wapi hasa nilikosea mpaka kushindwa kuung’oa mlima mkubwa kwa imani ndogo? ( nadhani nilihitaji imani inayokua kama mbegu ya haladali, mpaka kuzidi ukubwa wa mlima ndipo niung’oe)

Leo ninataka kukueleza kipimo cha imani yako kwa maelezo haya.

Kama imani yako ya kufa ni kubwa kuliko ya kuishi basi jua huna imani au imani yako ni haba, hivyo kikubwa lazima kishinde kidogo.

Kama imani yako ya kutokupona ina nguvu kuliko kupona basi huna imani, au imani yako haba na chenye nguvu kitashinda.

Kama imani yako ya kukosa ni hakika kuliko ya kupata basi imani yako ni ndogo hivyo kukosa kutashinda, na kama imani yako ya laana ni zaidi ya baraka nakuhakikishia kila utakapoongea, utakachowaza, utakachoota, utakacokiona na kukikiri kitakuwa ni laana, balaa, mikosi na chenye nguvu kwenye akili yako, moyo wako na kinywa chako ndicho kitakachoshinda na kutokea kwenye maisha yako.

Nadhani umeshajipima kwenye eneo lako, sasa ni kazi yako kuhakikisha unaifanya imani yako iwe kubwa kuliko, mlima, magonjwa, madeni, na mahusiano ndipo utakapoweza kubadilisha mwonekano wa kinachokutisha kwa imani. KUMBUKA CHENYE NGUVU, UZITO, NA UHAKIKA NDICHO HUSHINDA.
Wakati wewe unaona haiwezekani kuna watu imewezekana, tofauti yako na yao ni kile unachokiona kigumu wao walikiona chepesi. Iga mwenendo wao utafanikiwa
@official_evjohn
#victoriousyear2020

WAJIBU WAKO

UNAWAJIBIKA NA MAISHA YAKO MWENYEWE. “Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.” (Wagalatia 6:5) “Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari/hesabu zake mwenyewe mbele za Mungu.” (Warumi 14:12) “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.”
(Ezekieli 18:20)

Kwa msisitizo wa kipekee kabisa maandiko haya yanatuonesha kwamba kila mtu anawajibika na maisha yake mwenyewe. Hata mbele za Mungu hakuna atakaye hukumiwa kwa dhambi za mtu mwingine. Kwa maana hiyo hiyo basi hakuna anayewajibika na maisha ya mtu mwingine. Kwa mujibu wa maandiko haya ni makosa makubwa kuwa na MAWAZO TEGEMEZI, AKILI TEGEMEZI. Ile dhana ya KULAUMU WATU KWA SABABU HAWAJAKUSAIDIA inakemewa vikali na maandiko haya.
Simama upiganie maisha yako mwenyewe sio lazima watu wakusaidie hata kama uwezo wanao. Jukumu la kwanza la Baba yako ni kwa mke wake. Wewe ukishafika Miaka 18 unapaswa kuwaza kesho yako itakuwaje. Jukumu kubwa la Kaka na Dada zako ni maisha yao na watoto wao. Wewe sio jukumu lao. Acha kulaumu watu na usimame kutengeneza maisha yako mwenyewe.

Kama unataka kufunga Ndoa fanya unachomudu, usijiwekee bajeti kubwa kwa kuangalia mifuko ya watu. Kama hauna fedha achana na kusherekea Birthday, kunywa maji mshukuru Mungu. Kama umekosa kodi kalale kanisani saidiana na mlinzi ukiumwa mbu utapata akili ya kutafuta hela. Lakini usiwe mzigo kwa mtu yeyote na kulaumu na kuchukia watu. “Oh hawanisadii chochote!” Nani alikwambia unapaswa kusaidiwa!? KASIRIKA, CHUKIA, NUNA LAKINI UJUMBE NDIO UMEUPATA, PIGANIA MAISHA YAKO. KAMA AMBAVYO UTAHUKUMIWA KWA DHAMBI ZAKO MWENYEWE BASI VIVYO HIVYO AMUA KUFANIKIWA KWA JASHO LAKO MWENYEWE. -evjohn whatsup 0767386606
#2020

SIJAVIZOEA

SIJAVIZOEA.: 1 Samweli 17:38 Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii. 1 Samweli 17:39 Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, SIWEZI KWENDA na VITU HIVI, MAANA SIKUVIJARIBU (SIJAWAHI KUVITUMIA/SIJAVIZOEA). BASI DAUDI AKAVIVUA. 1 Samweli 17:40 AKAICHUKUA FIMBO YAKE MIKONONI, AKAJICHAGULIA MAWE LAINI MATANO KATIKA KIJITO CHA MAJI, AKAYATIA KATIKA MFUKO WA KICHUNGAJI ALIOKUWA NAO, MAANA NI MKOBA WAKE, NA KOMBEO LAKE ALIKUWA NALO MKONONI MWAKE, AKAMKARIBIA YULE MFILISTI. Mara nyingi huwa tunasubiri Mungu atupe wazo jipya la biashara au namna mpya ya utendaji ili tuweze kufanikiwa na tunasumbuka sana kuiga mifumo ya watu wengine na kuacha kuboresha kile ambacho tunakijua na kufanya kwa ubora tunasubiri wazo jipya na namna mpya ili kufanikiwa na kujikuta tunajichelewesha. Nimegundua mara nyingi sana Mungu huwa anatumia kile tunachokijua na kukiboresha ndipo hapo anatufanya kuwa bora na tofauti. Anamuuliza Musa “BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, NI FIMBO. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake.” (Kutoka 4:2-3) Kipawa hicho unachokidharau, huduma hiyo hiyo unayoichukulia kawaida, biashara hiyo hiyo ya kawaida, ujuzi na uwezo ulionao ndio Mungu huwa anatumia kukufanya kuwa Mkuu. Usitafute sana kubuni ndege nyingine wakati unaweza kuboresha hii iliyopo na ukatajirika. USIHANGAIKE KUFUNGUA CHAMPAGNE 🍾 NA VIDOLE WAKATI UMEZOEA KUFUNGUA SODA KWA MENO, TUMIA UJUZI WAKO, ANAYEKUONA MSHAMBA NI KWA SABABU ANA NAMNA YAKE YA KUFANYA. KUWA BORA KATIKA NAMNA YAKO. – Ev.john